Friday, February 15, 2013

Familia ya Joseph Nyerere haimtambui mtuhumiwa Makongoro


 
Familia ya mdogo wake Hayati  Mwalimu Julius Kambarage Nyerere,  Marehemu Joseph Nyerere, imejitokeza na kusema haimtambui mtuhumiwa wa kesi ya mauaji, anayejitambulisha kwa jina la Makongoro Joseph Nyerere.

Taarifa iliyotolewa na Nuru Nyerere-Inyangete, kwa niaba ya familia hiyo jana, ilisema hadi kifo cha baba yao, Joseph Kizurira Nyerere, mwaka 1994 haina taarifa zozote za kuwa na ndugu yao anayeitwa Makongoro Joseph Nyerere.
Hadi baba anafariki dunia hatukuambiwa tuna ndugu anayeitwa Makongoro Joseph Kizurira Nyerere …watoto wote wa Mzee Joseph tunafahamiana, lakini kwa huyu ndiyo kwanza tunaambiwa kuwa ni ndugu yetu. Tunauhakikishia umma kwamba hadi kifo cha baba yetu hatukuambiwa juu ya kuwapo kwa ndugu mwenye jina hilo, hii ina maana kwamba hatumtambui.
Naye mtoto mwingine wa Joseph, Matare, alisema:
Tangu kutangazwa kwa habari hizi tunapata simu nyingi za pole. Tunashangaa kwa sababu huyu mtu hatukuwahi kuambiwa kuwa ni ndugu yetu, na wala yeye mwenyewe hakuwahi kuja kwetu kujitambulisha kama ni mmoja wa watoto wa Mzee Joseph.

Tumesoma kwa mshituko kwenye magazeti ya Februari 14, 2013 na katika mitandao ya kijamii, kuwa kuna mtu anayejiita Makongoro Joseph Nyerere. Huyu huyu hatumtambui kwa uhusiano, taarifa wala sura. Watoto wote wa marehemu Joseph Nyerere wanafahamika, hakuna mtoto wa marehemu mwenye jina hilo.
Juzi, Makongoro ambaye ni mfanyabiashara, mkazi wa Dar es Salaam, alifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini humo akikabiliwa na mashitaka ya mauaji ya mfanyabiashara mwenzake, Onesphory Kitoli. Mtuhumiwa huyo anatarajiwa kuunganishwa katika kesi hiyo na mtuhumiwa mwingine mfanyabiashara maarufu, Marijani Abubakari marufu kama Papaa Msofe (50). Kesi hiyo itatajwa Februari 20, mwaka huu.

Wakili wa Serikali, Charles Anindo, alimsomea Makongoro mashitaka mbele ya Hakimu Mkazi, Agnes Mchome, na kudai kuwa Novemba 6, 2011 huko Magomeni Mapipa, Makongoro alimuua kwa makusudi Kitoli kinyume na kifungu cha 196 cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu ya mwaka 2002.

Anindo alidai kuwa upelelezi wa kesi hiyo haujakamilika na aliomba Mahakama iahirishe kesi hiyo hadi Februari 20, mwaka huu, ambako Makongoro ataunganishwa na Papaa Msofe kwenye mashitaka hayo.

Mtuhumkiwa hakutakiwa kujibu chochote kwa kuwa Mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi za mauaji.

---
via Michuzi blog

No comments:

Post a Comment