Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete
ametoa shilingi milioni 30 kuchangia mradi endelevu wa kulea na
kuhifadhi mbwa mwitu waliokuwa wameanza kutoweka kabisa katika Hifadhi
ya Taifa ya Serengeti, mkoani Mara.
Mhe. Rais pia amezishukuru na
kuzipongeza taasisi za umma na binafsi zinazoshiriki katika kuufanikisha
mradi huo unaojulikana kama Vodacom Foundation Serengeti Wild Dogs
Conservation Project.
“Juhudi hizi za kurudisha tena
makundi ya mbwa mwitu kwenye mbuga hii inayojulikana kimataifa ni ya
kupongezwa kwani itahakikisha kwamba wanyama hawa wanaendelea kuwepo
Serengeti na pia itaongeza idadi ya vivutio vyetu vya utalii mbugani
humu”, alisema Mhe. Rais
Aliyasema hayo Jumapili Desemba
23, 2012 wakati wa sherehe za kuachiwa huru kundi la pili lenye mbwa
mwitu 15 waliokuwa wamehifadhiwa kwa miezi kadhaa kwenye boma maalumu la
mradi huo, lililojengwa katika eneo la Nyamuma, Magharibi mwa Hifadhi
ya Taifa ya Serengeti, mkoani Mara.
“Nashukuru taasisi zote zinazounga
mkono juhudi za serikali katika kuhakikisha kwamba mbwa mwitu
wanakuwepo kwa wingi mbugani Serengeti kama ilivyo katika mbuga
zingine”, aliongezea Mhe. Rais.
Katika taarifa yake wakati wa
sherehe hizo, Mkurugenzi Mkuu wa Tawiri, Dk. Simon Mduma, alimueleza
Rais Kikwete kuwa jumla ya Mbwa mwitu ishirini na sita (26),
wamerudishwa mbugani hadi sasa, kufuatia kundi la kwanza la wanyama
mwitu hao kumi na moja (11) kuachiwa siku ya Alhamisi Agosti 30, 2012.
Alitanabahisha kwamba mradi huo
unaohusisha mbwa mwitu walioondolewa katika msitu wa Samunge wilayani
Loliondo ni mojawapo ya juhudi za kurudisha tena makundi ya wanyama hao
katika mbuga hiyo maarufu duniani, na kwamba baada ya kuhifadhiwa na
hatimaye kuachiwa kwao huku wakiwa wamevishwa collar maalumu zenye
redio ili kufuatilia nyendo zao, ni muendelezo wa juhudi za kupata
makundi sita yenye mbwa mwitu takriban kumi (10) kila moja, ikiwa ni
hatua endelevu ya muda mrefu ya kuhakikisha uwepo wa wanyama hao
mbugani humo.
Dkt. Mduma alisema kundi la
kwanza la mbwa mwitu hao kumi na moja (11) wote wapo hai na wanaendelea
vizuri katika maisha yao mbugani humo, na kwamba pamoja na wanyama hao
kutembelea hadi maskani yao ya awali ya Loliondo, malalamiko ya kuwapo
kwa uharibifu wa mifugo sehemu hizo kama ilivyokuwa awali hayajaripotiwa
hadi sasa.
Mkurugenzi Mkuu huyo wa utafiti wa
wanyama pori alieleza kuwa mbwa mwitu wamekuwa wakitoweka kutokana na
kuuawa kwa sumu na wananchi baada ya kula mifugo yao, ama kwa kuugua
magonjwa mbalimbali kama vile kichaa cha mbwa.
“Hivi sasa kuna makundi 11
yanayofuatiliwa, manane yakiwa Loliondo na matatu katika Hifadhi ya
Ngorongoro, yakifanya idadi ya mbwa mwitu kuwa 200″, alisema Dkt Mduma.
Aliongezea kuwa awali, katika
Hifadhi ya Taifa ya Serengeti makundi ya mbwa mwitu yalikuwa yakionekana
kwa wingi, lakini yamekuwa yakitoweka kwa kasi sana kiasi hata mara ya
mwisho ni wanyama mwitu hao wawili tu walioonekana katika mbuga ya
Serengeti mnamo mwaka 1998.
Mbwa mwitu ni miongoni mwa wanyamapori ambao wapo hatarini kutoweka duniani.
Takwimu zinaonyesha kuwa katika
Bara la Afrika kuna mbwa mwitu takriban 8,000 na kwamba Tanzania pekee
inakadiriwa kuwa na wanyama hao 3,500 katika mbuga mbalimbali nchini,
isipokuwa katika Hifadhi h ya Taifa ya Serengeti ambako walianza
kutoweka kabisa kabla ya juhudi hizi za kuwarejesha kuanza.
Kampuni ya simu za mkononi ya
Vodacom imechangia dola za Marekani 450,000 kwa kipindi cha miaka
mitatu ili kufanikisha mradi huo, ambao ulizinduliwa rasmi mwezi Julai
mwaka 2011.
“Vodacom tunajisikia furaha sana
kuwa sehemu ya juhudi za serikali katika kuimarisha sekta ya utalii
ambayo kwa sasa mchango wake ni mkubwa sana kwa taifa”, alisema Bw.
Salum Mwalimu, Meneja Uhusiano wa Nje wa Vodacom wakati wa sherehe za
kuwarudisha mbugani mbwa mwitu hao 15.
Bw. Mwalimu alisema kampuni yake
siku zote inalenga kubadili maisha ya watu na kwamba ni wazi kuimarika
kwa Hifadhi ya Taifa ya Serengeti inayochangia kwa kiasi kikubwa sekta
ya utalii nchini na ambayo inategemewa kwenye kuongeza pato la Taifa na
ustawi wa watu ni jambo muhimu sana.
Taasisi zingine zinazoshiriki
katika zoezi hilo ni Idara ya Utafiti wa Wanyamapori (TAWIRI), Mamlaka
ya Hifadhi za Taifa (TANAPA), Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCCA),
Frankfurt Zoological Society (FZS) , Grumeti Fund (GF) na Halmashauri
ya Wilaya ya Ngorongoro.
Mwisho.
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu.
Dar es Salaam.
24 Desemba, 2012
No comments:
Post a Comment