Na Abdallah Khamis
NENDA Mwangosi nenda si kama nimekudharau kwa muda wote kukaa kimya
juu ya madhila yaliyokukuta hapana Daudi ningali ninaisikia sauti yako
ikiwaeleza maaskari wale katili kuwa wewe si muhalifu ni mwandishi wa
habari unayetimiza majukuimu yako.
Inanijia picha yako kila mara ninapotaka kuandika kuhusiana na wewe
Daudi, namna ulivyokuwa ukijitahidi kuinuka katika kundi la watesi
wako huku ukiishiwa nguvu hata kufikia kushindwa kusimama baada ya
kipigo cha marungu teke na ngumi zilizokuwa zikikufikia.
Machozi yananitoka Daudi si kwa sababu umekufa tu bali umekufa kinyama
mbele ya kamanda wa Polisi mkoani Iringa, hukustahili kifo kile na
hata sauti yangu haikuweza kuwazindua madhalimu wale waliokuwa
wakikugombania mithili ya Mwizi, mnyang’anyi au dudu lisisloastahili
kuonekana katika uso wa Dunia.
Wamekuuwa Daudi ukitimiza majukumu yako ya kutaka kuwahabarisha
watanzania juu ya kile kilichokuwa kinaendelea katika kijiji cha
Nyololo kwa kuwa kamera yako ilibeb vitu vingi vilivyokuwa vinaendelea
pale ikiwa ni pamoja na namna walivyokuwa wakimimina mabomu ya Machozi
katika jingo la ofisi ya Chadema
Kaka yangu Daudi huenda kazi yako hiyo iliwatisha zaidi Polisi baada
ya kuona wanachokifanya hakiendani na dhamira halisi ya kutuliza
ghasia kwa kuwa sasa walihamishia machungu yao katika jengo ambalo
sina hakika kama lilikuwa na watu ndani au la.
Kwa sababu ulitaka kuonyesha upuuzi wao huo ndiyo maana hata kamanda
wa Polisi Michael Kamuhanda nilipomwambia akusaidie wasiendelee
kukudhuru hakuthubutu kuinua mkono au kupaza sauti yake kukuhami ili
kuonyesha thamani yako kwake, na hii inanifanya niamini ni kutokana na
maswali mazito uliyokuwa ukimuuliza kuanzia asubuhi na hata pale
katika eneo la tukio kabla ya mauti hayajakufika.
Kwanini Daudi uliuliza maswali ya msingi kutaka kujua maana ya kikao
cha ndani kama ni lazima watu wakae ndani ya jengo ama ni kile
kinachowahusisha wanachama peke yao, ambayo dhahiri yalimkera Rpc
Kamuhanda hadi akakuangalia kwa chuki na kukueleza “inaonekana
hujashiba majibu yangu ya tokea asubuhi eeh”aahh Mwangosi tulicheka
pamoja juu ya maelezo ya majibu ya Kamuhanda kumbe sikujua kuwa ndiyo
kicheko chako cha mwisho hapa duniani.
Daudi ni wewe uliyemwambia Kamuhanda kuwa waandishi wanataka
kujiridhisha na hali halisi ili wasipotoshe pale alipokerwa na
Mawswali ya Mwandishi Renatus Mutabuzi hata Kamanda huyo akafikia
kumwambia wewe kijana ninakufahamu.
Hukukaa kimya Mwangosi wakati RPC Kamuhanda alipokuwa akilalamika kuwa
mimi tokea asubuhi ya septemba 2 katika ukumbi wa mikutano ya jengo
la Polisi mkoani Iringa nilikuwa nikimuuliza maswali aliyotafsiri kuwa
ni tofauti na muono wake “Negative”.
Mwangosi tumshukuru mungu hakutupa nguvu ya kubaini yatakayotokea
mbele yetu vinginevyo tungeweza kubaini kuwa yale malalamiko ya RPC ni
maagizo kwa vijana wake kuwa tunamkera hivyo ni lazima waandishi
washughulikiwe.
Kama tungeweza kubaini yajayo juu ya maisha yetu Mwangosi basi
tusingewasogelea wale amabo mimi ninaamini kuwa ndiyo wauaji wako hata
kama wengine watakuja na tafsiri tofauti juu ya hilo.
Mwangosi umeenda na juzi wamekulaza katika eneo la Itete huko Tukuyu,
ninachoweza kushuhudia kauli yako sasa ni kwamba hukuogopa kifo bali
uliogopa kuishi milele.
Mwangosi ni wewe asubuhi ya Septemba 2 wakati tukitaniana na baadhi ya
askari waliovaa kiraia tulipokuwa tunatoka katika mkutano kwa RPC wa
Iringa uliwaambia huogopi kufa kwa kuwa hiyo ni ada ya kila mwanadamu
na kwamba utaogopa ikiwa utaambiwa utaishi milele, sasa umenifahamisha
kuwa ulikuwa ukiishi vile ulivyosema.
Daudi wasio kuwepo katika eneo la tukio wamekuja na kauli zao za ajabu
kuwa mara ulikuwa umejifunga bomu mara umerushiwa kitu kizito kutoka
kwa wafuasi wa Chadema na hata sasa wakati umelala katika nyumba yako
ya Milele tayari kuna tume imeundwa kuchunguza njia iliyotumika
kukufikisha wewe katika makazi ya Milele.
Najua kuna uwezekano wakaja na majibu tofauti ambayo yatakuwa
yameandikwa katika makaratasi na kuita ripoti ya uchunguzi, naomba
nikuhakikishie sitokusaliti sasa na hata kesho katika kuufahamisha
umma kuwa ulilipuliwa na kitu kilichotoka katika mtutu wa bunduki
ulielekezwa kwako na mmoja wa askari waliokuzunguka hata baadhi ya
nyama ya mwili wako kurukia katika nguo zangu.
Sisemi hivi kwa kuhadithiwa Daudi niliyashuhudia mateso yako na hata
sauti yangu na mikono yangu iliyokuwa ikigonga gari la mkuu wa Polisi
mkoani Iringa nikitaka wakusaidie vitakuwa shahidi siku
nitakayokusaliti.
Mwisho
No comments:
Post a Comment