Monday, December 31, 2012

KISANDU KAJIVUA UANACHAMA -CHADEMA

TAARIFA KWA UMMA WA WATANZANIA

KUACHIA NYADHIFA ZOTE ZA UONGOZI NDANI YA CHAMA NA KUJIVUA UANACHAMA WA CHADEMA

Ndugu wanahabari naomba mnifikishie taarifa hii kwa Watanzania wenzangu wenye uchungu na nchi hii;

1.0.UTANGULIZI

Kwa muda mrefu sasa kumekuwa na hisia hasi juu yangu na mkoa wa Tanga kwa ujumla juu ya ushiriki wangu kwenye shughuli za chama. Natambua kwamba wapo ambao tayari wameniona mnafiki, mamluki na msaliti kwasababu tu ya kutopenda kutambua ukweli juu ya mwenendo wa chama changu cha CHADEMA.

Nimeamua kuandika waraka huu nikitambua ya kwamba, kutambua ukweli ni njia ya kuibua fikra chanya, kuamini matendo chanya kuelekea kupata mafanikio zaidi. Ni heri kuzungumza ukweli ulio wazi kuliko kuwa kondoo na mnafiki ndani ya chama. Kupitia barua hii naomba nitoe dukuduku langu la moyoni kwa manufaa ya chama changu cha CHADEMA.


1.2.UCHAGUZI WA 2010.

Mwaka wa 2010 nilikuwa mwaka wa kwanza chuo kikuu cha Sebastian Kolowa (SEKUCo). Kwa ujasiri mkubwa niliamua kuchukua fomu na kugombea ubunge kupitia CHADEMA jimbo la Lushoto mkoani Tanga, japo kuwa sikuwa mzawa wala mkazi wa Lushoto.

Pamoja na kujenga mazingira mazuri kisiasa, nasikitika kusema kwamba viongozi wa chama changu ngazi ya Taifa wamekuwa wepesi sana kupuuza mkoa wa Tanga ikiwamo wilaya ya Lushoto katika ujenzi wa chama. Wamekuwa wepesi sana kulaumu viongozi wa chama kuliko kufika katika maeneo husika na kuona hali halisi. Kumbukeni kwamba tangu uchaguzi wa 2010 mkoa wa Tanga umesahaulika kabisa na kususia viongozi wa wilaya na majimbo. Vilevile ikumbukwe kwamba ujenzi wa chama ni kazi ya kujitolea, hivyo kazi hii haiwezi kufanikiwa bila mawasiliano mazuri na viongozi wa kitaifa.



1.3.CHAGUZI NDOGO ZA MADIWANI.

Uaminifu finyu kwa viongozi wa chini wa chama ni sababu ya kufanya vibaya. Kumekuwepo na mgawanyo mbovu wa madaraka ndani ya chama unaokiuka misingi ya katiba ya chama. Kumejengeka utamaduni wa viongozi wa juu wa chama kuhodhi madaraka ya viongozi wa chini wa chama na kuvuruga utendaji wa viongozi kwa kisingizio kwamba viongozi wa chini ni mamluki takribani nchi nzima. Hatuwezi kupata mafanikio makubwa ya kisiasa na kujenga mtandao imara wa chama kama tutaendelea na utamaduni huu wa kudharau viongozi wa chini wa chama.

1.4.ZIARA ZA M4C.

Ziara za M4C zimekuwa za kiupendeleo zaidi bila kuzingatia maeneo ambayo hayakufikiwa na kampeni za Urais mwaka 2010. Mkoa wa Tanga umekuwa ukitengwa sana na kutokuthaminiwa katika ujenzi wa chama. Pamoja na ukweli kwamba chama kimejengwa kwa misingi ya kujitolea, ubinafsi wa viongozi ni kikwazo kikubwa kwa CHADEMA. Ushindi wa CHADEMA hautatokana na baadhi ya mikoa ya Tanzania bali wastani mzuri wa kura kwa kila mkoa wa Tanzania.

Ninashindwa kuelewa vigezo vya M4C katika kuchagua viongozi wanaotakiwa kushiriki ziara za vuguvugu la mabadiliko(M4C). Inanishangaza kuona mwanachama aliyejiunga jana CHADEMA akitokea CCM leo anapewa kipaumbele kuliko viongozi waliojenga chama kwa muda mrefu kwa nguvu ya kujitolea hasa ma wilayani, majimboni na mikoa kwani viongozi hawa wa chini hawalipwi chochote zaidi ya nguvu zao na mwisho wa siku wanaitwa majina mengi mara mamluki, wasaliti, wametumwa na CCM. Kwa mwendo huu hatuwezi kufika wakati viongozi waliopo juu wanalipwa mishahara na wanaojenga chama huku chini wanaitwa majina ya kila aina.



1.5.UDHAIFU WA BARAZA LA VIJANA WA CHADEMA(BAVICHA).

Baraza hili limeshindwa kabisa kufanya kazi yake ya kuwa unganisha vijana bali limekuwa ndio chanzo cha migogoro. Migogoro yote inayoendelea CHADEMA hivi sasa inatoka na Baraza hili kutokuwa makini na utendaji kwani imekuwa kila mtu ni kibaraka, mamluki, kirusi, anatumiwa hata kama anaongea ukweli, je tukipewa nchi nani atasimamia rasilimali za nchi?

Unaweza sema baraza linafanya kazi kwa maana ya Mwenyekiti na Katibu wake. Tunaposema baraza tunamaanisha wajumbe wote wa majimbo, wilaya na mikoa wanashiriki vipi kujenga chama kupitia Baraza lao. Ukiangalia vikao vya Taifa vya BAVICHA tangu vianze vimekuwa vikishirikisha wenyeviti wa mikoa kinyume na katiba ya chama na mwongozo wa Mabaraza upande wa BAVICHA ibara ya 6.8.6 wajumbe wa kamati tendaji ambapo makatibu wa mikoa ni wajumbe lakini kinyume chake kikao kilichofanyika Morogoro mwaka huu walishiriki wenyeviti badala ya makatibu tena makatibu tumekuwa tukiletewa taarifa na wenyeviti. Lazima demokrasia ichukue mkondo ndani ya chama tusifanye mambo kwa kupeana fadhila za uchaguzi. Na hii ni ukritimba ndani ya chama na ulafi wa madaraka.


1.6.BUSARA IMEPOTEZA MWELEKEO CHAMANI.

Si kila mwenye kosa anastahili kuvuliwa uanachama, ukombozi wa watanzania unahitaji kulindana na kujengana kwani wapinzani bado tuko wachache sana, wengi ni mashabiki tu. Tunapofukuzana kwa makosa madogomadogo hatujengi chama bali tunaongeza chuki na kupoteza imani kwa wananchi. Mgogoro wa madiwani wa Arusha na Mwanza haikuwa njia nzuri ya kuwafukuza madiwani bali ilitakiwa kuwajenga na kuwa fanya wawe imara. Unajua hata mamluki kama wanavyo dai kwenye mitandao ya kijamii wanaweza kubadilika kwa busara nzuri.

Nakumbuka hata kule nyumbani kwetu wilaya ya kahama viongozi waliokuwa kamati tendaji ya jimbo la kahama pamoja na aliyekuwa mgombea wa ubunge walivuliwa uanachama na Mwenyekiti wa wilaya na viongozi wa Taifa wakabariki, nimesikia majuzi tu mwezi desemba 2012 kule Mbeya kuna viongozi wamevuliwa uanachama. Hizi ni sampo tu.


Style hii ya vuavua uanachama haitawezesha chadema kushika dola, kwani chama makini hakifukuzi bali humjenga mtu ili abadilike. Mimi binafsi na kerwa sana na hali hii ya fukuzafukuza kwa kutumia kigezo cha Katiba ya chama, watu wamekuwa wakikomoana kupitia katiba ya chama ili kuoneshana ubabe. Hii hata mikoani imetawala sana kutokana na hofu ya baadhi ya watu kutaka kuwa viongozi au baadhi ya viongozi kuonekana wanang’aa kisiasa au kukubalika kuliko wengine. Hii pia kisaikolojia inaweza kuwa ni hofu ya wabunge kuzidiwa kete na baaadhi ya vijana au viongozi majimboni na wilayani na kuogopa kukosa nafasi zao kipindi kijacho.


1.7.USHAURI WANGU.

Kama CHADEMA ina dhamira ya dhati ya kushika dola basi itambue mtu au kiongozi anapo dai haki msimwite mamluki au katumwa na CCM hii itasaidia kujenga chama, kwani viongozi wanajua fika mawazo yao katika vikao hayawezi kukubalika kutokana na imani na kuabudu watu badala ya kufata misingi ya chama.

1.8.URAIS 2015

Tangu nilipotangaza kugombea urais katika uchaguzi mkuu ujao wa mwaka 2015 viongozi wajuu wamekuwa wakijikanyagakanyaga na kuhoji nani kamtuma huyu kijana. Chadema hakuna demokrasia ya kweli ndani ya chama kwani watanzania mmeona wenyewe John Shibuda alipotangaza kuutaka urais akaitwa mamluki, msaliti. Na Zitto Kabwe alipotangaza kuutaka Urais anaitwa majina mengi mara msaliti, ooh anatumika na CCM. Sasa mimi nashindwa kuelewa nini maana ya demokrasia, au nani anafaa kusema anataka kuwa Rais ndani ya chama.

Nchii hii sasa ina siasa za kiliberali, tumeshatoka kwenye siasa za Chama Kimoja ambao ulikuwa ni mfumo wa Chama cha Mapinduzi. Sasa kama mambo yenyewe ndio hivi CCM itatuwia vigumu kuwapokonya utawala. Nilichojifunza ndani ya chama wanaogopa kasi ya vijana wenye uwezo walioko chini na kuanza kuhofu nafasi zao, ndio maana wengine wanasema BAVICHA wanatakiwa waheshimu wakubwa(ARFI awaonya bavicha-Mtanzania ya 29/12/2012). Hivi hawa wakubwa waheshimiwe hata kama wanatupeleka kusiko.


Urais ni uwezo wa mtu na karisma ya mtu, kama wewe huwezi muache mwenzako, wewe unapiga kelele eti Kisandu hawezi kuwa Rais, sawa mbona wewe hujatangaza nia ya kuwa Rais? Tuache ujinga wa kuendekeza kila kitu kinacho semwa na Fulani ndio sahihi. CHADEMA kuna wanachama wa aina tatu 1. walio anzisha chama 2. waliokipokea chama na 3. wanachama waliowapatikana kipindi cha uchaguzi mkuu 2010 amabapo na mimi nilikuwa mgombea wa ubunge jimbo la Lushoto na baada ya uchaguzi mkuu huo, hawa wanachama namba3 hawa kijui chama vizuri wao wanaenda na upepo tu, yaani kiongozi wa juu akisema kitu Fulani ni sahihi hata kama kakosea au anataka ushauri. Ona Chadema tuko mstari wa mbele kuipinga CCM na serikali yake kwa uongozi mbovu, sasa naomba vyama vyote vya siasa hasa viongozi wa juu hapa Tanzania acheni ubinafsi na ukritimba wapeni nafasi vijana msiwabanie.Jifunzeni kutoka Kenya jirani zetu muone walivyo pewa vijana nafasi za kutetea nchi yao. Mambo kama haya ndio yaliyo mfanya mwenyekiti wa vijana wa ANC Afrika kusini kuvuliwa uanachama. Hebu turuhusu demokrasia.


1.9.HITIMISHO.

Nachukua maamuzi magumu japo mtaona nimekurupuka au nimepoteza dira lakini ukweli utabaki kuwa ukweli. Naachia nyazifa zote za uongozi nilizo nazo ndani ya chama(Katibu wa BAvicha mkoa wa Tanga) na ninajivua uanachama wa Chadema na kubaki mwanachi huru.Fanyieni kazi niliyowaambia kuimarisha chama. Maamuzi ya kujiunga na chama kingine ni demokrasia. Msimamo wangu wa Urais uko palepale .


DEOGRATIUS KISANDU.


ALIYE KUWA KATIBU WA BARAZA LA VIJANA WA CHADEMA(BAVICHA)

MKOA WA TANGA.
.29/12/2012

No comments:

Post a Comment