WAZIRI wa Uchukuzi, Dk Harrison Mwakyembe amewapiga marufuku
wafanyakazi wote walio chini ya wizara yake kusafiri kwa ndege katika
daraja la kwanza, akieleza kuwa huo ni ubadhirifu wa fedha za
umma.Akizungumza na waandishi wa habari mkoani Tanga jana, Mwakyembe
alisema atakayekaidi agizo hilo, atakatwa fedha katika mshahara wake.
Mwakyembe ambaye tangu ateuliwe kuwa Waziri wa Uchukuzi amekuwa akifanya uamuzi magumu, alisema hawezi kuvumilia
mtu yeyote ambaye atatumia hovyo fedha za walipa kodi, huku akiwataka
wafanyakazi wa wizara yake kufanya kazi kwa maadili na kuwatumikia
wananchi.
“Kulingana na hali halisi ya maisha ya baadhi ya ya Watanzania, wizara
yangu haitakuwa tayari kuona fedha zikitafunwa na watu wachache kwa
njia za kifisadi. Matumizi yafanyike kulingana na hali halisi ya
Watanzania,” alisema Mwakyembe na kuongeza;
“Kuanzia leo nawapiga marufuku watendaji wote wa wizara yangu kusafiri na ndege kwa kutumia daraja la kwanza.”
Akizungumzia hali za Mamlaka za Bandari Tanzania (TPA), Dk Mwakyembe
alisema, Wizara yake imeunda bodi ya watu wanane ambao wataanza kazi
Januari mwakani. Alisema kikosi kazi hicho, kitaleta mapinduzi ya
utendaji wa kazi katika mamlaka hiyo.
Alisema bodi hiyo itatambulishwa mara baada ya kukamilika kwa baadhi ya mambo muhimu na hivyo kuwataka wananchi kuwa wavumilivu.
Alisema kwa sasa bodi hiyo imeanza mikakati ya kuhakikisha Tanzania
inaingia kwa nguvu zote katika soko la ushindani la Jumuiya ya Afrika
Mashariki (EAC).
Alisema Wizara yake inakusudia kuleta mageuzi katika sekta ya
usafirishaji katika bandari zake (PTA) ili kuweza kuleta ushindani wa
kibiashara na nchi jirani na kuweza kuwavutia wafanyabiashara
watakaoweza kushusha shehena zao katika bandari zake.
‘Baada ya kuunda bodi mpya ya watu wanane ya (PTA), tumedhamiria kwa
dhati kuondoa madudu ambayo yalikuwa yanatusumbua katika bandari zetu
na kuonekana kama tumeshindwa,” alisema Dk Mwakyembe.
Akizungumzia kuhusu Bandari Mpya ya Mwambani ambayo ujenzi wake bado
haujaanza, Waziri Mwakyembe, alisema wale ambao wana ubeza mradi huo
mwisho wake wataumbuka kwani ndani ya miezi sita ijayo utaanza.
Alisema mradi huo wa kujenga bandari mpya utaanza ndani ya miezi sita
ijayo, hivyo wale ambao wamekuwa wakiubeza na kuleta upinzani
watambue kuwa mradi huo upo na utaendelea kuwepo na Serikali
itahakiksha inatekeleza azma yake.
“ Hao wapinzani wanaoubeza mradi huu wajue kuwa mwisho wake wataumbuka
kwani mradi upo na ndani ya miezi sita tutaanza kwani kila kitu kiko
tayari na bado utekelezaji wake tu” alisema Dk Mwakyembe.
Kuhusu bandari ya nchi kavu Mwakyembe alisema itajengwa Wilayani
Korogwe sambamba na mradi wa reli ambao utakuwa mkombozi kwa watu
Korogwe na maeneo ya jirani husasuani kwa wafanyabiashara.
Alisema bandari hiyo ambayo itajengwa sambamba na mradi wa reli utaweza
kuwanufaisha wananchi wa Tanga na mikoa jirani kwani mbali ya ajira
pia wataweza kujitafutia masoko katika nchi jirani.
No comments:
Post a Comment