Thursday, February 21, 2013

ACHENI WIZI WA MAJI!!

Na Magreth Kinabo-Maelezo
WAZIRI wa Maji Profesa Jumanne Maghembe amezitaka  Mamlaka zinazosimamia Usambazaji wa maji safi na maji taka  jijini  Dar es Salaam (DAWASCO na DAWASA) kuhakikisha  tatizo la  wizi  wa  maji linatafutiwa ufumbuzi, huku  akionya kuwa mfanyakazi  atakayehusika atafukuzwa kazi.

Akizungumza na wafanyakazi wa mamlaka hizo Dar es Salaam   Prof.Maghembe amesema jumla ya maji lita mil 300 yaliitajika kusambazwa lakini kutoka katika vyanzo vikuu vya maji lakini kutokana na kuwepo kwa utaratibu mbovu inasababisha asilimia 56 ya kupotea ambapo kati ya hizo asilimia 30 yanaibwa na kudai kuwa wanawajua na kuwafahamu wezi hao.

Amesema mbali na uchakavu wa miundombinu inayosababisha maji kupotea pia alizitaja sababu nyingine ni  mgawo wa upelendeleo  unafanywa na baadhi ya viongozi  katika kusimamia maji hayo ili waweze kujipatia chochote.


Prof.Maghembe amewataka maofisa wanaosimamia  mgawo wa maji kuacha kudanga watu kwa kuwapa maji kwa masaa machache wakati ni haki yao kwa siku hiyo kupata maji kama utaratibu ulivyo.

"Nataka muwe wazalendo katika kuwatendea haki wananchi kwa kuwapa maji badala ya kuwasambazia rafiki zenu wauza maji ili mpate mshiko,nikigundua kuna sehemu maji hayakupelekwa meneja husika na wafanyakazi wake nitawafukuza kazi papo hapo"alisema.

 Alidai kuwa  baadhi ya wafanyazi wakishirikiana na wauza maji kwa kuwafungia mitambo akitolea mfano katika eneo la Mkwajuni ambapo kuna mfanyabiashara ambaye anasambaza maji hadi katika maeneo ya Mwanyamala ingawaje mitambo hiyo ilishaondolewa ila cha kushangaza hadi juzi imefungwa tena.

"Bomba hilo la Mkwajuni ni kubwa mtu wa kawaida hawezi kufunga mitambo hiyo hata hivyo kuna mitambo kumi katika maeneo hayo ambayo nayo inaiba maji"alisema

Prof.Maghembe alisema kutokana na mazingira hayo kwa namna moja nyingine mnahusika kwa kuhujumu maji hivyo hatuwezi kukubali tabia hiyo.
   .
"Sikubali kuona wafanyakazi ambao wanahujumu mashirika  nitawachukulia hatua wale wote watakaokamatwa pamoja na kuwafukuza kazi mara moja "alisema Prof Maghembe.

Prof Maghembe aliwataka Wenyeviti wa mashirika hayo kuhakikisha kuwa watu wote wanauza maji  na malori wajiandikishe na kutambuliwa  kisheria na DAWASCO, maji wanayoyauza yawe safi, wawe na mita , leseni  , namba ya mplipa kodi , pia bei ya kuuza  maji idhibitiwe na EWURA .

Alitaka zoezi hili lianze  kuanzia  Mwezi Machi hadi April 30, mwaka huu  liwe limekamilika. 
     
"Hivyo nataka wizi wa maji ifikie asilimia zero mara moja kwani hatuwezi kubadilisha maisha  yenu wakati maji yanapotea. Ninyi mabwana maji acheni vituko haiwezekani mnafanya mambo haya mpewe heshima   ya kuwahudumia Watanzania."alisisitiza Prof Maghembe.

Aliwaomba wananchi na wafanyakazi wengine kuwataja wezi kwani atakayetaja atalipwa sh.100,000 na atalindwa.

No comments:

Post a Comment