WAKILI wa upande wa utetezi katika kesi ya wafuasi 54 wa Katibu wa
Jumuiya na Taasisi za Kiislam, Sheikh Issa Ponda, Hamidu Ubaidi
ametangaza kujitoa kuendelea kuwatetea washitakiwa hao kwa kile
alichodai kuwa kesi hiyo imekuwa ikiendeshwa haraka na mfululizo na
mahakama.
Kesi hiyo ambayo ilikuja kwa ajili ya kusikilizwa,
wakati mshitakiwa wa 24 anatoa utetezi wake, wakili Ubaidi mbele ya
hakimu Sundi Fimbo aliomba kesi hiyo isiendelee kusikilizwa kwa sababu
yeye anawasilisha ombi rasmi la kujitoa.
“Naona sitawatendea haki
washitakiwa ambao ni wateja wangu kulingana na kesi hiyo ya maandamano
haramu ya kutaka kwenda ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP), Dk
Eliezer Feleshi ili wamshinikize aondoe hati yake ya kumfungia dhamana
Ponda, kwa sababu kesi hii inavyokwenda haraka na mfululizo sipati muda
wa kuzungumza na kuwaandaa washitakiwa,” alidai wakili Ubaidi.
Hata
hivyo ombi hilo lililamikiwa na mawakili waandamizi wa Serikali Benard
Kongora, Joseph Mahugo kwa madai hiyo ni mbinu ya kuichelewesha kesi
hiyo:
“Mhesimiwa hakimu ni huyu huyu wakili Ubaidi, Jumatatu na
Jumatano aliomba kesi hii tuairishe mara kwa lisaa limoja lakini
hakutokea …leo hii anakuja kuieleza mahakama kuwa eti anajitoa kuwatetea
washitakiwa kwasababu kesi hii inaendeshwa mfululizo na hapati muda wa
kuwaandaa washitakiwa wake…. sisi upande wa Jamhuri tunasema hii ni
mbinu ya kutaka kuchelewesha kesi hii isimalizike mapema. Ni uongozi wa
mahakama ndiyo uliotoa fursa ya kesi hii kuendeshwa mfululizo hivyo sisi
tunaona tutumie fursa hiyo kuendesha kesi hii,” alidai wakili Kongora.
Kwa
upande wake hakimu Sundi Fimbo aliarisha kesi hiyo hadi Machi 11 mwaka
huu, itakapokuja kwa ajili ya washitakiwa kuendelea kujitetea.
Wakati huo huo; Jumla
ya washitakiwa tisa wa kesi ya uchochezi na wizi wa malighafi zenye
thamani ya Sh. Milioni 59 inayomkabili Ponda na wenzake 49, wamedai
hawamfahamu Shekhe Mkuu wa Tanzania, Mufti Issa bin Shaban Simba wala
Baraza la Waislamu Tanzania (BAKWATA).
Pia waliyakana maelezo
waliyoyatoa wakati wakihojiwa na Jeshi la Polisi ambapo walikuwa
wamekiri kuwa walikamatwa katika eneo la kiwanja cha Markas Chang’ombe
kinachomilikiwa na kampuni ya Agritanza Ltd., lakini leo wakati wakitoa
utetetezi wao walikanusha kukamatwa eneo hilo na kwamba wao walikamatwa
na polisi Oktoba 16 mwaka jana, wakiwa ndani ya Msikiti wa shule ya
Markas Chang’ombe wakisali sala ya Itikaf.
Washitakiwa hao ambao walikuwa wakiongozwa na wakili wao Nassor Juma, ni mshitakiwa 10,11,12,13,14,15,16 na 17.
Wakihojiwa
na wakili Mwandamizi wa serikali Tumaini Kweka ni kwa nini walipopanda
kizimbani wametoa maelezo mapya wakati walipohojiwa na polisi walitoa
maelezo ya kikiri kukamatwa ndani ya kiwanja hicho ambacho kiliuzwa na
BAKWATA kwa kampuni ya Agritanza Ltd., washitakiwa hao wakijibu swali
hilo wengine walidai hawajui kusoma na kuandika na wengine wakadai kuwa
hayo maelezo ni yao na saini ni zao ila hizo saini waliziweka kwenye
hayo maelezo baada ya kulazimishwa na askari polisi. Wengine walidai
kuwa hawakufahamu ni kitu gani kilikuwa kikiandikwa na polisi waliokuwa
wakiwahoji kwa sababu polisi hawakuwasomea maelezo hayo. Mshitakiwa
mwingine alidai maelezo aliyochukuliwa na askari yaliandikwa na wino wa
blue na siyo mweusi kama alivyoonyeshwa leo nakala ya maelezo yake
ambayo yapo mahakamani kama kielelezo na wakili Kweka.
Aidha, kwa
ujumla wao washitakiwa hao walidai kuwa polisi waliwafanyia unyama,
waliwapora simu zao za mikononi, waliwatukana matusi ya nguoni na
waliwapiga virungu. Wkasema baadhi ya Askari Polisi waliokuwa wamekuja
kuwakamata ndani ya Msikiti walikuwa wananuka pombe na hawakuvua viatu
wakati wanaingia ndani ya msikiti.
Viongozi wa Jumuiya hiyo,
Sheikh Ponda ambaye ni mshitakiwa wa kwanza na Swalehe Mukadam,
walikwepa kuanza kutoa utetezi wao, baada ya Wakili Juma Nassoro, kudai
kuwa wataanza na washitakiwa wengine.
No comments:
Post a Comment