Naibu
Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Lazaro Nyalandu (wapili kutoka
kulia) akimsikiliza kwa makini Kaimu Mkurugenzi wa Mafunzo, Naiman Mbise
alipokuwa akimuelezea matumizi ya majiko ya kisasa yatakayotumika
kufanyia mafunzo kwa vitendo kwa wanafunzi Chuo cha Taifa cha Utalii
kilichopo mtaa wa Garden Avenue na Shaaban Robert mkabara na Chuo cha
IFM na Makumbusho ya Taifa na nyumba ya Utamaduni alipotembelea chuo
hicho hivi karibuni.
……………………………………………………….
Na Tulizo Kilaga
Naibu Waziri wa Maliasili na
Utalii, Mhe. Lazaro Nyalandu ameutaka uongozi wa Chuo cha Taifa cha
Utalii (NCT) kuhakikisha chuo hicho kinatoa elimu yenye ubora wa
kimataifa.
Aliyasema hayo Dar es
Salaam hivi karibuni alipotembelea jengo jipya la Chuo cha Taifa cha
Utalii lililopo mtaa wa Garden Avenue na Shaaban Robert mkabara na Chuo
cha IFM na Makumbusho ya Taifa na nyumba ya Utamaduni kwa mara ya kwanza kuona shughuli zinazofanywa na chuo hicho.
Mhe. Nyalando alisema chuo hicho
ambacho kina vifaa vya kisasa, kitakuwa na mafanikio zaidi na
kutambulika duniani kote na kuijengea heshima Tanzania iwapo mitaala
yake itazingatia zaidi viwango vya kimataifa.
“Tanzania tunatatizo lakutokuwa
na watu waliobobea katika tasnia ya utalii, kwa chuo hichi cha kisasa
hatuna budi kupanua wigo kwa kuhakikisha mafunzo mengine yanaongezwa
bila kusahau masuala ya lugha za kigeni kwa kuzingatia ubora na viwango
vinavyotambulika kimataifa na hivyo kuvutia wanafunzi kutoka ndani na
nje ya nchi na hata wadau wa sekta ya utalii nchini kuwapa ajira
wahitimu,” alisema Mhe. Nyalando ambaye pia ni mdau wa sekta ya utalii.
Alisema lengo la Serikali na
Wizara ni kuhakikisha chuo hicho kinakuwa miongoni mwa vyuo bora Barani
Afrika chenye kuzalisha wahitimu wanaotambulika kimataifa. Hivyo kuwa na
sifa yakufanya kazi hata akitoka nje ya mipaka ya nchi.
Waziri Nyalandu alisema Wizara
itahakikisha wakufunzi wa chuo hicho wanapewa nafasi za kwenda kusoma
kwenye vyuo vya nje ili kuongeza ujuzi, kutoa kipaumbele katika mgao wa
fedha ili kukipa uwezo wa kutanua wigo wa mafunzo yake na kukipa uhuru
binafsi wa kiutawala ili suala la ajira liishie kwenye bodi.
Naye Kaimu Mtendaji Mkuu wa Chuo
hicho, Rosada Msoma, alisema chuo hicho kinatoa kozi za miaka miwili kwa
ngazi ya Astashahada na Stashahada na tayari kimeanza na wanafunzi 171
ambao wanajifunza masuala ya Uzalishaji Chakula, Uokaji, Uandaaji wa
Chakula na Vinyaji, Uandaaji wa Vyumba, Mapokezi, Ugawaji Vyumba na
Sanaa ya Mapishi.
Alisema chuo hicho kimejipanga
kuhakikisha wahitimu wake wanakuwa bora katika soko la ajira kwa kuweka
msisitizo kwenye elimu ya nadhalia na vitendo, na tayari chuo
kimeanzisha maeneo ya kitalii yaliopo katika jiji la Dar es Salam kwa
ajili ya Safari za jiji zitakazoongozwa na wanafunzi wanaosoma masomo ya
Uongozaji Watalii.
No comments:
Post a Comment