POLISI mjini Mwanza imebaini kuwa mmoja wa watuhumiwa wa mauaji ya
aliyekuwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Liberatus Barlow, alikwenda
kuaga mwili wa Kamanda huyo katika uwanja wa Nyamagana sambamba na
wananchi wengine.
Kaimu Kamanda wa
Polisi wa Mkoa wa Mwanza, Lily Matola jana alimtaja mtuhumiwa huyo kuwa
ni Abdallah Petro ‘Ndayi’ (32) mkazi wa Mjimwema mjini hapa ambaye
anashikiliwa Polisi.
Kwa mujibu wa
Kamanda Matola, Petro mbali na kutajwa kuhusika na mauaji hayo, pia
anadaiwa kuwa na rekodi ya kufungwa miaka 30 jela katika gereza la
Butimba kwa unyang’anyi wa kutumia silaha mwaka 2006.
Alitoka
gerezani mwaka 2010 baada ya kukata rufaa Mahakama Kuu ya Tanzania.
Petro pia imebainika pia kuwa ni mdogo wa mtuhumiwa wa kwanza katika
kesi hiyo, Muganyizi Peter.
Vielelezo vyakamatwa
Kamanda
Matola alisema mbali na kuwa na uhusiano huo, Petro na mtuhumiwa
mwingine, Abdurahim Ismail Athuman ‘Dula’ (28) mkazi wa Mkudi Ghana, pia
mjini hapa, baada ya kukamatwa kwa nyakati tofauti Mjimwema na
Kilimahewa mwishoni mwa wiki, waliwapeleka polisi mahali walikoficha
baadhi ya mali za marehemu.
Mali
wanazodaiwa kuonesha polisi ni pamoja na redio ya mawasiliano ya Polisi
na funguo za gari alilotumia kamanda Barlow siku ya tukio la mauaji
yake.
Kamanda Matola alisema watuhumiwa
waliwapeleka polisi katika shimo la majitaka kwenye maeneo ya
Nyanshana, jijini Mwanza walipokuwa wameficha vitu hivyo.
Mkuu
wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai, Joseph Konyo alisema watuhumiwa baada
ya kutimiza uhalifu, walitenganisha redio hiyo ya mawasiliano ili
isipatikane.
“Damu ya mtu haipotei
bure, hayo yote ni pamoja na Mungu mwenyewe, kwani sisi peke yetu
hatuwezi, wananchi mmetusaidia sana,” alisema Kamanda Konyo.
Baada
ya kuonesha polisi vitu hivyo ambavyo sasa vimechukuliwa kama vielelezo
katika kesi ya mauaji ya Barlow, Kamanda Matola alisema watuhumiwa hao
walipekuliwa na kukutwa pia na kadi tatu za simu za Vodacom na Airtel,
simu ya mkononi, viatu vya ngozi na begi dogo.
Pia
walikutwa na kofia mbili za kijeshi aina ya bereti; moja ikiwa ya
Polisi na nyingine ya kampuni ya binafsi ya ulinzi, sare za kampuni ya
ulinzi, mtarimbo, bisibisi, mapanga, televisheni mbili, sub-hoofer na
deki.
Alisema walipohojiwa, walidai
wamekuwa wakihifadhiwa na Ryoba Matiku ‘Mama Nyangi’ katika eneo la
Nyakabungo Miembeni ambako mipango yote ya uhalifu imekuwa ikisukwa.
Mama huyo anashikiliwa pia kwa mahojiano.
via gazeti la HabariLeo
No comments:
Post a Comment