Refa wa zamani wa soka aliyewahi pia kuwa Mwenyekiti wa Chama cha Soka
Mkoa wa Mara, Abdallah Majura Bulembo, ameibuka kidedea na kuwa
Mwenyekiti Mpya wa Jumuiya ya Wazazi wa CCM Taifa baada ya kuzoa kura
nyingi na kuwaacha mbali wapinzani wake John Barongo na Martha Mlacha
(Mbunge wa Viti Maalum CCM).
Akitangaza matokeo ya uchaguzi huo
jana, msimamizi wa uchaguzi huo uliofanyika mjini Dodoma, Steven
Wassira, alisema Bulembo ameshinda baada ya kuzoa kura 680 atashika
wadhifa huo kwa kipindi kijacho cha miaka minne.
Alisema kuwa
Martha Mlata alipata kura 190 na hivyo kumaliza katika nafasi ya pili
huku John Barongo akiambulia kura 42 tu na hivyo kuwa nyuma ya Bulembo
na Mlata.
Akizungumza baada ya kutangazwa kuibuka mshindi na
kutangazwa rasmi kuwa mwenyekiti wa Jumuiya hiyo, Bulembo aliyekuwa
akishangiliwa ukumbini mfululizo aliwashukuru wajumbe kwa kumpa ushindi
wa kishindo, lakini akawaasa baadhi ya watu walioshindwa kwenye uchaguzi
huo kukubaliana na matokeo ili kuendelea kukijenga chama chao.
"Miaka
minne iliyopita nilisimama pia mbele yenu hna kuwaomba kura, lakini
nikashindwa kwa vile kura hazikutosha... hata hivyo niliwashukuru sana
na kuahidi kurudi. Leo nimetimiza wajibu huo. Lakini nasikitika kuona
wenzangu ambao hawakusimama hapa," alisema Bulembo.
"Kura zao
hazikutosha, hawakusaini, wamekimbia, wanaanzisha ajenda mpya...
nawakumbusha kuwa katika Chama cha Mapinduzi (CCM) kuna kushinda na
kushindwa. Wakubali matokeo kama mimi nilivyofanya miaka minne
iliyopita," alisema Bulembo ambaye katika uchaguzi uliopita alishika
nafasi ya pili baada ya kuzidiwa kura na Balozi Athumani Juma Mhina
(sasa Marehemu) aliyetwaa nafasi hiyo.
Wengine waliofanya vizuri katika uchaguzi huo ni pamoja na Pandu Silima na Haji waliotwaa nafasi za ujumbe wa NEC-CCM kutokea Zanzibar huku wagombea wengine watatu wakiwamo Mussa Azzan Zungu, Jasson Rweikiza na Adam Malima wakitwaa nafasi ya ujumbe wa NEC-CCM kutokea Tanzania Bara.
Mbali
na kuwahi kuwa refa na Mwenyekiti wa Chama cha Soka Mkoa wa Mara
(MRFA), Bulembo pia aliwahi kuwa Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya
Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).
---
Taarifa via blogu ya Sraika Mkali
No comments:
Post a Comment