Waziri
wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Dkt. Fenella Mukangara (wa
pili kushoto) akimsikiliza Mkurugenzi Msaidizi Mkaazi wa Shirika la Kazi
Duniani, Bibi Hopran Fololo wakati akimwelezea kuhusu utekelezaji wa
mpango wa Ujasiriamali kwa Vijana unaoendeshwa na Shirika hilo hivi
karibuni Jijini Dar es Salaam. Wa kwanza kushoto ni Mkurugenzi wa
Maendeleo ya Vijana, Dkt. Elisante Ole Gabrieln na wengine ni wajumbe
kutoka ILO.
(Picha na Concilia Niyibitanga, WHVUM)
,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,
Na Concilia Niyibitanga
WHVUM
Serikali kupitia Wizara ya Habari,
Vijana, Utamaduni na Michezo imelitaka Shirika la Kazi Duniani (ILO)
kutunisha Mfuko wa Maendeleo ya Vijana ili vijana wengi waweze kukopa na
kuanzisha miradi ya ujasiriamali.
Hayo yamesemwa hivi karibuni naWaziri
wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Dkt. Fenella Mukangara wakati
akiongea na ujumbe kutoka Shirika hilo uliokuja ofisini kwake kwa ajili
ya kuzungumzia Mradi wa Ujasiriamali kwa vijana unaoendeshwa na Shirika
hilo.
Dkt. Mukangara pia amelitaka ILO
kupitia mradi huo kutoa mafunzo husika katika vituo vya Vijana vya
Sasanda, Marangu na Ilonga kwa kuzingatia malengo ya uanzishwaji wa
vituo hivyo.
Akielezea mpango huo, Mkurugenzi
Msaidizi Mkaazi wa Shirika hilo, Bibi Hopran Fololo amesema kuwa
wataanza kutoa mafunzo ya ujasiriamali kwa vijana 225 waliomaliza Vyuo
Vikuu katika fani mbalimbali na baadae vijana hao watatakiwa kwenda
vijijini kuhamasisha vijana wenzao kuhusu elimu ya ujasiriamali na
umuhimu wake.
Bibi Fololo amesema kuwa Shirika
kwa kushirikiana na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi wanatarajia
kuingiza elimu ya Ujasiriamali katika mitaala ya elimu ya Sekondari na
Vyuo vya Ualimu kwa lengo la kuwawezesha vijana kuhitimu wakiwa na elimu
hiyo jambo amabalo litawasaidia kujiajiri wenyewe.
Katika mradi huo wenye lengo la
kuibua fursa za ajira kwa vijana kupitia ujasiriamali shirika litatoa
mafunzo kwa Maafisa Vijana wa Wilaya nchi nzima ili waweze kuwaongoza
vijana ipasavyo katika sekta ya ujasiriamali. Ameongeza Bibi Fololo.
Aidha, Fololo amesema kuwa Shirika
litatoa ruzuku kwa baadhi ya miradi itakayobuniwa na vikundi vya vijana
ambapo vikundi vitashindanishwa na washindi kupatiwa ruzuku ya kuanzia
Dola 15,000 hadi Dola 20,000 kwa ajili ya kuendesha miradi yao.
Ameendelea kueleza kuwa pamoja na
kutoa ruzuku kwa vikundi vya vijana, watazisaidia pia taasisi za fedha
zinazokopesha vijana kwa kuzitunishia mifuko ili ziwe na uwezo wa
kukopesha vijana wengi zaidi.
Mradi huu unalenga kuhamasisha vijana wapatao milioni moja na nusu katika maswala ya ujasiriamali ili waweze kujiajiri wenyewe.
No comments:
Post a Comment