Utangulizi
Mheshimiwa Dkt. Amani Abeid Karume, Makamu Mwenyekiti wa CCM na Rais Mstaafu wa Zanzibar;
Ndugu Pius Msekwa, Makamu Mwenykiti wa CCM wa Bara;
Mwenyekiti Mstaafu wa CCM, Ndugu Benjamin William Mkapa;
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania;
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi;
Waziri Mkuu;
Makamu wa Pili wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar ;
Viongozi Wakuu Wastaafu;
Katibu Mkuu wa CCM, Ndugu Wilson Mukama;
Ndugu Wajumbe wa Mkutano Mkuu wa Taifa wa CCM;
Wageni wetu waalikwa kutoka vyama rafiki,
Ndugu zetu wa Vyama vya Siasa Nchini;
Waheshimiwa Mabalozi,
Viongozi wa Dini,
Wageni Waalikwa,
Mabibi na Mabwana;
Kama
ilivyo ada, naomba tuanze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu, mwingi wa
rehema kwa kutujaalia uzima na kutuwezesha kukutana hapa Dodoma, siku ya
leo, kwenye Mkutano Mkuu wa Nane wa Chama cha Mapinduzi.
Ndugu Wajumbe;
Karibuni
Dodoma. Karibuni Mkutanoni. Nawapeni pole kwa safari. Tunamshukuru
Mungu kwa kutuwezesha kufika salama na tuombe turejee makwetu salama.
Kwa niaba yenu, niruhusuni niwashukuru wenyeji wetu, yaani wana-CCM na
wananchi wote wa Dodoma, wakiongozwa na Alhaji Adam Kimbisa, Mwenyekiti
wa CCM, Mkoa wa Dodoma na Mkuu wa Mkoa Dkt. Rehema Nchimbi, Mjumbe wa
Halmashauri Kuu ya Taifa. Tunawashukuru kwa kutupokea vizuri na kwa
ukarimu wao unaotufanya tujisikie tuko nyumbani katika huu mji ambao
ndiyo Makao Makuu ya nchi yetu na Chama chetu.
Ndugu Wajumbe;
Napenda kuchukua nafasi hii kutoa pongezi nyingi kwa
Halmashauri Kuu ya Taifa kwa matayarisho mazuri ya Mkutano huu wa Nane
wa Taifa wa CCM. Natoa pongezi maalum kwa Sekretarieti ya Halmashauri
Kuu ya Taifa chini ya uongozi mahiri wa Katibu Mkuu Ndugu Wilson Mukama
na Kamati zote za Maandalizi ya Mkutano kwa kazi kubwa na nzuri
waliyofanya ya kuwezesha Mkutano huu kufanyika. Kwenu nyote nasema
hongereni na asanteni sana.
Ndugu Wajumbe;
Karibuni tena Kizota. Nasikitika kwamba matumaini yangu ya kufanya
Mkutano Mkuu katika ukumbi wetu wenyewe hayakutimia. Hii ni kwa sababu
kazi ya matayarisho imechukua muda mrefu kuliko nilivyotazamia.
Tumechelewa kupata kiwanja kilichokidhi mahitaji yetu na matazamio
yetu. Kwanza tulipata kiwanja nyuma ya Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM).
Lakini tukaona ni mbali mno na walipo wananchi. Tukaja kupata kiwanja
kingine juu ya Kilimani Club ambacho hakikuwa kikubwa cha kutosha.
Mapema mwaka huu ndipo tulipopata kiwanja eneo la Makulu ambacho
kinakidhi sifa za kuwa kikubwa cha kutosha na kuwa karibu na katikati ya
mji wa Dodoma. Tumekiafiki na matayarisho ya kuanza ujenzi
yamekamilika. Leo asubuhi tumeweka jiwe la msingi kuzindua ujenzi wa
Ukumbi wa Mkutano (Dodoma Convention Centre). Baadae utafuta ujenzi wa
jengo la Makao Makuu ya CCM na jengo la Hoteli ya Kisasa.
Wageni Karibuni
Ndugu Wajumbe;
Kama
mjuavyo Chama cha Mapinduzi kina marafiki wengi Afrika na kwingineko
duniani. Tumekuwa na mazoea ya kualikana katika mikutano mikuu yetu.
Safari hii tumefanya hivyo tena. Kwa niaba yenu niruhusuni niwashukuru
sana wageni wetu wote wa kutoka vyama rafiki Afrika na duniani kwa
kukubali mwaliko wetu na kuja kujumuika nasi siku ya leo. Kuwepo kwao ni
kielelezo tosha cha udugu na urafiki uliopo baina ya vyama vyetu na
nchi zetu ambao hatuna budi kuudumisha, kuuendeleza na kuukuza. Hali
kadhalika, nawashukuru Mabalozi wa Nchi za Nje na Wawakilishi wa
Mashirika ya Kimataifa walioweza kuja kushiriki nasi katika sherehe za
ufunguzi wa Mkutano wetu.
Ndugu Wajumbe;
Tunawakaribisha
kwa furaha na upendo mkubwa viongozi na wawakilishi wa vyama vya siasa
vya hapa nchini kwa kukubali mwaliko wetu na kuja kuhudhuria Mkutano
Mkuu wa Taifa wa CCM siku ya leo. Tunawashukuru kwa moyo wao wa
uungwana kwani tofauti za vyama si uadui. Wamethibitisha jinsi
demokrasia ya vyama vingi inavyozidi kustawi na kukomaa hapa nchini.
Nawashukuru
sana pia, viongozi wetu wa dini na wananchi mbalimbali waliojumuika
nasi. Kuwepo kwao ni jambo la faraja kubwa. Dua za viongozi wa dini
zitasaidia kuponya na kuupa baraka mkutano wetu uende salama, uwe wa
mafanikio na kuwafanya wale wote wasiokiombea mema Chama chetu
watahayari na kufadhaika.
Karibuni Diaspora
Ndugu Wajumbe;
Napenda
kuwatambua na kuwakaribisha viongozi na wananchama wa Chama chetu
waliopo nje, Marekani, Italia, India na Uingereza. Ndugu zetu hawa kwa
upenzi wao kwa Chama wamesafiri masafa marefu kuja kushiriki nasi. Hawa
wanastahili pongezi maalum kwa jinsi wanavyopeperusha bendera ya CCM na
kueneza sera zake. Naomba tuwape makofi ya nguvu.
Agenda ya Mkutano
Ndugu Wajumbe;
Agenda ya Mkutano Mkuu wa Taifa wa Nane wa Chama cha Mapinduzi ina
mambo makuu manne. Kwanza kufanya marekebisho ya Katiba ya Chama cha
Mapinduzi. Mengi ya marekebisho hayo yanatokana na uamuzi wa
Halmashauri Kuu ya Taifa katika kikao chake cha trehe 11 – 12 Aprili
2011 wa kufanya mageuzi ndani ya Chama. Miongoni mwa matunda ya mageuzi
hayo ni kuundwa kwa Baraza la Ushauri na Wajumbe wa NEC kuchaguliwa
Wilayani badala ya Mikoani.
Kwa mujibu wa Katiba ya CCM,
Halmashauri Kuu ya Taifa ina mamlaka ya kufanya marekebisho ya Katiba na
marekebisho hayo kutumika. Hata hivyo, marekebisho hayo hayana budi
kuletwa katika Mkutano Mkuu wa Taifa ili yaingizwe rasmi kwenye Katiba.
Ndugu Wajumbe;
No comments:
Post a Comment