Rais
wa Madagascar, Mheshimiwa Andry Rajoelina amewasili mjini Dar Es Salaam
mchana wa leo, Ijumaa, Desemba 14 kwa ziara ya kikazi ya siku mbili
nchini.
Kwenye Uwanja wa Ndege wa
Julius Nyerere mjini Dar Es Salaam ambako ndege iliyomleta Rais
Rajoelina ilitua saa sita na dakika 45 mchana, amelakiwa na mwenyeji
wake, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete.
Rais Kikwete na Rais Rajoelina wamekula chakula cha mchana na wanatarajiwa kuanza mazungumzo rasmi baadaye leo.
Rais Kikwete ambaye ni Mwenyekiti
wa Tume ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya Jumuia ya Maendeleo Kusini mwa
Afrika (SADC) amepewa jukumu na viongozi wenzake ndani ya Jumuia hiyo
kukutana na viongozi wa Madagascar kuwalezea maamuzi ya mkutano wa
viongozi hao wa SADC uliofanyika mwishoni mwa wiki mjini Dar Es Salaam.
Rais Kikwete tayari amekutana na
kufanya mazungumzo na Mheshimiwa Marc Ravalomanana, kiongozi wa zamani
wa Madagascar aliyeondolewa madarakani na Rajoelina.
Kwenye mkutano na waandishi wa
habari uliofanyika Ikulu, Dar Es Salaam, mwanzoni mwa wiki hii,
Mheshimiwa Ravalomanana alithibitisha kuwa amekubaliana na maamuzi ya
viongozi wa SADC.
Miongoni mwa mambo mengine,
viongozi hao wa SADC wanataka viongozi hao wawili wa Madagascar
washawishiwe na wakubali kutogombea katika Uchaguzi Mkuu uliopangwa
kufanyika nchini humo mwakani.
No comments:
Post a Comment