Maandamano ya mgeni rasmi na viongozi wa GTI na TGNP
Bendi ya Jeshi la Polisi Tanzania ikiwajibika katika mahafali hayo.
Mgeni rasmi, John Mnyika akizungumza.
Mwenyekiti wa Bodi ya GTI, Marry Rusimbi akisoma hotuba yake.
Mkuu wa Chuo cha Mafunzo ya Jinsia, Dk. Diana Mwiru akihutubia katika hafla hiyo.
Na Joachim Mushi
MBUNGE
wa Jimbo la Ubungo kupitia tiketi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo
(CHADEMA), John Mnyika ameahidi kumsomesha mwanafunzi bora wa Chuo cha
Jinsia (GTI) kupitia sehemu ya mshahara wake wa ubunge.
Mbunge
huyo alitoa ahadi hiyo jana jijini Dar es Salaam katika sherehe za
Mahafali ya Kwanza ya Chuo cha Jinsia, GTI alipokuwa mgeni rasmi.
Alisema anatambua mchango wa chuo hicho katika kuiandaa jamii kupigania
usawa wa rasilimali za taifa, hivyo kupitia mshahara wake wa ubunge
atatoa mchango wa kumlipia ada mwanafunzi bora wa chuo hicho mwakani.
Mbunge
huyo aliupongeza uongozi wa GTI kwa mafanikio waliofikia ya kuanzisha
chuo kinachotoa mafunzo ya jinsia kwa jamii na kushauri uongozi
kujipanga na kuwasilisha ombi la kuomba fungu la fedha kutoka Mfuko wa
Mbunge wa Maendeleo wa Jimbo ili kukiwezesha chuo hicho kufanya shughuli
zake kiufanisi.
Awali
akizungumza katika mahafali hayo, Mkuu wa Chuo cha GTI, Dk. Diana-Bupe
Mwiru alisema mahafali hayo ni ya kihistoria kutokana na kwamba
yanafanyika kipindi ambacho Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP) ambao ni
wamiliki wa chuo hicho wakisherehekea miaka 20 tangu kuanzishwa kwa
taasisi hiyo.
"TGNP
inasherehekea miaka 20 ya harakati za ukombozi wa mwanamke kimapinduzi
dai kuu likiwa rasilimali za nchi kunufaisha watu wote na hasa wale
walioko pembezoni. Mwanamke wa kitanzania amekuwa miongoni mwa makundi
yaliyoko pembezoni kutokana na mila na sheria kandamizi ambazo
zilishindwa kutambua mchango wa mwanamke katika jamii na majukumu
makubwa ambayo ameyabeba ili kuhakikisha kuwa jamii inaendelea kuwepo,"
alisema Dk. Mwiru.
Aliongeza
kuwa GTI tangu kuanzishwa kwake imekuwa ikitoa mafunzo kwa umahiri
mkubwa katika soko la ndani na nchi za jirani, huku kikiwa kimefundisha
washiriki zaidi ya 6000 kutoka nchi za Msumbiji, Nigeria, Malawi,
zambia, Kenya, rwanda, Uganda, Ethiopia, Norway pamoja na Tanzania
yenyewe.
"Kutokana
na umahiri wake katika kutoa mafunzo GTI imeweza kutambuliwa kimataifa
kama chuo kilichotukuka katika kutoa maarifa na stadi katika nyanja ya
jinsia na maendeleo kwa Afrika Mashariki na Kati. Kwa GTI hii ni hatua
ya mafanikio ambayo tuna kila sababu ya kujivunia," alisema Mkuu wa Chuo
hicho.
Aidha
Dk. Mwiru alitoa shukrani kwa mashirika mfadhili wa GTI ambayo ni
'Foundation for Civil Society, UN Women, UNFPA, Deloitte, Action Aid na
SIDA kupitia TGNP na RATN ambayo yamekuwa sehemu ya mafanikio ya chuo
hicho. Ikiwa ni pamoja na kuiomba Serikali pamoja na taasisi zake nayo
kuanza kukitumia chuo hicho.
Akizungumza
kabla ya kumkaribisha mgeni rasmi, Mwenyekiti wa Bodi ya GTI, Profesa
Saida Othman aliiomba Serikali kushughulikia changamoto ya ubora wa
elimu kiujumla kwani matokeo yanavyokuwa mabaya hata vyuo vinavyotegemea
wanafunzi hukosa wanafunzi wenye sifa kujiunga na vyuo hivyo.
Jumla ya wahitimu wa 11 walifanikiwa kutunukiwa vyeti vya mafunzo ya jinsia katika mahafali hayo ya kwanza.
No comments:
Post a Comment