Serikali imetakiwa kuwa makini katika usajili wa Taasisi mbalimbali
hususan zinazohusiana na masuala ya dini ikiwa ni pamoja na kufuatilia
huduma za taasisi zilizosajiliwa nchini ili kudhibiti taasisi
zinazojisajili tofauti na kazi wanazofanya.
Aidha,
imetakiwa kuchunguza taasisi zote zinazofanya huduma na zile
zisizosajiliwa wasifanye shughuli yoyote mpaka wasajiliwe huku
wakidhibiti mapema taasisi au mtu ambaye ni hatari kwa nchi bila
kusubiri hali kuwa mbaya kwani inasababisha kuota mizizi na kusababisha
madhara kwa wasio na hatia.
Hayo
yalisemwa na Mkurugenzi wa Taasisi ya Tanzania Islamic Peace Foundation
(TIPF), Shekhe Sadik Godigodi alipozungumzia vurugu zilizojitokeza hivi
karibuni Dar es Salaam na Zanzibar huku akitaka polisi kuchukua hatua
zaidi kwa kuhakikisha vurugu zenye mrengo wa kidini zinafika mwisho.
Alisema
mara nyingi Serikali imekuwa ikielezwa kuhusu kundi la ‘Uamsho’
Zanzibar ambalo limesajiliwa kuwa linachochea vurugu ikiwa ni tofauti na
walivyosajiliwa lakini imekuwa ikisita kuwafutia usajili wao lakini kwa
matukio ya sasa iifike wakati kuwe na umakini zaidi kwenye usajili.
Alisema
kwa kitendo cha Jumuiya hiyo kuhisi kiongozi wao amechukuliwa na Polisi
na kufanya vurugu wameenda kinyume na dini ya Kiislamu inayotaka
kuchunguza na kuwa na uhakika kabla ya kuanza kudai haki kama kweli
unastahili, “Ukiangalia suala ya Shekhe Ponda amekuwa akisumbua serikali
kwa muda mrefu na kujiamulia mambo huku akisababisha vurugu kwa kutumia
taasisi ambayo haijasajiliwa lakini serikali imekuwa kimya bila
kumchukulia hatua, suala lililofanya kuota mizizi na kujiongezea wafuasi
kila kukicha,” alisisitiza.
Alitaka
Serikali kutowapuuza watu au vikundi kama hivyo ambavyo vinatishia
kuharibu uso wa nchi na kujenga chuki kwa jamii kwa mambo ambayo
yanaweza kushughulikia bila kusababisha migongano au kuchoma moto
makanisa.
Aliwapongeza Wakristo kwa
utiifu na kuheshimu sheria kutokana na uzalendo walioonesha na kuwasihi
kuendelea kuwa na moyo huku vyombo husika wakichukua sheria dhidi ya
wahalifu kwani yeye hafikirii kuwa hawana uwezo wa kulipiza kisasi bali
uvumilivu walionao ndio uliowafanya kutofanya hivyo.
---
via HabariLeo
No comments:
Post a Comment