Na Mwandishi wa Thehabari.com
SEKRETARIETI mpya ya Chama Cha
Mapinduzi (CCM) iliyoingia madarakani hivi karibuni chini ya uongozi wa
Rais Jakaya Kikwete, imesema itahakikisha vitendo vya rushwa hasa kwenye
chaguzi za chama hicho vinakoma mara moja, tofauti na ilivyokuwa
imezoeleka.
Kauli hiyo ya viongozi wa juu wa
CCM, Mwenyekiti Taifa (Rais Kikwete), Makamu Mwenyekiti Tanzania Bara
(Phillip Mangula) na Katibu Mkuu (Abdulrahman Kinana) imetolewa jana na
viongozi hao wakati wakizungumza na wana-CCM Mkoa wa Dar es Salaam
katika mkutano wa kumpongeza Rais Kikwete kuchaguliwa kushika nafasi
hiyo tena.
Akizungumza na umati wa
wanachama hao, Rais Kikwete aliwataka viongozi wapya kufanya kazi ya
ziada ya kuhakikisha wanarejesha imani ya Watanzania kwa CCM, ambayo
haiko kama ilivyokuwa zamani.
“Lazima kujiuliza nini
kimekifanya chama hiki kufikia hapo kilipo na kuangalia nini cha kufanya
ili kuondokana na hali hiyo. Pale mnapohisi hali ya kuungwa mkono
inapungua lazima tujiulize, kulikoni..! Nini cha kufanya ili kuimarisha
chama,” alisema na kuongeza kuwa kazi nyingine ni kuhakikisha
wanakijenga chama na kuimarisha zaidi ili kiendelee kuwaongoza
Watanzania.
“Chama chetu hakifanyi
mikutano…wenzetu wanafanya kwanini sisi hatufanyi, sasa tutatengeneza
utaratibu maalumu kuhakikisha viongozi wa chama kwa nafasi zao wanafanya
kazi yao ipasavyo ndani na nje ya chama,” alisema Rais Kikwete.
Alisema ipo haja ya kujipanga na
kuangalia namna ya kupambana na propaganda hasi za baadhi ya vyombo vya
habari na wapinzani ili kukabiliana na hali hiyo. Aliwataka wanaCCM
kuacha makundi na chuki ambayo yamekuwa yakikigawa chama hicho.
Awali akizungumza Kinana alisema
vitendo vya rushwa ndani ya CCM watahakikisha vinakoma mara moja ili
kurejesha imani ya Watanzania iliyopungua kutokana na tuhuma za wachache
dhidi ya vitendo viovu.
Alisema chini ya uongozi wake
atahakikisha mashaka yaliotawala kwa wananchi dhidi ya CCM yanaondoka
kwa kuwaengua wale wanaoendeleza vitendo vya rushwa, majumbu na vitendo
vinavyo leta sifa mbaya ya chama hicho.
“Hatuwezi kuiongoza nchi yetu
wakati watu wanamashaka na sisi, lazima tuondoe mashaka akisimama
mwana-CCM wote waseme naam huyu anaweza kusema…sio akisimama mwana-CCM
kusema watu wanahoji haaah, na huyu naye anakemea rushwa?
Aliwataka wana-CCM kushirikiana
katika kukisafisha chama na si kuwaachia viongozi jukumu hilo, ambalo
wao kama viongozi wamekubali kuongoza mapambano hayo.
Alisema CCM ina wanachama
milioni 5 ambao asilimia 99.9 wengi wakiwa ni masikini na waadilifu huku
asilimia 0.1 wakiwa ni wala rushwa wakubwa, wapenda mizengwe,
wapendeleaji hivyo kujikuta idadi hiyo ikikichafua chama chote jambo
ambalo alisema chini ya uongozi wao hawawezi kuacha hali hiyo iendelee.
Alisema atahakikisha anasimamia
ilani ya chama vizuri huku kanuni mbalimbali zikifuatwa ili kuleta haki
ndani ya chama hicho, alisema kuna kazi kubwa ya kukijenga chama hicho,
Alisema pamoja na viongozi
wenzake watahakikisha baadhi ya wana-CCM waliokuwa na tabia za mizengwe
pamoja na kupanga safu za viongoli ili kubebana kimaslahi inatoweka,
hivyo kumtaka kila mwanachama afanye kazi ya kumuingizia kipato na si
kutegemea kunufaika na nafasi ya uongozi.
Naye Makamu Mwenyekiti Bara,
Mangula alisema wapo baadhi ya viongozi wameingia ndani ya chama kwa
rushwa na tayari malalamiko juu ya mizengwe ya uchaguzi wa chama hicho
uliofanyika yamewafikia, hivyo kwa sasa wataanza kupitia kwa kina kila
malalamiko na atayebainika kuingia kwa rushwa ataenguliwa bila
kumuogopa.
“Tunajipa miezi sita ndani ya
miezi sita walioingia kihalali wataendelea lakini walioingia hovyo hovyo
‘out’…walioingia kwa pesa nje, hata wale waliokuwa wanatumwa vibahasha
nao tukiwajua wale nje, hatukubali chama chetu kituhumiwe kwa rushwa,
wala hatuta ngoja ushahidi sijui wa TAKUKURU, Polisi hakuna
tutakisafisha Chama Cha Mapinduzi,” alisema.
“…Lakini na nyingi mliokubali
kununuliwa kama sambusa mlifanya makosa, tusikubali tena…kwanini mtu
ukubali kuthaminishwa kama sambusa?,”
No comments:
Post a Comment