Mshambuliaji
wa timu ya Kilimajaro Stars, Simon Msuva akimfungisha tela beki wa timu
ya taifa ya Sudan, Faris Abdallah wakati wa mechi yao ya Kundi B la
michuano ya Kombe la Chalenji kwenye Uwanja wa Namboole mjini Kampala
jana jioni.
……………………………………………………………
JOHN Bocco ‘Adebayor’ alifunga
mara mbili na kusaidia kuipa Kilimanjaro Stars mwanzo mzuri wa michuano
ya Kombe la Chalenji wakati timu hiyo ya Tanzania Bara ilipochapa Sudan
kwa magoli 2-0 katika mechi ya Kundi B kwenye Uwanja wa Namboole nchini
Uganda jana jioni.
Nyota huyo wa klabu ya Azam,
aliyeibuka mfungaji Bora wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara msimu uliopita,
aliifungia Kili Stars goli la kuongoza
katika dakika ya 14 kufuatia
ushirikiano mzuri baina ya Mwinyi Kazimoto na Mrisho Ngassa aliyemsetia
Bocco kufunga katika goli tupu baada ya kipa Abd Elrahman Ali kutoka
kwenda kujaribu kumzuia Ngassa.
Bocco alifunga goli la pili katika
dakika ya 28 kufuatia kazi nzuri tena ya Ngassa aliyekimbia na mpira
kwa kasi na kupiga shuti ambalo lilikuwa likielekea wavuni lakini ili
kuwa na uhakika, Bocco aliliongeza nguvu baada ya kumpa mwili beki
aliyekuwa akikimbilia kwenda kujaribu kuokoa.
Kwa ushindi huo, Kili Stars
ilianzia katika nafasi ya pili ya msimamo kutokana na pointi 3, sawa na
vinara Burundi ambao walifungua mechi za kundi hilo kwa kuisambaratisha
Somali kwa magoli 5-1. Magoli katika mechi hiyo yalifungwa na Chriss
Nduwarugara na Selemani Ndikumana wa Burundi waliofunga mawili kila
mmoja na moja la Yusuph Ndikumana. La Somalia lilifungwa na Mohammed
Jabril kwa ‘tuta’ lililopigwa chini katikati ya lango likimuacha kipa
akihama mahala hapo.
Kilimanjaro Stars itacheza mechi
yake ijayo Jumatano wakati itakapowakabili vinara Burundi saa 12:00
jioni katika mtihani mwingine mkubwa kwa kocha Mdenmark Kim Paulsen wa
Kilimanjaro Stars. Mechi hiyo Jumatano itatanguliwa na mechi nyingine ya
Kundi B baina ya timu ambazo hazina pointi, Somalia na Sudan saa 9:00
alasiri.
Wawakilishi wengine wa Tanzania,
timu ya Zanzibar Heroes ya Zanzibar itacheza mechi ya ufunguzi wa Kundi C
kesho dhidi ya Eritrea saa 10:00 jioni wakati Rwanda watawavaa Malawi
saa 12:00 jioni.
Vikosi jana vilikuwa; Kilimanjaro
Stars: Juma Kaseja, Erasto Nyoni, Amir Maftah, Shomary Kapombe, Kelvin
Yondani, Salum Aboubakar, Mwinyi Kazimoto, Frank Domayo, Mrisho Ngassa,
Simon Msuva na John Bocco ‘Adebayor’.
Sudan: Abd Elrahman Ali, Moawia el
Amin, Sami Abdallah, Faris Abdallah, Hamoda Bashir, Mohammed el
Murtada, Sadam Abutalib, Mohammed Idris, Modathir Mohammed, Adam Sayer
na Mohammed Osman.
No comments:
Post a Comment