Na Mwandishi Wetu, Dodoma
SERIKALI imeshauriwa kubadili
utaratibu wa matibabu kwa Maofisa Waandamizi ili kuwawezesha kunufaika
na huduma za matibabu kupitia Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya.
Ushauri huo umetolewa na Wakuu wa
Mikoa na Wakuu wa Wilaya mjini Dodoma katika kikao kazi cha siku tatu
ambacho kiliongozwa na Waziri Mkuu Mizengo Pinda.
Wamesema kuwa utaratibu wa sasa
ambao unaonesha kuwa matibabu ni moja ya stahiki zao unawazuia Wakuu hao
kunufaika na huduma za matibabu kupitia NHIF ambazo walisema
zimeboreshwa sana kwa sasa na zina mtandao mkubwa unaowezesha kupata
huduma mahali popote nchini.
Akichangia mada iliyowasilishwa na
NHIF kwa wakuu hao, Mkuu wa Wilaya ya Kalambo, Moshi Chang’a alisema
kuwa “Tunataka kuwa wanachama wa NHIF hata sasa ila kinachotubana ni
hizo stahiki ambazo tumepewa ikiwemo ya matibabu kulipiwa na Serikali,
ipo haja sasa ya Serikali kupeleka fedha NHIF ili sisi tutibiwe na
Mfuko,” alisema Chang’a.
Alisema kuwa ni vyema wakajiunga
na NHIF ambayo itawasaidia kunufaika na fao la wastaafu lakini pia
itawapa hamasa kubwa katika uhamaishaji kutokana na ukweli kwamba
watakuwa miongoni mwa watumiaji wa huduma hizo.
Akijibu hoja hiyo, Waziri Mkuu
Mizengo Pinda alisema kuwa kwa sasa wakuu hao wanaweza wakajiunga wakati
Serikali ikiliangalia suala hilo ili liwe kwenye utaratibu wanaoutaka.
Akitoa maelezo ya awali kwa
viongozi hao, Mkurugenzi Mkuu wa NHIF, Emanuel Humba alisema kuwa ili
Mfuko ufanikiwe kuwafikia Watanzania wengi kama nchi zingine
zilizofanikiwa katika suala hilo ni lazima viongozi wakawa wanachama au
wanufaika wa huduma za Mfuko.
“Nchi zilizofanikiwa kuwaingiza
wananchi wake kwenye utaraibu wa Bima ya Afya kama Ufilipino, Korea,
Rwanda viongozi wake Wakuu ni wanachama wa Mifuko hiyo… hivyo nanyi
wakuu wetu mkijiunga itakuwa ni kazi rahisi kufikia malengo yetu,”
alisema Humba.
Aidha aliwaomba wakuu hao
kuhakikisha wanafuatilia fedha zinazolipwa na NHIF katika Vituo vya
Kutolea huduma kwenye maeneo yao ili zisaidie kuboresha huduma za
matibabu ikiwemo ununuzi wa dawa na Vifaa tiba.
Katika suala hilo la Malipo,
Waziri Mkuu aliutaka Mfuko kuweka utaratibu wa kuwapa taarifa za fedha
viongozi wakiwemo Wakuu wa Mikoa, Wilaya, wabunge ili waweze
kuzifuatilia katika matumizi yake.a
No comments:
Post a Comment