NA GLADNESS MUSHI FULLSHANGWE-ARUSHA
SEMINA na kikao cha wahariri na
waandishi wa habari waandamizi wa michezo na burudani nchini,
vinatarajiwa kufanyika April 12 na 13 mwaka huu, katika jiji la
Arusha.
Semina hiyo, pia itakwenda
sambamba na kumbukumbu ya kifo cha aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Moringe
Sokoine ambapo wanahabari hao watatembelea familia na Kaburi la
Sokoine wilayani Monduli ili kutoa pole.
Maamuzi ya kufanyika semina hiyo
na kikao cha wahariri jijini hapa, yalifikiwa juzi katika kikao baina ya
Mwenyekiti wa chama cha waandishi wa habari zamichezo nchini(TASWA),
Juma Pinto na viongozi wa TASWA Arusha katika hoteli ya palace mjini
hapa.
Akizungumza katika kikao hicho,
Pinto alisema TASWA inatarajia kuitisha kikao hicho, Arusha ikiwa ni
sehemu ya mipango yake,kukifanya chama hicho kuwa cha kitaifa zaidi na
pia kuongeza uelewa wa masuala ya michezo kwa wanahabari.
Pinto alisema ili kufanikisha
semina hiyo, TASWA taifa na Taswa Arusha, wanapaswa kushirikiana katika
maandalizi ya kutafuta wadhamini, ambapo pia watashirikishwa wanahabari
toka mikoa ya Kilimanjaro, Tanga na Manyara.
Wakizungumza katika kikao hicho,
Katibu wa TASWA Arusha, Mussa Juma na Katibu msaidizi Hamza Kalmera
walieleza TASWA Arusha kuwa tayari kuandaa semina hiyo, ambayo
itafanyika siku ya kumbukumbu ya aliyekuwa Waziri mkuu, Edward Moringe
Sokoine pia kutafanyika tamasha maalum la michezo mbali mbali.
No comments:
Post a Comment