Rais
Jakaya Kikwete akiwa katika picha yapamoja na wasanii mbalimbali
walioenda kumpongeza jana Ikulu kwa mchango wake wa kusaidia wasanii na
kutambua mchango wa wanamuziki wakongwe kwa kuwapa Nishani.
……………………………………………..
Serikali imeanza kutoa Nishani kwa wasanii kwa vile inatambua umuhimu wao katika jamii.
Rais Jakaya Mrisho Kikwete
amewaeleza wawakilishi wa sanaa mbalimbali nchini waliofika Ikulu leo
asubuhi kutoa shukrani kwa Mheshimiwa Rais kwa kuwatambua na kuwapa
heshima kubwa ya Tuzo na Nishani wasanii katika siku ya sherehe za Uhuru za tarehe 9 Disemba, Ikulu, Dar-Es-Salaam.
“Tumetoa Nishani kwa vile
wasanii wanatoa mchango mkubwa, tumeanza kutoa nishani mwaka huu na
tutaendelea kutoa miaka ijayo kwani kwa kuitambua sanaa, mnawapa moyo
wasanii kuendelea kujituma na kuwa wabunifu zaidi” Rais amesema na kuongeza, “Tumeingiza
Nishani ya Wasanii na Watafiti maana nao wanafanya kazi kubwa sana ya
kutafiti mazao na mbegu mbalimbali ambazo zinaongeza tija katika kilimo
nchini”.
Katika kumbukumbu ya kusherehekea
miaka 51 ya Uhuru wa Tanzania bara mwaka huu, Rais Kikwete alitunuku
nishani kwa makundi mbalimbali ya watu waliotoa mchango mkubwa katika
jamii na waliotumikia taifa kwa uadilifu.
Rais alitoa Nishani ya Sanaa na
Michezo kwa mara ya kwanza kwa wasanii nchini ambapo Bi. Fatma Baraka
Khamis (Bi Kidude) kupitia Baraza la Sanaa Zanzibar, Kiongozi wa Muziki
wa Dansi ya Msondo Ngoma Muhidin Maalim Gurumo, Kiongozi wa Zamani wa
Bendi ya Dar Intrenational Marehemu Marijan Rajab walipata tuzo hiyo.
Wengine ni Msanii wa maigizo na filamu nchini Marehemu Fundi Said (Mzee Kipara) na Mwanariadha mkongwe John Steven Akwari.
Rais amewataka wasanii
kushirikiana na serikali lakini pia wawe mstari wa mbele katika
kupigania haki zao na sio kusubiri serikali tu iwafanyie hivyo.
Wasanii hao wamefika Ikulu wakiongozwa na Bw. Ruge Mutahaba wa Clouds Media Group.
Wengine ni Addo Mwasongwe, Rais wa
Shirikisho la Muziki na Mwenyekiti wa Chama cha Muziki wa Injili, Bw.
Juma Ubao Mwenyekiti wa Chama cha Muziki Tanzania (CHAMUDATA),
aliyewakilishwa na Hamza Kalala.
Bibi Shakila Said, Mkongwe wa
Muziki wa Taarab Nchini, Bi Carola Kinasha Msanii wa Muziki , Mzee King
Kiki msanii wa Muziki wa Dansi Mwana FA, msanii wa Kizazi Kipya na Bw.
Waziri Ally , msanii wa Muziki.
Wawakilishi hao pia wamemshukuru
Rais kwa msaada wa hali na mali anaotoa kwa wasanii mbalimbali
wanapopata matatizo ambao hivi sasa wapo katika hatua mbalimbali za
matibabu ya afya zao hapa nchini na nchi za Nje.
“Haya mengine ninayafanya
tukama wajibu wa kibinadamu kwa vile nina nafasi ya kufanya hivyo na
pale tunapokua na uwezo tunasaidia kama binadamu wenzetu” Rais Amesema.
Imetolewa na Premi Kibanga,
Mwandishi Habari wa Rais, Msaidizi,
Ikulu – DSM
21 Desemba, 2012
No comments:
Post a Comment