Dar es Salaam. Wamiliki wa vituo vya utangazaji vya televisheni nchini, wamesema watasitisha kurusha ma tangazo ndani ya mwezi mmoja kuanzia sasa kutokana na kushindwa kumudu gharama za uendeshaji.
Hatua hiyo inatokana na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kuzima mitambo ya analojia na kuhamia dijitali Desemba 31, mwaka jana kitendo walichodai kimepunguza mapato yanayotokana na matangazo.
Mwenyekiti wa Chama cha Wamiliki wa Vyombo vya Habari Tanzania (Moat), Reginald Mengi alisema hakuna haja ya kurusha matangazo kwa hasara.
Mengi alisema kutokana na kuanza kwa mfumo wa dijitali, watangazaji wamesitisha kutoa matangazo kwa sababu wananchi wengi hawana ving’amuzi.
Mengi ambaye pia ni mmiliki wa vituo vya televisheni vya ITV, EATV na Capital TV, alisema licha ya nchi za Afrika, Tanzania imekuwa ya kwanza kuzima mitambo ilhali wananchi hawakuwezeshwa kumudu gharama za ving’amuzi.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa Sahara Media Group na mmiliki wa Kituo cha Star Tv, Samwel Nyalla alisema hivi sasa wanaendesha biashara hiyo kwa hasara.
No comments:
Post a Comment