Monday, April 1, 2013

TAMKO LA KAGASHEKI HALITAADILIKA-WIZARA

Wizara ya Maliasili na Utalii imefafanua kuwa tamko alilolitoa Waziri, Balozi Khamis Kagasheki kuhusu kupunguza eneo la pori tengefu la Loliondo halitakubalika na kuwa tamko hilo lililotolewa, limetolewa na mamlaka ya kisheria.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo na msemaji wa Wizara hiyo, George Matiko, ni kuwa tamko hilo limetolewa kutokana na maoni yaliyotolewa na baadhi ya watu kupitia vyombo mbalimbali vya habari, kuwa uamuzi alioufanya kuhusu pori tengefu la Loliondo, si sahihi kwa kuwa hautafuata sheria wala matokeo ya utafiti.

Taarifa hiyo imeeleza kuwa, Waziri Kagasheki alifuata sheria alipotoa tamko kuhusu kupunguza eneo la pori tengefu la Loliondo, kutoka kilometa za mraba 4,000 hadi 1,500 na kuliacha eneo kilometa za mraba 2,500 litumiwe na wananchi.

Taarifa hiyo imeongeza kuwa, Waziri alifanya hivyo kwa mujibu wa Sheria ya Wanyamapori namba 5 ya mwaka 2009, na kuwa sheria hiyo, inampa Waziri mwenye dhamana, uwezo wa kupitia upya, mapori tengefu na kufanya marekebisho mbalimbali muhimu kwa manufaa ya wananchi bila kuathiri uhifadhi.

Pia, taarifa hiyo imeeleza kuwa, waziri alifanya uamuzi huo kwa kuzingatia taarifa mbalimbali za utafiti na uchunguzi, ambazo ziliwahi kufanywa na Taasisi ya Utafiti wa Wanyamapori (TAWIRI) kwa kuzingatia mapendekezo ya tume mbalimbali zilizoundwa kuchunguza mgogoro uliokuwepo.

Hivi karibuni, baadhi ya wananchi na viongozi Halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro walipinga uamuzi wa Serikali wa kuwapa sehemu ya pori tengefu la Loliondo wakidai sehemu iliyomilikiwa na Serikali ndiyo yenye huduma muhimu.

Taarifa ya Wizara/Serikali aliyoitoa Waziri Balozi Kagasheki ni hii ifuatayo:
Picture
Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Balozi Khamis Kagasheki akisisitiza jambo kwa waandishi wa habari juu ya msimamo wa serikali juu ya mgogoro wa muda mrefu kwenye Pori Tengefu la Loliondo, leo jijini Dar es Salaam.

SERIKALI KUGAWANA NA WANANCHI ENEO LA PORI TENGEFU LOLIONDO

Wizara ya Maliasili na Utalii imekusudia kurekebisha mipaka na ukubwa wa eneo la Pori Tengefu la Loliondo kutoka kilomita za mraba 4,000 hadi 1,500 ili kumaliza migogoro ya muda mrefu inayotoka na mwingiliano wa matumizi ya ardhi katika eneo hilo.

Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam, Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Balozi Khamis Kagasheki amesema serikali imefikia uamuzi huo kama njia bora ya kumaliza tatizo hilo kiserikali.

“Ili kutatua migogoro iliyopo, kunusuru ikolojia ya Hifadhi za Serengeti, Ngorongoro na pori Tengefu Loliondo, Serikali itameamua kutoa kilomita za mraba 2,500 kuwapa wananchi kuwa vijiji na wa kilometa za mraba 1,500 zitabaki serikalini na kuendelea kuwa na hadhi ya Pori Tengefu kwa ajili ya kulinda mazalia ya wanyamapori, mapito na vyanzo vya maji kwa ajili ya ustawi wa hifadhi na Taifa,’’ anasema Mhe. Kagasheki.

Mhe. Waziri aliongeza kuwa Serikali itawawezesha wananchi kuanzisha Jumuiya la Hifadhi ya Wanyamapori katika ardhi ya kijiji, na mipango ya matumizi Bora ya Ardhi ya vijiji katika eneo la Loliondo utaandaliwa na kuambatana na huduma za mifugo ndani ya vijiji.

Mhe. Kagasheki aliongeza kuwa Pori Tengefu la Loliondo ni eneo la serikali kisheria lakini baadhi ya vijiji wamelichukua na kulifanya kuwa lao na wengine wameingia mikataba na makampuni binafsi yanayofanya shughuli za uwindaji na utalii wa picha bila kufuata taratibu.

“Serikali imeona tatizo la ardhi kwa wanavijiji waliopo kwenye Pori Tengefu la Loliondo ndio maana limeamua kugawa eneo la ardhi kwao. Hata hivyo, nasisitiza sehemu ya vyanzo vya maji, mazalia ya wanyamapori na mapito ya wanyama katu serikali haitakubari kuwapa wananchi,” anasema Mhe. Kagasheki.

Mhe. Waziri anasema utekelezaji wa uamuzi huo unaanza mara moja kwa kushirikiana na Aidhana Wizara ya Mifugo itakayoandaa na ukubwa wa eneo la malisho lililopo katika kijiji pamoja na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi ili kuona uhalali wa Kampuni zinazomiliki ardhi katika eneo lililohifadhiwa kwa madai kuwa wameuziwa na serikali za vijiji.

Aidha, Mhe. Kagasheki alisema, Serikali iko tayari kuangalia upya eneo kubwa lililotolewa kwa Ottelr Business Corporation ili kuona jinsi linavyoweza kupunguzwa ili wananchi wapate maeneo ya kufanyia shughuli zao na si kumfukuza mwekezaji huyo.

TAARIFA YA WIZARA YA UFAFANUZI KUHUSU TAMKO LA WAZIRI KAGASHEKI KUHUSU ENEO LA PORI TENGEFU LA LOLIONDO

JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
WIZARA YA MALIASILI NA UTALII

TAARIFA KWA UMMA

UFAFANUZI KUHUSU TAMKO LA WAZIRI KAGASHEKI KUHUSU ENEO LA PORI TENGEFU LA LOLIONDO

TAMKO HALITABADILIKA
Wizara ya Maliasili na Utalii imefafanua kuwa tamko alilolitoa Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe Khamis Kagasheki mbele ya waandishi wa habari tarehe 26 Machi 2013 kuhusu kupunguza eneo la Pori Tengefu la Loliondo halitabadilika na kuwa alilitoa kutokana na mamlaka ya kisheria aliyo nayo.

Ufafanuzi huu umetolewa kutokana na maoni ya baadhi ya watu waliyoyatoa kwa njia ya mtandao na kwenye vyombo vingine vya habari kuwa uamuzi uliofanyika kuhusu Pori Tengefu la Loliondo si sahihi kwa kuwa haukufuata sheria wala matokeo ya utafiti. Maoni hayo si sahihi.

TAMKO NI KWA MUJIBU WA SHERIA
Ukweli ni kuwa Waziri Kagasheki alifuata sheria alipotoa tamko kuhusu kupunguza eneo la Pori Tangefu la Loliondo kutoka  kilomita za mraba 4,000 hadi 1,500 na kuliacha eneo la kilomita za mraba 2,500 litumiwe na wananchi. Alifanya hivyo kwa kwa mujibu wa Sheria ya Wanyamapori Namba 5 ya Mwaka 2009, Sehemu ya 16 Vifungu Na. 4, 5 na 6. Sheria hiyo inampatia Waziri mwenye dhamana uwezo wa kupitia upya mapori tengefu na kufanya marekebisho mbalimbali muhimu kwa manufaa ya wananchi bila kuathiri uhifadhi.

Aidha, Waziri alifanya uamuzi huo kwa kuzingatia taarifa mbalimbali za utafiti na uchunguzi ambazo ziliwahi kufanywa na Taasisi ya Utafiti wa Wanyamapori (TAWIRI). Pia alizingatia mapendekezo ya tume mbalimbali zilizoundwa kuchunguza mgogoro uliokuwapo.

Mojawapo ya tume hizo ni Tume  ya  Waziri Mkuu ya mwaka 2010 ambayo ilijumuisha wajumbe kutoka wizara 9, Mkoa wa Arusha na Wilaya ya Ngorongoro. Pamoja na mambo mengine Tume hiyo ya Waziri Mkuu ilipendekeza kuwa kuna umuhimu wa kupunguza eneo la Pori Tengefu la Loliondo bila kuathiri mapito ya wanyamapori, na vyanzo vya maji.

Vilevile, kwa muda mrefu viongozi wa Wizara wamekuwa wakikutana na wananchi na viongozi wa Mkoa wa Arusha na Wilaya ya Ngorongoro kujua kero zilizopo ili zitatuliwe. Mikutano hiyo imemwezesha Waziri Kagasheki kufanya uamuzi alioufanya wa kuligawa eneo hilo la Pori Tengefu la Loliondo.

UMUHIMU WA PORI TENGEFU LA LOLIONDO
Wizara inasisitiza kuwa eneo la kilomita za mraba 1,500 litaendelea kuwa Pori Tengefu na kumilikiwa na Wizara kwa mujibu wa Sheria ya Uhifadhi wa Wanyamapori namba 5 ya mwaka 2009 kwa sababu zifuatazo:
  • Ni sehemu ya mazalia ya wanyamapori;
  • Ni sehemu ya mapito ya wanyamapori;
  • Ni vyanzo vya maji.
Kwa ajili hiyo eneo hilo litaendelea kuwa chini ya Wizara, kwa kuwa linachangia kwa kiwango kikubwa kuimarisha mfumo-ekolojia wa Serengeti.

MASLAHI YA WANANCHI YANAZINGATIWA
Wizara imesisitiza pia kuwa ardhi iliyobaki baada ya kuondoa eneo la Pori Tengefu la Loliondo itasimamiwa na vijiji kwa mujibu wa Sheria ya Ardhi ya Vijiji Namba 5 ya Mwaka 1999. Vilevile Wananchi watawezeshwa ili waanzishe Eneo la Jumuiya ya Hifadhi ya Wanyamapori (WMA) katika ardhi hiyo kwa manufaa yao.

Tanzania inajali uhifadhi lakini pia inajali maslahi ya wananchi, ndiyo maana asilimia 25 ya eneo la nchi hii limehifadhiwa bila kuwepo migogoro. Hakuna migogoro kati ya wananchi na Serikali, kwa kuwa wananchi wanatambua umuhimu wa uhifadhi kwao na kwa vizazi vijavyo. Ndiyo maana wananchi wanachangia kwa kiwango kikubwa katika kufanikisha uhifadhi.

Pale ambapo kunajitokeza mgogoro kuhusu uhifadhi Serikali na wadau husika hujadili na kufikia mwafaka. Hivyo ndivyo ilivyokuwa kwa Loliondo, ndiyo maana kilomita za mraba 2,500 zimemegwa na kukabidhiwa wananchi.

WANAHARAKATI WANACHOCHEA MGOGORO
Tatizo la Lolindo, tofauti na maeneo mengine ya hifadhi, ni kuwa mgogoro uliopo unachochewa na wanaharakati na mashirika yasiyo ya kiserikali (NGOs), mengi yakiwa yanatoka nje nchi. Hata hivyo, ajenda yao ya siri imeshagundulika na haitaifanya Serikali kufanya uamuzi kinyume cha sheria za nchi na maslahi ya wananchi.

Wananchi wa Loliondo wametakiwa kupuuza mbinu za wanaharakati ambazo hazina maslahi kwao, wala kwa uhifadhi na taifa kwa ujumla.

[MWISHO]

George Matiko
MSEMAJI
WIZARA YA MALIASILI NA UTALII
Simu +255 784468047                      
1 Aprili 2013

No comments:

Post a Comment