Friday, May 3, 2013

UKOSEFU WA MADAWA YA AKILI CHANZO CHA KUONGEZEKA KWA MAGONJWA YA AKILI KILIMANJARO


 
UKOSEFU wa dawa za magonjwa ya akili katika hospitali na vituo vya afya mkoani Kilimanjaro, umeelezewa kuwa tatizo kubwa linalosababishakasi ya ugonjwa huo kuzidi kuongezeka, na kuwatesa wananchi wengi wa mkoa huo.

Takwimu zinaonyesha kuwa watu wanaougua ugonjwa huo wameongezeka kutoka 10,286 katika kipindi cha waka 2011 hadi kufikia 15,838 mwaka 2012.

Hayo yalibainishwa jana na kaimu mratibu wa magonjwa ya akili mkoani Kilimanjaro Bi. Ester Maro, wakati akizungumza na gazeti hili ofisini kwake kuhusiana na hali ya ugonjwa huo na jitihada ambazo zimekuwa zikichukuliwa na serikali katika kukabiliana na tatizo hilo.

Bi. Maro ambaye ni afisa muuguzi kitengo cha magonjwa ya akili katika hospitali ya mkoa wa Kilimanjaro Mawenzi, alisema pamoja na ugonjwa huo kuwatesa wananchi wengi, dawa bado ni tatizo kubwa ambalo linakwamisha jitihada za mkoa za kumaliza tatizo hilo.

“Hali ya magonjwa ya akili katika mkoa huu bado si ya kuridhisha,na wagonjwa wanaougua ugonjwa huu wamekuwa wakiongezeka kwa kasi sana kila kukicha,lakini pamoja na tatizo hili kuendelea kuwa kubwa upatikanaji wa dawa umekuwa wa shida sana hali ambayo imekuwa ikiwafanya wananchi wengi hasa wa kipato cha chini kukata tama kutokana na kukosa fedha za kununua dawa hizo kwenye maduka ya dawa ya binafsi”alisema Bi. Maro.

Aidha alisema kukosekana kwa dawa kwenye hospitali kunatokana na bohari ya dawa MSD nayo kukosa dawa hizo hali ambayo imekuwa ikiwafanya madaktari na wauguzi katika vitengo vya magonjwa ya akili kuwaagiza wagonjwa kwenda kununua dawa kwenye maduka ya dawa.

“Dawa za magonjwa ya akili zinauzwa kwa gharama kubwa katika maduka ya dawa,hali hii huwakwaza wagonjwa wengi na kuwafanya waache kutumia dawa na kuishia mitaani,lakini pia tatizo hili la ukosefu wa dawa limezifanya familia nyingi kuwatenga wagonjwa wa akili kwa kuona hawawezi kuwahudumia hivyo kuishia kuishi mitaani na kula majalalani”alisema

Kutokana na hali hiyo Bi. Maro aliishauri serikali kuangalia uwezekano wa kuongeza bajeti ya dawa ili kupunguza tatizo hilo ambalo limekuwa kero na kikwazo kikubwa kwa wagonjwa.

Akizungumza na TAIFA LETU.com, mganga mfawidhi wa Hospitali ya mkoa wa Kilimanjaro Mawenzi Dkt.SagandaKapalala alikiri kuwepo kwa tatizo kubwa la ukosefu wa dawa za magonjwa ya akili na kusema kuwa hali hiyo imekuwa ikiwasumbua na kuwaumiza kichwa madaktari na wauguzi wa kitengo hicho.

Alisema kutokana na tatizo hilo Hospitali imekuwa ikijitahidi kununua dawa zamagonjwa hayo ili kupunguza tatizo na kuwasaidia wagonjwa ambao wengi wao hawamudu gharama za dawa.

“Tatizo la dawa za magonjwa ya akili linaninyima usingizi,kwani limekuwa tatizo kubwa na wagonjwa wanapofika hospitali na kuagizwa wakanunue dawa huwa wanaona kama wanaonewa kutokana na kwamba hospitali dawa hizi huwa zinatolewa bure,niwaombe MSD wajitahidi kuagiza dawa hizi ili kutupunguzia mzigo na tatizo”alisema

No comments:

Post a Comment