Na Anna Nkinda – Maelezo
Mke wa Rais Mama Salma Kikwete
ametunukiwa tuzo na Taasisi ya Kimataifa ya Gavi Alliance kutokana na
mchango wake mkubwa kwa jamii wa kuhakikisha kuwa vifo vya kina mama
wajawazito na watoto vinavyotokana na tatizo la uzazi vinapungua hapa
nchini.
Tuzo hiyo ilitolewa jana usiku
katika Hoteli ya Serena na Mwenyekiti wa bodi ya Taasisi hiyo Dagfinn
Hoybraten wakati wa hafla ya utoaji tuzo ilienda sambamba na mkutano wa
kimataifa wa siku tatu wa Gavi Alliance unaoendelea jijini Dar es
Salaam.
Akiongea kabla ya kukabidhiwa tuzo
hiyo Mwanamuzi maarufu wa Afrika ya Kusini Yvonne Chakachaka ambaye
pia ni Balozi wa heshima wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kushughulikia
watoto Duniani (UNICEF) na mshereheshaji wa shughuli hiyo alisema kuwa
hivi sasa wake wa marais wamekuwa wakijitoa kuisaidia jamii hasa katika
mambo yahusuyo afya ya mama wajawazito na mtoto.
Mke wa rais wa Zambia Dk. Christine Kaseba Sata naye alipewa tuzo kama aliyopewa Mama Kikwete.
Aidha Wizara za Afya na Ustawi wa
Jamii pamoja na Fedha zilipewa tuzo kwa ajili ya kuandaa mkutano huo wa
kimataifa wa Umoja wa wadau wa chanjo na Kinga Duniani uliohudhuriwa na
wataalamu wa afya, mawaziri wa afya na wake wa marais kutoka barani
Afrika.
Mama Kikwete kupitia Taasisi yake
ya WAMA amekuwa akitoa vifaa tiba katika Zahanati, vituo vya afya na
Hospitali hapa nchini, kutoa elimu kwa jamii na wataalamu wa afya juu
ya uzazi salama na afya ya mtoto , wanafanya program ya kupunguza
maambukizi ya Virusi Vya Ukimwi (VVU) kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto
ambayo inasaidia mtoto kuzaliwa salama ingawa wazazi wake wanakuwa na
maambikizi.
Pia wamekuwa wakiwawezesha
wanawake kiuchumi katika miradi mbalimbali jambo ambalo limewafanya
waweze kupata kipato cha ziada na hivyo kupunguza makali ya maisha na
kuweza kuwatunza watoto wao kwani wanawake wengi wenye kipato cha
kutosha wanaweza kuwatunza vizuri watoto wao na kupunguza vifo
vinavyoepukika.
No comments:
Post a Comment