Habari imeandikwa na Halima Mlacha na Anastazia Anyimike HabariLeo ---
UONGOZI wa
kiwanda cha Tanzania Pharmaceutical Industries Limited (TPI), umekana
kuzalisha ARVs bandia na kutaka waliohusika na udhalimu huo wachukuliwe
hatua kali kwa sababu ni wauaji.
TPI pia imesema haijapokea barua
kutoka Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii ya kuitaka kusitisha
uzalishaji wa dawa ya aina yoyote ili kupisha uchunguzi na kudai
imepokea barua kutoka Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) iliyowafikia
juzi ikiwapa siku 14 za kujieleza kabla ya kuchukuliwa hatua.
Naibu
Mkurugenzi Mtendaji wa TPI, Zarina Madabida alisema dawa hizo bandia
hazikutengenezwa na kiwanda hicho na zinazotengenezwa na kiwanda hicho
ni kimuundo, nembo na hata vifungashio. Kutokana na hali hiyo, Madabida
alisema anatilia shaka kuwapo mchezo mchafu wa kukiharibia kiwanda
chake.
Alisema nembo iliyo kwenye dawa bandia za ARVs ni TT-VR30
wakati dawa halisi ambazo zinatengenezwa na TPI nembo yake ni TT-VIR30.
Pia
vifungashio alisema ni tofauti ambapo wao wamekuwa wakitumia chupa
nyembamba na hata rangi yake imepauka ikilinganishwa na bandia. “TFDA
haijatuonesha sampuli walizokamata, ila wametuletea picha ya dawa hizo,
hata kwa macho ya mtu asiyejua kusoma lazima ataona tofauti.
“Nimeambiwa
vifungashio ni tofauti, kwani dawa bandia zimewekwa kwenye chupa pana,
zisizo na shingo na kifuniko kipana wakati chupa tunazotumia ni
nyembamba zenye shingo na mfuniko mwembamba,” alisema.
Akizungumza
huku akionesha utofauti wa dawa hizo, Madabida alisema teknolojia ya
kiwanda chake waliyochukua Thailand ni ya kutengeneza dawa za vidonge
vya kapsuli (vyenye umbo la yai) na vyenye rangi nyeupe na si vya duara
ambavyo vinatoa tabaka za rangi za dawa zilizotumika- nyeupe na chungwa.
“Teknolojia
iliyotumika kutengenezea dawa bandia kwenye kiwanda chetu haipo na sisi
hatuwezi kusambaza dawa ambazo hatuzalishi kwenye kiwanda chetu. Dawa
hizo hazikukutwa kwenye kiwanda chetu, hivyo ni dhahiri aliyefanya hivyo
alikuwa na dhamira mbaya kwa Watanzania. “Ni kitu ambacho hakiingii
akilini mtu uzalishe bidhaa wewe peke yako halafu ujitengenezee tena
bidhaa bandia! Sisi ni ndio pekee tunaotengeneza ARVs nchini, hivyo
tusingeweza kuzalisha kitu bandia. Mara ya mwisho kuiuzia MSD dawa ni
Machi na Aprili mwaka jana, iweje hizo bandia zikutwe Agosti mwaka huu,
tena Tarime?” Alihoji Madabida.
Alisema tangu kuanzishwa kwa
kiwanda hicho ambacho kina ubia na Serikali yenye hisa asilimia 40,
wamezalisha dozi milioni 2.28 za ARVs na kuhoji iweje leo wazalishe dawa
hizo bandia za dozi 8,000.
Madabida alisema baada ya Agosti 6
kupokea malalamiko kutoka TFDA ya kupatikana kwa dawa bandia, walikutana
na Mamlaka husika na kukubaliana kuwa wakati suala hilo linachunguzwa,
dawa hizo ziondolewe kwenye mzunguko kwa lengo la kunusuru watumiaji.
Alisema
pamoja na makubaliano hayo, lakini mpaka Agosti 28 hakuna
kilichofanyika jambo ambalo TPI iliamua kuiandikia Mamlaka hiyo barua ya
kuwakumbusha hatua hiyo, “Wana malengo yasiyo mazuri kwetu, na wanajua
tuko katika mchakato wa kupata kibali cha WHO (Shirika la Afya la
Kimataifa) ambapo tutafanya biashara ndani na nje ya nchi. Hatutaacha
jiwe lolote lirushwe mpaka hapo wahalifu wakamatwe na haki itendeke,”
alisema.
Wizara yakomaa Ofisa Habari wa Wizara ya Afya na Ustawi
wa Jamii, Nsachris Mwamwaja alipoulizwa, alisema Waziri hawezi kusema
wamekifungia kiwanda bila kuwaandikia barua, “Sisi tumepeleka barua kama
haijamfikia hilo ni jambo lingine.”
Hata hivyo, Mwamwaja alisema
hana uhakika kama barua kutoka TPI imeshamfikia Waziri, kwa sababu yuko
nje ya ofisi na kusisitiza kuwa suala la kukana dawa bandia linafanyiwa
uchunguzi na hivyo hayuko tayari kulizungumzia.
Juzi Waziri wa
Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Hussein Mwinyi alitoa agizo la kukifungia
kiwanda hicho kuzalisha aina yoyote ya dawa ili kupisha uchunguzi wa
vyombo vya usalama kuhusu uzalishaji wa dawa bandia.
Kuwapo kwa
dawa bandia za ARVs kulibainika Agosti kwenye Hospitali ya Tarime, huku
Baraza la Watu Wanaoishi na Virusi Vya UKIMWI likidai kuwa dawa hizo
zimesambazwa katika mikoa ya Mara, Tanga na Dar es Salaam tofauti na
kauli ya Serikali kuwa ni Tanga, Iringa na Mwanza.
Kutokana na hali hiyo, Baraza hilo liliitaka Serikali kuchukua hatua dhidi ya wahusika.
No comments:
Post a Comment