MBUNGE wa Singida Mashariki, Tundu Lissu (Chadema) amemtaka Rais Jakaya
Kikwete kufuta haraka uteuzi wa baadhi wa majaji, akisema hawana sifa na
kwamba kinyume cha hapo, atawasilisha bungeni hoja maalumu ya
kumshitaki Rais.
Aidha, amemtaka Spika,
Anne Makinda kutangaza bungeni uchunguzi uliofanywa dhidi yake na
Kamati ya Bunge ya Haki, Maadili na Madaraka inayoongozwa na Mbunge wa
Mlalo, Brigedia Jenerali Hassan Ngwilizi baada ya kutoa tuhuma bungeni
dhidi ya majaji.
Alisisitiza kuwa umma
unapaswa kujua ukweli, kwani baada ya baadhi ya viongozi waandamizi wa
Serikali kukanusha bungeni na hatimaye kuundwa kamati, sasa ni wakati
ukweli ujulikane, huku akitamba kuwa ana uhakika na alichokisema.
Alisema
hayo katika ofisi ya Kambi ya Upinzani bungeni mjini hapa jana
akisisitiza kuwa majaji anaowalalamikia wamo vihiyo, wasio na maadili na
wengine uteuzi wao umekiuka Katiba ya nchi.
Alisema
mmoja wa majaji anaotaka aondolewe hana sifa za kielimu kuwa Jaji,
akisema hana Shahada ya Kwanza katika Sheria, huku akiongeza kuwa Jaji
huyo wa Mahakama ya Rufani nchini kwa sasa ameingia darasani kusomea
Shahada ya Sheria.
“Kama hana hata Shahada ya Sheria, anakaaje mahakamani, anatoaje haki kwa mujibu wa sheria ambayo hajasomea?”
Alihoji na kuongeza kuwa wengine wawili si waadilifu, akisema waliwahi kukamatwa wakihonga mahakimu wakati huo wakiwa mawakili.
“Majaji
wa aina hiyo watamtendea nani haki. Nani ambao watakuwa na imani
mashauri yao yatakapofika mbele yao? Mfumo wetu wa utoaji haki uko
salama kiasi gani na majaji wa aina hii?”Aliendelea kuhoji.
Lissu,
ambaye pia ni Mnadhimu wa Kambi ya Upinzani Bungeni, alidai pia wamo
majaji wasiojua kuunda hata sentensi moja kwa lugha ya Kiingereza, huku
akimtaja mmoja kuwa alipata ujaji miaka mitatu baada ya kuhitimu Shahada
yake Chuo Kikuu Huria na kuanza kazi, ilhali utaratibu unataka awe
amefanya kazi angalau miaka 15.
Wengine
aliodai hawastahili kufanya kazi za ujaji ni majaji wastaafu wanaofanya
kazi kwa mikataba, lakini bila kuapa. Alidai kuwa karibu majaji wote
walioongezwa mkataba na kuanza kazi bila kuapa tena, wanafanya kazi
kinyume cha sheria.
Aliongeza kudai
kwamba kutokana na uzito wa kashfa hizo, Rais Kikwete afute uteuzi wao
haraka iwezekanavyo, vinginevyo ataanzisha mchakato wa kuwasilisha hoja
maalumu ya kumjadili Rais na uteuzi wa majaji.
Alisema
ili kutimiza azma yake, anapaswa kukusanya asilimia 20 ya saini za
wabunge, sawa na wabunge kati ya 70 na 72, ili kuwasilisha hoja kwa kuwa
sasa kanuni haziruhusu kumjadili Rais ndani ya Bunge bila hivyo.
Aliongeza
kuwa, njia pekee ya kumaliza tatizo hilo ni kwa Rais kutengua uteuzi
wao, “Hatuwezi kuwa na Mahakama chafu yenye majaji vihiyo, wasio na
maadili na ambao wananchi wanakosa imani nao.”
Aidha,
Lissu alidai kuwa, mmoja wa majaji mwenye jina kubwa nchini, ana kashfa
ya kughushi umri wa kuzaliwa ili aendelee kubaki madarakani kwa muda
mrefu, akimtuhumu kuwa amediriki hata kunyofoa nyaraka muhimu Chuo Kikuu
cha Dar es Salaam alikosoma ili kuficha taarifa muhimu zinazomhusu,
“Tunamfahamu, hatuna shaka ya chanzo chetu…tunamtaka azirudishe,
vinginevyo tutamtaja hadharani. Na tukimtaja, hapatakalika,” alionya na
kudokeza kuwa ameghushi miaka mitano.
--
HabariLeo
No comments:
Post a Comment