Michoro
ya ujenzi wa Kampasi ya Mloganzila iliyo kijijini Kwembe katikati ya
Wilaya za Kisarawe Mkoa wa Pwani na Kinondoni Mkoa wa Dar es salaam. Hii
ni sehemu ya Chuo cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili
(MUHAS) inayojengwa kwenye eneo la ekari
3800 kwa ajili ya kutolea mafunzo kwa wanafunzi wa udaktari na huduma
za Afya wapatao 15,000 kwa mwaka, na pia itakua sehemu ya kutolea
matibabu ya maradhi yote makuu na ya kawaida nchini.
Kwa mujibu wa Makamu Mkuu wa Chuo cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili, ujenzi wa
Hospitali hii, ambayo pesa ya ujenzi wake imeshapatikana, unatarajiwa
kuanza mwishoni mwa mwezi Januari, 2013 na unatarajiwa kukamilika miaka
miwili baada ya ujenzi kuanza. Kwa maneno mengine Kampasi ya Muhimbili
ya Mloganzila inategemewa kuanza kazi mwanzoni mwa mwaka 2015.
Tayari wataalamu na wafanyakazi
wanaotarajiwa kufanya kazi katika kampasi ya Mloganzila wameshaanza
mafunzo ndani na nje ya nchi. Mara hospitali hiyo kubwa na ya kisasa
itakapokamilika itakua na uwezo wa vitanda vya kulaza wagonjwa mia sita
(600).
Sambamba na kampasi ya MUHAS ya Mloganzila pia ujenzi wa Kampasi ya Afya ya Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) umeshaanza na kufikia hatua ya juu na ambapo pia hospitali hiyo inatarajiwa kuanza shughuli zake rasmi mwaka 2015.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Mfuko wa
Afya ya Jamii (National Health Insurance Fund) NHIF Bw. Emmanuel Humba
mchakato wa kufanikisha uanzishaji wa Chuo Hospitali hiyo vimeshaanza
ambapo baadhi ya wataalamu wakiwemo Madaktari na watumishi wengine wako
nchini na nje ya nchi kwa ajili ya masomo na mafunzo mbalimbali.
Chuo hicho kinatarajia kuwa na vifaa vya
kisasa vya tiba vinavyokidhi mahitaji ya Afya na Elimu ya Udaktari wa
kiwango cha Kimataifa, ikiwa ni mikakati
kabambe ya serikali ya awamu ya nne katika kuhakikisha nchi ina
wataalamu wengi na huduma za kisasa za afya ili kuondokana na adha ya
kupeleka wagonjwa nje ya nchi kwa ajili ya matibabu.
Kwa sasa MUHAS inachukua
takriban wanafunzi 2442 wa udaktari na huduma za afya kwa mwaka. Hivyo
ujio wa kampasi ya Afya Mloganzila na Kampasi ya afya ya UDOM
utaharakisha mpango wa serikali wa kupunguza wastani wa wagonjwa kwa
daktari mmoja kwa kiwango kikubwa. Hivi sasa wastani ni daktari mmoja anahudumia wagonjwa 30,000.
No comments:
Post a Comment