Tuesday, December 25, 2012

CHEKA NA CHIMWEMWE NUSURA WAZICHAPE KAVUKAVU KATIKA HOTELI YA NAURA SPRINGS!!!

Mafahali mawili wanaotegemea kuzichapa tarehe 25, 2012 kugombea mkanda wa IBF katika bara la Afrika, Ghuba ya Uajemi na Mashariki ya Kati Mtanzania Francis Cheka na Mmalawi Chiotcha Chimwemwe nusura wazichape kavukavu wakati wa upimaji uzito na mkutano wa waandishi wa habari katika hoteli ya nyota 5 ya Naura Springs, jijini Arusha leo tarehe 25 Desemba 2012.
 Hii ni mara ya kwanza kwa ngumi za kulipwa kupewa hadhi kubwa kama hiyo ya kuwekwa kwenye hoteli ya nyota tano (5) hapa Tanzania.
 Wawili hao walikuwa katika hoteli hiyo ya kifahari ya Naura Springs inayomilikiwa na bwana Felix Mrema anayemiliki mahoteli lukuki katika jiji la Arusha na Moshi ambazo ni Naura Springs Hotel, Impala Hotel, Ngurudito Hotel, Impala Moshi na Livingstone Hotel za Moshi!
 Mpambano huo uliopewa jina la “Vurumaini chini ya Mlima Meru”umekuwa ni gumzo katika jiji la Arusha, Moshi, Tanga, Dodoma, Manyara pamoja na nchi jirani za Kenya, Uganda, Burundi na Rwanda na unaandaliwa na kampuni ya kizalendo ya Green Hills (T) Limited inayomilikiwa na bondia wa zamani wa taifa katika ngumi za ridhaa na kuloipwa George Andrew na familia yake.
 Aidha, watalii wengi walioko katika jiji la Arusha wakati huu wa sikukuu ya Xmas wameonyesha nia zao za kuliangalia pambano hili na wengine wameshakata tiketi tayari kuingia katika ujwanja wa Sheik Amri Abeid kuwashughudia mafahali hao wawili wakitoana jasho.
 Chiotcha mwana wa Chimwemwe mwanajeshi wa ngazi ya Luteini Usu katika jeshi la Malawi amepania kulibeba juu taifa lake lililoko pembezoni mwa ziwa Nyasa kwa kumwonyesha Francis Cheka kuwa ngumi zinaendana na ushupavu.
 Chimwemwe anadai kuwa hakuja Tanzania kutalii kama walivyo watalii wengine bali alikuja kuwakilisha nchi yake aipendayo ya Malawi na kurudi kwao na mshipi wa IBF katika bara la Afrika, Ghuba ya Uajemi na Mashariki ya Kati. Alisema kuwa kushinda kwake sio kitu cha kubahatisha ila ni uhakika.
 Naye Francis mwana wa Cheka, Mtanzania aliyeipeperusha vyama bendera ya taifa hili katika mapambano mengi bila kuzivunja nyoyo za mashabiki wa ngumi nchini alisema kuwa “Mwache Mmalawi huyo ajifurahishe tu kwani hajui kinachongojea ulingoni”

No comments:

Post a Comment