Mkuu wa Mkoa wa Mbeya,Abbas Kandoro.
MWANAFUNZI
wa darasa la sita Shule ya Msingi Kasumulu, Kata ya Ngana, wilayani
Kyela, Kaselema Mpale (14) ameuawa kikatili kwa kuchinjwa na kitu
chenye ncha kali, kisha kunyofolewa baadhi ya viungo vyake sehemu ya
mwili.
Mama
mzazi wa mwanafunzi huyo, Lucia Kamnyonge alisema tukio hilo
lilitokea Februari 8, mwaka huu saa 1:30 usiku, alipotumwa na baba
yake kwenda nyumba ya jirani kuchukua mpunga ambao ungetumika kwa
chakula usiku.
Kamnyonge
alisema mtoto wake hakupatikanika hadi alipokutwa siku ya pili yake,
akiwa amechinjwa na kunyofolewa baadhi ya sehemu zake za mwili ambazo ni
pua, mdomo, jicho, kuondolewa sehemu zake za siri na kuchunwa ngozi ya
kichwa karibu na utosi na mwili wake kutundikwa juu ya mti.
Aliendelea
kuwa baada ya hali hiyo taarifa ilipelekwa ofisi ya serikali ya kijiji,
uliitishwa mkutano wa wananchi wote na walitawanyika kuanza kumtafuta
mtoto huyo bila ya mafanikio.
Baadaye, baba yake alimkuta juu ya mti akiwa ametundikwa kichwa chini miguu juu na viungo vyake hivyo vikiwa vimenyofolewa.
Mwenyekiti
wa Kitongoji cha Ibungumbati lilipotokea tukio hilo, Adam Mkese alidai
tukio hilo limewashtua na kwamba, mkutano wa kijiji ulioitishwa kwa
dharura wananchi walimhusisha baba mzazi wa mtoto huyo na mauaji hayo.
Mkese
alidai watu wa kijiji hicho walimhusisha kutokana na mazingira tata ya
kifo chenyewe na maelezo ya kujichanganya aliyoyatoa.
Ofisa
mtendaji wa kijiji hicho, Naomi Charles alidai kuna dalili za mzazi
huyo kuhusishwa na mauaji hayo na kwamba, polisi wanaendelea na
uchunguzi zaidi.
Mwenyekiti
wa kijiji hicho, Baruti Mwakasala alidai kuwa hali katika kijiji hicho
siyo nzuri na kushukuru polisi kwa hatua za haraka walizochukua.
Kamanda
wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Diwani Athuman alithibitisha kutokea kwa
mauaji hayo na kukiri kumshikilia baba mzazi wa mtoto huyo kwa uchunguzi
zaidi.
No comments:
Post a Comment