Friday, December 7, 2012

MWANASHERIA ASHIKILIWA MKOANI ARUSHA

Mahmoud Ahmad,Arusha
 …………………………..
JESHI la polisi mkoani Arusha linamshikilia na kumhoji  mwanasheria maarufu jijini hapa,Deogratias Urasa kwa tuhuma za kufyatua risasi hovyo katika ugomvi baina yake na mfanyabiashara maarufu,James Ndika anayeishi  jijini Dar es salaam.
 
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana na kamanda mkuu wa jeshi la polisi mkoani Arusha,Liberatus Sabas alisema kwamba tukio hilo lilitokea mwishoni mwa wiki iliyopita katika mgahawa maarufu wa ViaVia uliopo mkabala na ofisi ya mkuu wa mkoa wa Arusha.
 
Mgahawa wa Viavia umejijengea umaarufu kwa kutembelewa na raia wa wageni kutoka nchi za Ulaya,Marekani na Asia ambapo katika siku za hivi karibuni umekumbwa na matukio ya watu kupigana hovyo.
 
Kamanda,Sabas alisema kwamba pamoja na mwanasheria huyo anayefanya kazi kutoka kampuni ya Maro Advocates ya jijini Arusha kufyatua risasi tatu hovyo hewani lakini katika tukio hilo hakuna mtu yoyote aliyejeruhiwa.
 
Alitaja chanzo cha ugomvi katika tukio hilo ni baada ya kutokea majibishano makali baina ya mwanasheria  huyo na Ndika yaliyosababishwa  na masuala ya kibiashara miongoni mwao.
 
“Hawa watu wana mambo yao ya  kibiashara sasa siku ya tukio walijibishana ndipo huyu mwanasheria akachukua silaha yake na kufyatua risasi hewani hovyo hali iliyopelekea kuleta taharuki”alisema Sabas
 
Alisema kwamba mara baada ya majibishano hayo mwansheria huyo alikosa uvumilivu na kufyatua risasi hewani  hali iliyopelekea taharuki  ndani ya mgahawa huo na kupelekea watu kukimbia hovyo huku wengine wakilala chini kuhofia usalama wa maisha yao.
 
Kamanda,Sabas aliliambia gazeti hili kwamba baada ya jeshi lake kupokea taarifa lilimshikilia mwanasheria huyo katika kituo kikuu cha polisi cha kati na kisha kumwachia huru ambapo kwa sasa yuko nje kwa dhamana.

Alienda mbali na kusisitiza ya kwamba mbali na kushikiliwa jeshi lake lilimhoji mwanasheria huyo juzi atika makao makuu ya jeshi hilo mkoani hapa na pindi uchunguzi utakapokamilika atafikishwa mahakamani kujibu makosa yanayomkabili.
 
Alisisitiza kwamba mbali na kushikiliwa kwa mwanasheria huyo pia jeshi lake linawasaka watuhumiwa wawili(majina yao yamehifadhiwa) wanaotajwa kuhusika kwa ukaribu katika tukio hilo .

No comments:

Post a Comment