Saa chache baada ya Rais Jakaya Kikwete kuwasihi viongozi na waumini wa
dini za Kikiristo na Kiislamu nchini kuwa wavulilivu na kujiepusha na
vitendo vya kulipiza visasi, Kanisa la la Pentekoste (MMPT) lililopo
Buronge katika Manispaa ya Kigoma/Ujiji limechomwa moto na kutetekezwa
kabisa na watu wasiojulikana.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kigoma,
Frasser Kashai, alisema jana kuwa tukio hilo lilitokea juzi usiku majira
ya saa 4:00 usiku katika eneo la Buronge mjini Kigoma.
Kashai
alisema kanisa hilo lilichomwa na watu wasiojulikana na kwamba mali
mbalimbali zenye thamani ya Sh. 1,337,000 ziliteketea.
Alisema
sababu za kuchomwa kwa kanisa hilo hazijafahamika na kwamba hakuna mtu
aliyejeruhiwa huku upelelezi wa tukio hili ukiendelea ili kuwabaini
wahalifu hao kabla ya kuchukuliwa hatua za kisheria.
Mchungaji wa
Kanisa hilo, Emmanuel Simon, alisema: “Nilipata taarifa kuwa kanisa
langu limeteketea kwa moto, nilikwenda Polisi Central kutoa taarifa
ndipo tulikwenda eneo la tukio tukakuta kanisa lote limeteketea kwa
moto.”
Alisema katika kanisa kulikuwa na mabechi 14, mlango
mmoja, virago vitatu, masanduku ya sadaka na ubao wa kufundishia, vyote
vikiwa na thamani ya Sh. 1,337,000.
Mchungaji Simon alisema hajui
watu waliochoma kanisa hilo na kuiomba serikali iangalie matukio ya
uchomaji wa makanisa yanayoendelea nchi nzima.
Pia, alilitaka Jeshi la Polisi kufanya doria kwenye makanisa wakati wa usiku ili kukomesha vitendo vya uchomaji wa makanisa.
Alisema
kanisa ni taasisi ya jamii, hivyo anaomba serikali ichangie gharama ya
ujenzi wa jengo hilo ili wananchi wanaoabudu katika kanisa hilo wapate
sehemu ya kuabudia.
---
Ni sehemu ya taarifa kwenye gazeti la NIPASHE
No comments:
Post a Comment