Baadhi ya wasanii wakiwa katika mazishi ya msanii wa filamu marehemu Sajuki. (Picha zote na habari Mseto Blog)
Rais Jakaya kikwete akizungumza na Meya wa Ilala Jerry Silaa (kulia) na Rais wa Shirikisho la Filamu, Mwakifyamba
Mbunge wa Kigoma Kaskazio, Zitto Kabwe akizungumza na waandiushi wa habari jinsi alivyoguswa na msiba wa Sajuki
Mamia ya wakazi wa jijini wakiwa katika mazishi ya Sajuki.
Nahodha wa timu ya taifa ya Tanzania 'Taifa Stars' Juma Kaseja
(katikati) akiwasili katika makaburi ya Kisutu Dar es Salaam leo.
Mmiliki wa mtandao wa kijamii wa Blog ya Nkoromo Daily, Bashiri Nkoromo
(kulia) akiwa na Msanii wa filamu, Hamis Magari wakati wa mazishi ya
Sajuki yaliyofanyika katika makaburi ya Kisutu jijini Dar es Salaam leo.
Baadhi ya wasanii wa filamu nchini, kutoka kushoto,
Hamis Mwinjuma Mwana FA’, Issa Mussa ‘Cloud’, Hisson Muya ‘Tino’, na Singo
Mtambalike ‘Richie Richie’, wakishiriki kubeba jeneza lenye mwili wa marehemu
Juma Kilowoko ‘Sajuki’, wakati wa mazishi yake yaliyofanyika leo kwenye makaburi ya
Kisutu jijini Dar es Salaam.
Rais
Jakaya Mrisho Kikwete akiwa na baba mzazi wa marehemu Sajuki wakati wa
mazishi ya msanii huyo leo katika makaburi ya Kisutu jijini Dar es
salaam
Rais
Jakaya Mrisho Kikwete akiweka udongo kaburini wakati wa mazishi ya
msanii Sajuki leo katika makaburi ya Kisutu jijini Dar es salaam
DAR ES SALAAM, Tanzania
RAIS
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Kikwete, jana aliongoza mamia ya
waombolezaji, wakiwamo wabunge na viongozi wa vyama vya siasa katika mazishi ya
aliyekuwa mtayarishaji na msanii wa filamu nchini, Juma Kilowoko ‘Sajuki’
aliyefariki dunia Januari 2 mwaka huu baada ya kusumbuliwa na maradhi ya kansa
ya damu.
Rais
Kikwete aliwasili katika Makaburi ya Kisutu yalikofanyika mazishi hayo saa 7:30,
dakika tano kabla ya mwili wa Sajuki kuwasili hapo ukitokea kusaliwa msikitini
Kariakoo, tayari kwa mazishi hayo yaliyoteka hisia za wengi na kukusanya kundi
kubwa la wasanii na wadau wengine wa sanaa.
Mbali
ya wasanii, vijana wa rika mbalimbali walijitokeza nyumbani kwa marehemu Tabata
Bima na kuupokea mwili, wakiongozwa na Mbunge wa Kigoma Kaskazini na Naibu
Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo, (Chadema), Kabwe Zitto, Naibu
Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Bara, Mtatiro Julius, Mbunge wa Iramba
Magharibi na Naibu Katibu Mkuu Chama Cha Mapinduzi (CCM), Mwigulu Nchemba.
Mwili
wa marehemu uliwasili nyumbani kwake Tabata Bima majira ya saa 3 asubuhi na
baada ya kusomewa dua, uliondolewa na kwenda kuswaliwa katika msikiti wa
Kariakoo kisha kwenda kuzikwa makaburi ya Kisutu, ambako Rais Kikwete aliungana
na waombolezaji wengine kumzika Sajuki.
Kikwete
alivyowasili makaburini
Rais
Jakaya Kikwete aliwasili makaburi ya Kisutu saa 7:30 akiingia kupitia geti
namba mbili, huku akiwaacha ‘solemba’ wapiga picha wa magazeti na televisheni
waliokuwa wamejipanga katika geti kuu la makaburi hayo.
Ujio
wake ulisababisha kukimbizana kwa wapiga picha hao kutoka geti kuu kuja geti
dogo lililokuwa karibu kabisa na lilipochimbwa kaburi la Sajuki, ambapo dakika
chache baadaye mwili wa marehemu uliingia makaburini hapo.
Mvutano
mkubwa wa kuwania upigaji wa picha za rais pamoja na jeneza la mwili wa
marehemu zilishika hatamu na kusababisha usumbufu kwa walinzi wa Rais,
waliokuwa wakijaribu kuwatenganisha wahudhuriaji na njia za kupitisha jeneza
kuelekea kaburini.
Baada
ya kusimama kwa dakika zipatazo 10 hadi mwili wa marehemu kufika na kuingizwa
kaburini, Rais Kikwete alitakiwa kuchota mchanaga na kutia kaburini kama ishara
ya kumzika Sajuki na kisha watu wengine wa familia nao kuendelea na zoezi hilo.
Rais
Kikwete akaruhusiwa kutoka pembeni ya kaburi, ambako alitengewa viti maalumu
alikokaa na walinzi wake, huku akisubiri kumalizika kwa mazishi hayo, ili
aondoke makaburini hapo.
Sita
waliomzika Sajuki watajwa
Wakati
hali ikiwa ya vurugu ikiwamo baadhi ya wanahabari na waombolezaji wengine
kupanda juu ya miti kuweza kushuhudia kinachojiri na kisha kushushwa na walinzi
wa Rais, watu sita waliopata bahati kuingia kaburini kumzika Sajuki
walitangazwa.
Katika
matangazo hayo ambayo pia yalielekeza namna sahihi ya kusimama kushuhudia tukio
hilo, Baba mzazi wa Sajuki, Saidi Kilowoko alitajwa kuongoza wazikaji hao,
akifuatiwa na baba mkubwa, Idd Issa Kilowoko.
Wengine
waliopata nafasi hiyo walikuwa ni kaka wa marehemu Issa Kilowoko, shemeji wa
marehemu Issa Juma, mwakilishi wa wasanii Issa Mussa ‘Claudi’ na mtu mmoja
aliyetajwa kwa jina la Salum Ahmed.
Ving’amuzi
vya Startimes gumzo mazishini
Katika
hali isiyokuwa ya kawaida, teknolojia mpya ya dijitali iliyoanza kutumiwa
kurusha matangazo ya televisheni usiku wa Januari 1, 2013 yalishika hatamu
katika mazishi hayo, ambapo waombolezaji walionekana kulalamikia huduma hafifu
za ving’amuzi vya kampuni ya Startimes.
Waombolezaji
hao walikiri kupata wakati mgumu kutumia huduma hiyo, huku baadhi ya wasanii
wakionekana kufurahia kwa madai kuwa ndio wasaa halisi utakaowawezesha
Watanzania kuangalia kwa mapana kazi zao za sanaa na kuchangia pato lao.
Mmoja
wa wasanii hao ambaye hakutaka kutaja jina gazetini, alikiri kuumia moyoni
kutokana na vilio vya Watanzania kutomudu gharama za ving’amuzi na kutofanya
kazi kwa baadhi ya walio na uwezo wa kuvinunua, lakini akakiri sanaa zao sasa
zitatazamwa.
“Nawahurumia
Watanzania wanaoshindwa kununua, lakini pia walionunua na kutopata
walichotegemea. Lakini naamini huu sasa ni wakati wa wasanii kuonekana sana kwa
kazi zao, kwani mitaani DVD ndio zinauza zaidi kwani TV hazina ving’amuzi,”
alisema.
Kauli
hiyo iliungwa mkono na baadhi ya wasanii waandamizi, wakiwamo wanachama wa
Shirikisho la Filamu Tanzania (Taff), ingawa pia hawakusita kuiomba Serikali
kuvipatia ufumbuzi vilio hivyo vya wananchi ambao ni wadau wao wakubwa.
Familia,
Taff kuamua juu ya 40 ya Sajuki
Wakati
baba wa marehemu Sajuki akitakiwa kuungana na Rais Kikwete kwa mazungumzo
mafupi na kisha kuondoka makaburini hapo, MC wa shughuli hiyo alifikisha kwa
wazikaji taarifa muhimu kuhusu shughuli ya 40 ya msiba huo.
“Familia
ya Sajuki na wasanii nchini, wanapenda kuwashukuru wote kwa kufanikisha mazishi
haya. Haina cha kuwalipa, ila Mungu atawalipa. Familia itakaa na Taff, kisha
itawatangazia tarehe maalum ya sahughuli ya 40 ya Sajuki, ila kwa sasa
hakutakuwa na matanga,” alisisitiza MC.
Idd
Azzan, Zito Kabwe wanena mazishini
Kwa
nyakati tofauti wakati wa mazishi hayo, wabunge na wanasiasa waliofika makaburini
hapo walitumia fursa zao kumuelezea Sajuki, masikitiko waliyonayo kwa kifo
chake na saana kwa ujumla.
Wabunge
hao ambao walikuwa sambamba na Meya wa Ilala, Jerry Silaa, ni pamoja na mbunge
wa jimbo la Kinondoni, Idd Azzan, mbunge wa Kigoma Kaskazini Zito Kabwe na yule
wa Mchinga, Said Mtanda.
Azzan
alisema kwa kifo cha Sajuki ni pigo katika tasnia ya sanaa na soko la filamu
nchini, ambapo aliwataka wasanii kuunganisha nguvu katika shirikisho lao, ili
kusukuma mbele harakati za kuleta maendeleo yao na tasnia kwa ujumla.
Azzan,
pia alitoa pole kwa ndugu na jamaa, akiwamo mke wa marehemu aliyemtaja kama
mwanamke shujaa aliyekabiliana bila kuchoka katika harakati za kuokoa maisha ya
mumewe, hadi Mungu alipomtwaa.
“Wasanii
kwa sasa waendeleze umoja wao ikiwamo kujiunga na Shirikisho lao (Taff), ili
kuiwezesha Serikali na mashirika mengine kumudu kuwasaidia kwa pamoja, tofauti
na hali ya sasa,” alisema Azzan.
Pia
Azzan alisema kuwa, atakutana na wabunge wa majimbo ya Dar es Salaam na kuona
namna ya kuja kuwasaidia wasanii kwa namna moja ama nyingine, ili waweze kujitambua na kutambua haki na
hadhi zao sambamba na kuwashauri kuanzisha mfuko maalum wa kuwainua.
Kwa
upande wake, Mbunge wa Mchinga (CCM) Said Mtanda, alisema kifo cha Sajuki ni
pigo kwa wanaharakati waliojitoa kupigania haki za wasanii hapa nchini kupitia
kazi zao hasa juu ya kudhulumiwa haki zao kwa kurudufisha.
“Mimi
nilikutana na Sajuki siku chache kabla ya kifo chake pale Muhimbili, na
niliongea naye machache na kubwa alikuwa akilalamikia wizi wa kazi zao unaofanya
na wasambazaji wao wa ‘Kidosi’’ alisema Mtanda.
Mtanda
ambaye pia yupo kwenye Kamati ya
Maendeleo ya Jamii, alisema wabunge wamekuwa wakipigania haki za wasanii
ikiwemo suala la stika maalum ambazo zitawasaidia kukuza pato lao endapo wataujua
vizuri mpango huo kwa kushirikiana na mamlaka husika ikiwamo TRA na Chama cha
Haki Miliki (COSOTA).
Mbunge
wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe, alisema pengo lililoachwa na Sajuki katika
utayarishaji na uigizaji wa filamu Tanzania, halitazibika kwa sasa kutokana na
mchango wake aliokuwa akiutoa enzi za uhai wake na kuwataka wasaniii kuwa kitu
kimoja katika kipindi hiki kigumu.
Aidha,
wananchi waliojitokeza katika mazishi hayo kwenye makaburi ya Kisutu, waliungana
na kauli za wabunge hao na kuwataka wasanii kuendeleza umoja wao na kujipanga
katika kipindi hiki kigumu.
Kuugua
kwa Sajuki na alikotokea kisanii
Marehemu
Sajuki alianza kuugua mwaka 2010 na kupatiwa matibabu nchini India katika
kipindi hicho na kwa mara ya pili, alikwenda India mwaka 2011 kwa fedha ambazo
zilitokana na michango ya wasamaria.
Sajuki
alifikwa na umauti akiwa kwenye harakati za kupelekwa kwa mara nyingine nchini
India kwa matibabu zaidi, lakini mapenzi ya Mungu yakatimia.
Marehemu
Sajuki alianza kujishughulisha na kazi za sanaa akiwa kati ya wasanii waliokuwa
wakiunda kundi la sanaa la Kaole, kabla ya kulipa kisogo.
Baada
ya hapo akawa anafanya kazi za kujitegemea kama mtayarishaji, muigizaji na
mzalishaji wa filamu ambako ndiko alikoanza kupata mafanikio makubwa.
Sajuki
aliyezaliwa mwaka 1986 mkoani Ruvuma, ameacha mjane na mtoto mmoja wa miezi 10.
Mashabiki
wake watamkumbuka kwa kupitia filamu zake zilizompa umaarufu kwa kuzicheza kwa
umahiri sambamba na mke wake Wastara, kupitia Kampuni yao ya Wajey Production
ambazo ni ‘Mboni Yangu’, ‘Round’, ‘Shetani wa Pesa’, ‘Hero of the Church,’ ‘Vita’,
‘Briefcase’, ‘Revenge’, ‘Dhambi’,
‘Two Brothers’ na ‘Behind The
Scene’
No comments:
Post a Comment