Wednesday, March 20, 2013

WATOTO WALEMAVU WA NGOZI (ALBINO) WAPATA TABU MBARALI MBEYA HUKU TAASISI NA MASHIRIKA BINAFSI YANAYOJIHUSISHA NA KUWALEA YAKIWA YAMEJIKITA MJINI

Watoto hao  wenye ulemavu wa ngozi(Albino) wanaosoma katika shule ya Msingi Motomoto iliyoko katika Kata ya Ruiwa Wilaya ya Mbarali Mkoani hapa wamesahaulika katika kupatiwa misaada ambapo wanaofaidi wako mijini tu.
  










WAKATI baadhi ya Taasisi na mashirika binafsi yanayojihusisha na kulea na kuhudumia watoto wenye ulemavu na kujikita zaidi mijini na kusahau vijijini wamepewa wito wa kutembelea maeneo yote.

Mashirika hayo ambayo yamewasahau watoto walioko vijijini wametakiwa kuwatembelea walemavu hao ambao hawajui sehemu ambayo wanaweza kupata misaada ikiwemo mafuta ya kupaka kwa ajili ya kutunza ngozi zao pamoja na miwani na kofia.
  
Mwito huo umetolewa baada ya kukutwa kwa watoto wenye ulemavu wa ngozi ambao wanasoma katika shule za msingi huku wakiwa wamechanganywa na watoto wengine ambao hawana matatizo.
  
Watoto hao  wenye ulemavu wa ngozi(Albino) wanaosoma katika shule ya Msingi Motomoto iliyoko katika Kata ya Ruiwa Wilaya ya Mbarali Mkoani hapa walisema wamesahaulika katika kupatiwa misaada ambapo wanaofaidi wako mijini tu.
  
Watoto hao waliokutwa nawaandishi wa habari shuleni hapo huku wakiwa wamechanganywa na wanafunzi wengine katika darasa moja huku wakiwa hawawezi kuendana na wenzao ambapo wamebainika kushindwa kusoma wala kuandika kutokana nakukosa vifaa.
  
Aidha watoto hao walisema wanaiomba Serikali na mamlaka inayohusika kuwahamisha na kuwatenganisha na wanafunzi wengine ili iwe rahisi kwa wao kupewa misaada ikiwa ni pamoja na vifaa vya kujifunzia na mafuta ya kupaka.
  
Walisema wamesahaulika kwa kiasi kikubwa kutokana na kuchanganywa katika darasa moja ambapo inakuwa si rahisi kwa mwalimu kuwaangalia kwa ukaribu na kujua kama kuna mahitaji mengine tofauti na watu wengine ambao hawana uhitaji wa dawa na vifaa.
  
Baadhi ya watoto hao ambao wako darasa la kwanza na darasa la tatu walikutwa wakitumia daftari za kawaida ili hali wanamatatizo ya kuona mbali bila kuwa na vifaa kama miwani na kofia za kusaidia kuzuia na kupunguza mwanga.
  
Mmoja wa walimu katika shule hiyo ambaye hakutaka jina lake liandikwe kwa sababu ya kutokuwa msemaji wa  tukio hilo alisema tangu watoto hao waanze shule hiyo hawajawahi kupatiwa msaada wa aina yoyote.
  
Alisema hata namna ya ufundishaji wa watoto hao unakuwa mgumu kutokana na kuchanganywa na watoto wengine katika darasa moja ambapo Mwalimu inambidi kufundisha kwa ujumla bila kujali mahitaji ya mtu mmoja mmoja.
  
Aidha aliwashukuru wazazi na walezi ambao wamekuwa wakijitolea kuwahudumia watoto hao kwa kuwapeleka na kuwarudisha shuleni ambapo pia aliwaomba wasamaria wema kujitolea kuwahamisha watoto hao ili wakasome kwenye shule maalumu kutokana na hali mbaya ya hewa Wilayani Mbarali.
  
Alisema hali ya hewa ya Mbarali ni joto ambalo linawaathiri watoto hao hivyo amewaomba wasamaria wema kujitolea kwa kuwahamisha na kuwatafutia shule maalumu ambazo zinamahitaji yote yanayotakiwa kwa ajili ya walemavu wa ngozi ambao asilimia kubwa pia wanasumbuliwa na macho.

Picha na kamanga

No comments:

Post a Comment