MAMLAKA ya Bandari Tanzania (TPA), imetajwa kuongoza kwaviashiria vya
rushwa katika ununuzi wa bidhaa na huduma unaosimamiwa na Mamlaka ya
Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA).
Mkurugenzi
Mtendaji wa PPRA, Ramadhani Mlinga alisema hayo jana wakati akizungumza
na waandishi wa habari kuhusu ukaguzi wa ununuzi katika taasisi za umma
uliofanyika hadi Juni 30.
Mlinga
alisema walipotumia kanuni za kupima rushwa katika ununuzi, TPA
ilibainika kuongoza miongoni mwa taasisi za umma zilizokutwa na viwango
vya juu vya uwezekano wa kuwapo rushwa kwa zaidi ya asilimia 20 ya
shughuli za ununuzi.
Mbali na TPA
iliyokuwa na asilimia 44 ya viashiria vya rushwa, ilifuatiwa kwa karibu
na Wizara ya Mambo ya Ndani katika mradi wa ujenzi wa makao makuu ya
kikosi cha Zimamoto iliyokuwa na asilimia 41 ya viashiria vya rushwa.
Taasisi
ya tatu kwa kuwa na viashiria vingi vya rushwa kwa mujibu wa PPRA, ni
Wizara ya Maji na Umwagiliaji katika mradi wa maji Chalinze iliyokuwa na
asilimia 40.
Nyingine ni Halmashauri
ya Wilaya ya Kyela (28%), Halmashauri ya Wilaya ya Makete (27%),
Halmashauri ya Jiji la Mbeya (28%), Halmashauri ya Wilaya ya Tabora
(20%), Halmashauri ya Wilaya ya Bukombe (28%), Chuo cha Usafirishaji cha
Taifa (27%) na Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga (23%) Kuhusu ukaguzi
wa miradi kwa thamani ya fedha, Mlinga alisema kati ya miradi 137
iliyokaguliwa, ni miradi 63 tu ndiyo ilitekelezwa kwa thamani ya fedha
na kwa mujibu wa mkataba.
Alisema
asilimia 49 ya miradi hiyo, utekelezaji wake ulikuwa wa wastani ambapo
miradi saba sawa na asilimia 5, utekelezaji wake haukuridhisha kabisa.
Shilingi bilioni 2 zayeyuka
Kuhusu
malipo yanayotia shaka, Mlinga alisema ukaguzi huo umebaini kuwa kuna
taasisi kumi zilizofanya malipo yenye shaka ya Sh bilioni 2.1 kwa
makandarasi.
Alitaja taasisi hizo kuwa
ni Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa, Halmashauri ya Wilaya ya Ulanga,
Halmashauri ya Wilaya ya Kilombero, Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya na
Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro.
Nyingine
ni Halmashauri ya Manispaa ya Sumbawanga, Halmashauri ya Mji wa Kibaha,
Wakala wa Vizazi na Vifo (RITA), Mfuko wa Akiba kwa Wafanyakazi wa
Serikalini (GEPF) na Halmashauri ya Wilaya ya Chato.
SUMA JKT yafungiwa
Mlinga
alisema PPRA pia imefungia kampuni nne kushiriki zabuni zinazotangazwa
na taasisi za umma kwa mwaka mzima baada ya kushindwa kutekeleza
masharti ya mikataba yao katika zabuni walizowahi kupewa na kusababisha
mikataba yao kuvunjwa.
Kampuni hizo ni
pamoja na Shirika la Uzalishaji JKT (SUMA JKT) ya Dar es Salaam, Vector
International ya Mwanza, Shy Builders Limited ya Shinyanga na Earthline
Construction Limited ya Bukoba.
---
via HabariLeo
No comments:
Post a Comment