Chama Cha Mapinduzi kinasikitishwa na kitendo cha kinyama alichofanyiwa
Sheikh Fadhili Soraga cha kumwagiwa tindikali sehemu ya uso na kifuani.
Sheikh Soraga ni mtu maarufu hapa Zanzibar kwani huwa anashiriki katika
shughuli mbali mbali za kidini hapa nchini, yeye ni Katibu wa Mufti Mkuu
wa Zanzibar. Sheikh Soraga amefanyiwa unyama huo na watu
wasiojuulikana wakati akitoka kwenye mazowezi ya viungoasubuhi ya leo.
Sheikh
Soraga ni miongoni mwa masheikh wachache hapa zanzibar wenye
kuheshimika na kueleweka. Hivi karibuni Sheikh Soraga alitoa hutuba
nzuri na fasaha kwenye sala ya Eid-Haji juu ya kuimarisha amani na
utulivu katika visiwa vyetu vya Zanzibar na Tanzania kwa ujumla. Khutba
hiyo aliitoa mbele ya viongozi wakubwa wakitaifa waliohudhuria katika
sala hio, miongoni mwa viongozi hao ni pamoja na Rais wa Zanzibar na
Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mh. Dk. Ali Mohamed Shein, Makamo wa
kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharifu Hamadi, Rais Mstaau wa
awamu ya sita wa Zanzibar Dk. Amani Abeid Karume .a viongozi wengine
kadhaa.
Siku hiyo hiyo katika Baraza la
Iddi lililofanyika katika Ukumbi wa Salama Bwawani Sheikh Soraga wakati
akitoa khutba ya utangulizi aliwaasa tena wazanzibari na watanzania kwa
ujumla juu ya umuhimu wa amani, lakini katika hafla hiyo Sheikh Soraga
alikwenda mbali zaidi kwani alitoa takwimu za hasara iliyoipata Serikali
ya Mapinduzi ya Zanzibar na Jamhuri ya Muungano, mashirikaya watu
binafsi na ya Umma, taasisi za Kidini pamoja na vyama vya Siasa hasa
Chama Cha Mapinduzi kufuatia vurugu mbali mbali zilizokuwa zikifanywa na
Uamsho.
Vitendo vya kumwagiwa watu
tindikali hapa Zanzubar vimeanza siku nyingi. Kama tutakumbuka mnamo
mwaka 1995 Kada wa Chama Cha Mapinduzi ndugu Ali Mwinyi Msuko alimwagiwa
tindikali na watu wasiojuulikana huko Wete Pemba, mwaka 2007 wakati
zoezi la uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapigakura huko Pemba Sheha
mmoja alimwagiwa tindi kali, na mwaka uliopita Ndu. Rashid Ali
Juma Mkurugenzi wa Baraza la Mji wa Zanzibar nae alimwagiwa tindikali
na watu wasiojuulikana na leo hii Sheikh Fadhil Soraga Katibu wa Mufti
Muu wa Zanzibar nae amemwagiwa tindikali pia na watu wasiojuulikana.
Chama
Cha Mapinduzi kinasema kimechoka kusikia vitendo hivi vya kinyama vya
kumwagiwa watu tindikali na watu wasiokuulikana. Tunaviomba vyombo vya
Dola kuwatafuta watu hawa waovu wasio na huruma na wenzao ili wakamatwe
waweze kufikishwa kwenye vyombo vya Sheria, na kama Jeshi letu la Polisi
uwezo wake ni mdogo wa kuuwafichua wahalifu hawa basi ni vyema wakaomba
msaada kwenye vyombo vya upelelezi vya Kimataifa kama vile INTAPOL.
Mwisho
Chama Cha Mapinduzi kinawaomba wananchi wote wapenda amani na utulivu
kumuombea duwa Mwalimu wetu Sheikh Fadhil Soraga Mwenyezi Mungu ampe
moyo wa subira yeye na familia yake na amjaalie wepesi ili apone haraka.
Sheikh Soraga hivi sasa amesafirishwa kupelekwa Muhimbili kwa Matibabu
zaidi.
“KIDUMU CHAMA CHA MAPINDUZI’
MAPINDUZI DAIMA
Issa Haji Usssi Gavu
Katibu wa Kamati Maalum ya NEC
Idara ya Itikadi na Uenezi
No comments:
Post a Comment