Nukuu ya gazeti la NIPASHE
Waziri
wa Maliasili na Utalii, Balozi Khamis Kagasheki, amesema shehena na
makontena mawili ya meno ya tembo yaliyokamatwa Hong Kong, yatachunguzwa
kwa kutumia vinasaba (DNA) ili kubaini kama asili yake ni Tanzania.
Aidha,
amesema maofisa wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) wale waliokuwa zamu
siku shehena hiyo ikipitishwa bandarini Dar es Salaam kwenda Hong Kong,
wanachunguzwa ili kubaini ukweli.
Alisema
hayo wakati akifanya majumuisho ya hoja za wabunge waliokuwa wakijadili
maazimio mawili ya Bunge kuhusu marekebisho ya mpaka na upanuzi wa
Hifadhi ya Taifa ya Gombe na lile la kuanzisha Hifadhi ya Taifa ya
Kisiwa cha Saanane, “Hatuna uhakika bado kama meno yaliyokamatwa huko
Hong Kong yana asili ya Tanzania au yalikuwa yakipitishwa nchini
mwetu…tunafanya mazungumzo na balozi wetu kule China kuhusu suala hilo,”
alisema.
Alisema
taarifa ambazo zimekwishapatikana zinaonyesha kwamba kontena moja
linatokea Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) na kontena lingine bado
halijaeleweka wazi kwamba linatokea Tanzania au la, na ndio maana
uchunguzi utahusisha vipimo vya DNA ili kujua asili ya meno hayo.
Oktoba
16, mwaka huu, maofisa usalama wa Hong Kong waliyakamata makontena
mawili yaliyokuwa yamesheheni meno ya tembo yenye thamani ya dola za
Marekani milioni 3.4. Hata hivyo, kontena moja kati ya hayo lenye
thamani ya dola za Marekani milioni 1.7 linadaiwa kuwa linatokea
Tanzania. Kama hiyo haikutosha, shehena ya meno ya tembo ilikamatwa
bandarini Dar es Salaam Jumapili iliyopita na hali ambayo inaonyesha
kasi ya kuuwa kwa tembo ni kubwa.
Mapema
katika mchango wake binafsi, mbunge wa Iringa Mjini (CHADEMA),
Mchungaji Peter Msigwa, alisema kuongeza mipaka ya hifadhi ni suala zuri
lakini serikali inawajibu wa kulinda hifadhi hizo.
Alizungumzia
tukio la hivi karibuni la kukamatwa kwa meno ya tembo huko Hong Kong na
bandarini Dar es Salaam yanaashiria kwamba tembo waliopo kwenye hifadhi
wanauawa, “Hii inaonyesha jinsi gani tembo wetu wanavyoteketea,”
alisema na kuongeza, “sifurahishwi sana kuona tembo wetu wanakufa.”
No comments:
Post a Comment