Tuesday, December 25, 2012

ASKOFU MALASUSA HAPENDEZWI NA MATUMIZI YA NGUVU YANAYOFANYWA NA JESHI LA POLISI

ASKOFU wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri (KKKT), Alex Malasusa amesema hapendezwi na matumizi ya nguvu yanayofanywa na Jeshi la Polisi hata kwenye migogoro ya wanafunzi wa shule za msingi.
 
Kauli hiyo iliitolewa jijini Dar es Salaam leo, Askofu huyo, wakati akitoa ujumbe wa amani wa Siku ya njema ya kuzaliwa Yesu (Christmas).
 
Malasusa alisema matumizi ya nguvu tena kwa kuwapiga mabomu watoto hao wa shule za msingi inamtia hofu kwa kuwa haelewi baada ya miaka kumi watoto hao watakuwa wamejifunza nini.
 
“Wakati nikiwa mtoto nilizoea kuwaona askari  wakitembea na fimbo lakini siku hizi matumizi ya silaha yamekuwa yakiongezeka sehemu mbalimbali”alisema.
 
Askofu Malasusa alisema utasikia baadhi ya watu wanasistiza kudumishwa kwa amani na utulivu lakini hao hao wanakuwa wakwanza kuharibu amani hiyo huku wakitegemea jeshi.
 
Aliwakumbusha viongozi kuwa ili amani indelee kudumu nchini ni lazima wajenge tabia ya kuvumiliana katika masuala mbalimbali, kwani amani hailindwi kwa silaha bali ni utashi wa watu.
 
Akifafanua zaidi katika ujumbe huo wa Christmas, alisema amani ni lazima iwe tabia ndani ya maisha ya kila mtu na inapokosekana watu wote wasiwe na furaha.
 
Alisema kuna familia nyingi ambazo amani kati ya mume na mke imetoweka kutokana na kushuka kwa maadili.
“Kuna ndoa nyingi zimekuwa za majuto kwa sababu watu wengi wameshindwa kutii amri ya mungu”alisema Malasusa.
 
Askofu Malasusa alisema wapo wengi wanaotaka kuwa juu kimaendeleo, hilo siyo baya bali kikubwa ni kumuweka Yesu moyoni.

No comments:

Post a Comment