Saturday, March 9, 2013

YANGA KATILI, YAUA TOTO LAKE, AZAM YAKWAMA CHAMAZI

Nizar akishangilia baada ya kufunga bao pekee la ushindi leo. Kwa hisani ya Bin Zubeiry Blog

Na Mahmoud Zubeiry
BAO pekee la kiungo Nizar Khalfan leo, limezidi kuipaisha Yanga SC kileleni mwa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, kufuatia ushindi wa 1-0 dhidi ya Toto Africans Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Kwa ushindi huo, Yanga imefikisha pointi 45 baada ya kucheza mechi 20 hivyo kuzidi kujitanua kileleni mwa Ligi Kuu kwa pointi nane zaidi, dhidi ya Azam FC wanaoshika nafasi ya pili, wakati kwa Toto imezidi kujichimbia kaburi.
Katika mechi hiyo iliyochezeshwa na refa Andrew Shamba, aliyesaidiwa na Abdallah Mkomwa na Abdallah Rashid, hadi mapumziko ngoma ilikuwa ngumu.
Timu zilicheza soka isiyo na mashambulizi ya kusisimua, zaidi mipira iliishia nje ya eneo la hatari na mashuti machache ya mbali yalikwenda nje.
Burudani ilikuwa katika eneo la kiungo, Toto ikiongozwa na Emmanuel Swita na Yanga walikuwa na Haruna Niyonzima.
Dakika ya 42 almanusra Niyonzima achapane makonde na Swita. Niyonzima alikasirika jinsi Swita alivyomuingia na kumpokonya mpira na akamvaa kiungo huyo wa Toto, ambaye naye alionyesha yuko tayari kwa lolote, lakini hawakutupiana mikono zaidi ya kutunishiana vifua. 
Hali ya mvua ilionekana kuchangia kupunguza kasi ya mchezo kutokana na nyasi kuteleza, hivyo cheche za wachezaji wenye kasi kama Simon Msuva wa Yanga na Mohamed Jingo wa Toto Africans hazikuonekana.
Kipindi cha pili kilikuwa kigumu pia, hadi pale Toto Africans ilipompoteza mchezaji wake mmoja, beki Eric Mulilo aliyetolewa nje kwa kadi nyekundu dakika ya 67 ndipo mambo yakawa laini kwa Yanga.
Beki huyo alionyeshwa kadi ya pili ya njano baada ya kumchezea rafu Simon Msuva na alipoonyeshwa kadi nyekundu akawa anatoka uwanjani taratibu kiasi cha kuwakera mashabiki wa Yanga walioona anachelewesha muda.
Yanga iliongeza kasi ya mashambulizi baada ya Toto kupoteza mchezaji mmoja na hatimaye katika dakika ya 78, krosi maridadi ya Hamisi Kiiza iliunganishwa nyavuni na Nizar.
Mpira wa krosi hiyo kwanza ulimpita Msuva aliyejaribu kutaka kuunganisha kimiani na Nizar akauwahi pembezoni mwa lango kwenye kona ukiwa unataka kutoka na kuutumbukiza nyavuni kwa guu lake la kushoto.   
Katika mchezo huo, kikosi cha Yanga SC kilikuwa; Ally Mustafa ‘Barthez’, Godfrey Taita/Didier Kavumbangu dk73, David Luhende, Mbuyu Twite, Kevin Yondan, Athumani Iddi ‘Chuji’, Simon Msuva, Frank Domayo, Jerry Tegete/Nizar Khalfan dk64, Hamisi Kiiza na Haruna Niyonzima.
Toto Africans; Eric Ngwengwe, Eric Mulilo, Robert Magadula, Eric Kyaruzi, Everist Maganga, Hamisi Msafiri, Severine Constantine/Heri Mohamed dk60, Emmanuel Swita, Chika Olugbe/Suleiman Kibuta dk 62, Mussa Mussa/Simba Boaz dk 90 na Mohamed Jingo.  
Katika mechi nyingine ya ligi hiyo, Azam FC ilitoka sare ya 1-1 na Polisi Morogoro kwenye Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam, hivyo kufikisha pointi 37.
John Raphael Bocco alitangulia kuifungia Azam FC dakika ya nne na Mokili Rambo akaisawazishia Polisi kwa penalti dakika ya 55. 
Penalti hiyo ilikuwa ya utata, kwani beki David Mwantika alioneka akuunawa mpira huo nje ya eneo la hatari dakika ya 53 na baada ya mabishano ya hapa na pale, ndipo ikapigwa na Rambo akafunga.  
Mwantika alionyeshwa kadi nyekundu dakika ya 90, baada ya kurudisha pigo kwa kumpiga kiwiko Rambo.

No comments:

Post a Comment