Friday, January 4, 2013

RAIS KIKWETE AONGOZA MAZISHI YA SAJUKI

 Baadhi ya wasanii wakiwa katika mazishi ya msanii wa filamu marehemu Sajuki. (Picha zote na habari Mseto Blog)
 Rais Jakaya kikwete akizungumza na Meya wa Ilala Jerry Silaa (kulia) na Rais wa Shirikisho la Filamu, Mwakifyamba
 Mbunge wa Kigoma Kaskazio, Zitto Kabwe akizungumza na waandiushi wa habari jinsi alivyoguswa na msiba wa Sajuki
 Mamia ya wakazi wa jijini wakiwa katika mazishi ya Sajuki.
 Nahodha wa timu ya taifa ya Tanzania 'Taifa Stars' Juma Kaseja (katikati) akiwasili katika makaburi ya Kisutu Dar es Salaam leo.
Mmiliki wa mtandao wa kijamii wa Blog ya Nkoromo Daily, Bashiri Nkoromo (kulia) akiwa na Msanii wa filamu, Hamis Magari wakati wa mazishi ya Sajuki yaliyofanyika katika makaburi ya Kisutu jijini Dar es Salaam leo.
Baadhi ya wasanii wa filamu nchini, kutoka kushoto, Hamis Mwinjuma Mwana FA’, Issa Mussa ‘Cloud’, Hisson Muya ‘Tino’, na Singo Mtambalike ‘Richie Richie’, wakishiriki kubeba jeneza lenye mwili wa marehemu Juma Kilowoko ‘Sajuki’, wakati wa mazishi yake yaliyofanyika leo kwenye makaburi ya Kisutu jijini Dar es Salaam.
Rais Jakaya Mrisho Kikwete akiwa na baba mzazi wa marehemu Sajuki  wakati wa mazishi ya msanii huyo  leo katika makaburi ya Kisutu jijini Dar es salaam
Rais Jakaya Mrisho Kikwete akiweka udongo kaburini wakati wa mazishi ya msanii Sajuki leo katika makaburi ya Kisutu jijini Dar es salaam
 Rais Jakaya Mrisho Kikwete akiweka udongo kaburini wakati wa mazishi ya msanii Sajuki leo katika makaburi ya Kisutu jijini Dar es salaam.



DAR ES SALAAM, Tanzania

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Kikwete, jana aliongoza mamia ya waombolezaji, wakiwamo wabunge na viongozi wa vyama vya siasa katika mazishi ya aliyekuwa mtayarishaji na msanii wa filamu nchini, Juma Kilowoko ‘Sajuki’ aliyefariki dunia Januari 2 mwaka huu baada ya kusumbuliwa na maradhi ya kansa ya damu.

Rais Kikwete aliwasili katika Makaburi ya Kisutu yalikofanyika mazishi hayo saa 7:30, dakika tano kabla ya mwili wa Sajuki kuwasili hapo ukitokea kusaliwa msikitini Kariakoo, tayari kwa mazishi hayo yaliyoteka hisia za wengi na kukusanya kundi kubwa la wasanii na wadau wengine wa sanaa.

Mbali ya wasanii, vijana wa rika mbalimbali walijitokeza nyumbani kwa marehemu Tabata Bima na kuupokea mwili, wakiongozwa na Mbunge wa Kigoma Kaskazini na Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo, (Chadema), Kabwe Zitto, Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Bara, Mtatiro Julius, Mbunge wa Iramba Magharibi na Naibu Katibu Mkuu Chama Cha Mapinduzi (CCM), Mwigulu Nchemba.

Mwili wa marehemu uliwasili nyumbani kwake Tabata Bima majira ya saa 3 asubuhi na baada ya kusomewa dua, uliondolewa na kwenda kuswaliwa katika msikiti wa Kariakoo kisha kwenda kuzikwa makaburi ya Kisutu, ambako Rais Kikwete aliungana na waombolezaji wengine kumzika Sajuki.

Kikwete alivyowasili makaburini

Rais Jakaya Kikwete aliwasili makaburi ya Kisutu saa 7:30 akiingia kupitia geti namba mbili, huku akiwaacha ‘solemba’ wapiga picha wa magazeti na televisheni waliokuwa wamejipanga katika geti kuu la makaburi hayo.
Ujio wake ulisababisha kukimbizana kwa wapiga picha hao kutoka geti kuu kuja geti dogo lililokuwa karibu kabisa na lilipochimbwa kaburi la Sajuki, ambapo dakika chache baadaye mwili wa marehemu uliingia makaburini hapo.

Mvutano mkubwa wa kuwania upigaji wa picha za rais pamoja na jeneza la mwili wa marehemu zilishika hatamu na kusababisha usumbufu kwa walinzi wa Rais, waliokuwa wakijaribu kuwatenganisha wahudhuriaji na njia za kupitisha jeneza kuelekea kaburini.

Baada ya kusimama kwa dakika zipatazo 10 hadi mwili wa marehemu kufika na kuingizwa kaburini, Rais Kikwete alitakiwa kuchota mchanaga na kutia kaburini kama ishara ya kumzika Sajuki na kisha watu wengine wa familia nao kuendelea na zoezi hilo.

Rais Kikwete akaruhusiwa kutoka pembeni ya kaburi, ambako alitengewa viti maalumu alikokaa na walinzi wake, huku akisubiri kumalizika kwa mazishi hayo, ili aondoke makaburini hapo.

Sita waliomzika Sajuki watajwa

Wakati hali ikiwa ya vurugu ikiwamo baadhi ya wanahabari na waombolezaji wengine kupanda juu ya miti kuweza kushuhudia kinachojiri na kisha kushushwa na walinzi wa Rais, watu sita waliopata bahati kuingia kaburini kumzika Sajuki walitangazwa.

Katika matangazo hayo ambayo pia yalielekeza namna sahihi ya kusimama kushuhudia tukio hilo, Baba mzazi wa Sajuki, Saidi Kilowoko alitajwa kuongoza wazikaji hao, akifuatiwa na baba mkubwa, Idd Issa Kilowoko.

Wengine waliopata nafasi hiyo walikuwa ni kaka wa marehemu Issa Kilowoko, shemeji wa marehemu Issa Juma, mwakilishi wa wasanii Issa Mussa ‘Claudi’ na mtu mmoja aliyetajwa kwa jina la Salum Ahmed.

Ving’amuzi vya Startimes gumzo mazishini

Katika hali isiyokuwa ya kawaida, teknolojia mpya ya dijitali iliyoanza kutumiwa kurusha matangazo ya televisheni usiku wa Januari 1, 2013 yalishika hatamu katika mazishi hayo, ambapo waombolezaji walionekana kulalamikia huduma hafifu za ving’amuzi vya kampuni ya Startimes.

Waombolezaji hao walikiri kupata wakati mgumu kutumia huduma hiyo, huku baadhi ya wasanii wakionekana kufurahia kwa madai kuwa ndio wasaa halisi utakaowawezesha Watanzania kuangalia kwa mapana kazi zao za sanaa na kuchangia pato lao.

Mmoja wa wasanii hao ambaye hakutaka kutaja jina gazetini, alikiri kuumia moyoni kutokana na vilio vya Watanzania kutomudu gharama za ving’amuzi na kutofanya kazi kwa baadhi ya walio na uwezo wa kuvinunua, lakini akakiri sanaa zao sasa zitatazamwa.

“Nawahurumia Watanzania wanaoshindwa kununua, lakini pia walionunua na kutopata walichotegemea. Lakini naamini huu sasa ni wakati wa wasanii kuonekana sana kwa kazi zao, kwani mitaani DVD ndio zinauza zaidi kwani TV hazina ving’amuzi,” alisema.

Kauli hiyo iliungwa mkono na baadhi ya wasanii waandamizi, wakiwamo wanachama wa Shirikisho la Filamu Tanzania (Taff), ingawa pia hawakusita kuiomba Serikali kuvipatia ufumbuzi vilio hivyo vya wananchi ambao ni wadau wao wakubwa.

Familia, Taff kuamua juu ya 40 ya Sajuki

Wakati baba wa marehemu Sajuki akitakiwa kuungana na Rais Kikwete kwa mazungumzo mafupi na kisha kuondoka makaburini hapo, MC wa shughuli hiyo alifikisha kwa wazikaji taarifa muhimu kuhusu shughuli ya 40 ya msiba huo.

“Familia ya Sajuki na wasanii nchini, wanapenda kuwashukuru wote kwa kufanikisha mazishi haya. Haina cha kuwalipa, ila Mungu atawalipa. Familia itakaa na Taff, kisha itawatangazia tarehe maalum ya sahughuli ya 40 ya Sajuki, ila kwa sasa hakutakuwa na matanga,” alisisitiza MC.

Idd Azzan, Zito Kabwe wanena mazishini

Kwa nyakati tofauti wakati wa mazishi hayo, wabunge na wanasiasa waliofika makaburini hapo walitumia fursa zao kumuelezea Sajuki, masikitiko waliyonayo kwa kifo chake na saana kwa ujumla.

Wabunge hao ambao walikuwa sambamba na Meya wa Ilala, Jerry Silaa, ni pamoja na mbunge wa jimbo la Kinondoni, Idd Azzan, mbunge wa Kigoma Kaskazini Zito Kabwe na yule wa Mchinga, Said Mtanda.

Azzan alisema kwa kifo cha Sajuki ni pigo katika tasnia ya sanaa na soko la filamu nchini, ambapo aliwataka wasanii kuunganisha nguvu katika shirikisho lao, ili kusukuma mbele harakati za kuleta maendeleo yao na tasnia kwa ujumla.

Azzan, pia alitoa pole kwa ndugu na jamaa, akiwamo mke wa marehemu aliyemtaja kama mwanamke shujaa aliyekabiliana bila kuchoka katika harakati za kuokoa maisha ya mumewe, hadi Mungu alipomtwaa.
“Wasanii kwa sasa waendeleze umoja wao ikiwamo kujiunga na Shirikisho lao (Taff), ili kuiwezesha Serikali na mashirika mengine kumudu kuwasaidia kwa pamoja, tofauti na hali ya sasa,” alisema Azzan.

Pia Azzan alisema kuwa, atakutana na wabunge wa majimbo ya Dar es Salaam na kuona namna ya kuja kuwasaidia wasanii kwa namna moja ama nyingine,  ili waweze kujitambua na kutambua haki na hadhi zao sambamba na kuwashauri kuanzisha mfuko maalum  wa kuwainua.

Kwa upande wake, Mbunge wa Mchinga (CCM) Said Mtanda, alisema kifo cha Sajuki ni pigo kwa wanaharakati waliojitoa kupigania haki za wasanii hapa nchini kupitia kazi zao hasa juu ya kudhulumiwa haki zao kwa kurudufisha.

“Mimi nilikutana na Sajuki siku chache kabla ya kifo chake pale Muhimbili, na niliongea naye machache na kubwa alikuwa akilalamikia wizi wa kazi zao unaofanya na wasambazaji wao wa ‘Kidosi’’ alisema Mtanda.
Mtanda ambaye pia yupo kwenye Kamati ya  Maendeleo ya Jamii, alisema wabunge wamekuwa wakipigania haki za wasanii ikiwemo suala la stika maalum ambazo zitawasaidia kukuza pato lao endapo wataujua vizuri mpango huo kwa kushirikiana na mamlaka husika ikiwamo TRA na Chama cha Haki Miliki (COSOTA).

Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe, alisema pengo lililoachwa na Sajuki katika utayarishaji na uigizaji wa filamu Tanzania, halitazibika kwa sasa kutokana na mchango wake aliokuwa akiutoa enzi za uhai wake na kuwataka wasaniii kuwa kitu kimoja katika kipindi hiki kigumu.

Aidha, wananchi waliojitokeza katika mazishi hayo kwenye makaburi ya Kisutu, waliungana na kauli za wabunge hao na kuwataka wasanii kuendeleza umoja wao na kujipanga katika kipindi hiki kigumu.

Kuugua kwa Sajuki na alikotokea kisanii

Marehemu Sajuki alianza kuugua mwaka 2010 na kupatiwa matibabu nchini India katika kipindi hicho na kwa mara ya pili, alikwenda India mwaka 2011 kwa fedha ambazo zilitokana na michango ya wasamaria.
Sajuki alifikwa na umauti akiwa kwenye harakati za kupelekwa kwa mara nyingine nchini India kwa matibabu zaidi, lakini mapenzi ya Mungu yakatimia.

Marehemu Sajuki alianza kujishughulisha na kazi za sanaa akiwa kati ya wasanii waliokuwa wakiunda kundi la sanaa la Kaole, kabla ya kulipa kisogo.

Baada ya hapo akawa anafanya kazi za kujitegemea kama mtayarishaji, muigizaji na mzalishaji wa filamu ambako ndiko alikoanza  kupata mafanikio makubwa.

Sajuki aliyezaliwa mwaka 1986 mkoani Ruvuma, ameacha mjane na mtoto mmoja wa miezi 10.
Mashabiki wake watamkumbuka kwa kupitia filamu zake zilizompa umaarufu kwa kuzicheza kwa umahiri sambamba na mke wake Wastara, kupitia Kampuni yao ya Wajey Production ambazo ni ‘Mboni Yangu’, ‘Round’, ‘Shetani wa Pesa’, ‘Hero of the Church,’  ‘Vita’,  ‘Briefcase’, ‘Revenge’, ‘Dhambi’,  ‘Two Brothers’  na ‘Behind The Scene’

No comments:

Post a Comment