Shirikisho
la Kimataifa la Vyama vya Mpira wa Miguu (FIFA) limesema litaifungia
Tanzania iwapo itabainika kuwa Serikali imekuwa ikiingilia shughuli za
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF).
FIFA
imesema kumekuwa na shutuma kupitia taarifa mbalimbali za vyombo vya
habari nchini kuwa Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo
imeonesha nia ya kuingilia uendeshaji wa TFF.
Kwa mujibu wa
barua ya jana (Machi 10 mwaka huu) ya FIFA kwenda kwa Rais wa TFF,
Leodegar Tenga, vyombo vya habari vimemkariri Waziri (Dk. Fenella
Mukangara) kuwa Serikali imeiagiza TFF kutumia Katiba ya mwaka 2006
katika uchaguzi wakati tayari imeshafanyiwa marekebisho.
“Pia imeelezwa
kuwa TFF imetakiwa kufanya Mkutano Mkuu pamoja na ule wa uchaguzi kwa
tarehe ambazo zimepangwa na Serikali. Vilevile imeelezwa kuwa Serikali
inakusudia kuunda Kamati ya Muda iwapo TFF haitatekeleza maagizo yake,”
imesema sehemu ya barua hiyo iliyosainiwa na Katibu Mkuu wa FIFA, Jerome
Valke.
FIFA imesema
iwapo yaliyoripotiwa na vyombo vya habari yatathibitika kuwa kweli,
maana yake huo ni uingiliaji wa wazi wa Serikali kwa shughuli za TFF.
“Tunapenda
kuwakumbusha kuwa wanachama wote wa FIFA wanatakiwa kuendesha shughuli
zao kwa uhuru bila kuingiliwa na mtu mwingine kama ilivyoelezwa katika
ibara za 13 na 17 za Katiba ya FIFA.
“Hivyo kama
maagizo hayo yanayodaiwa kutolewa na Serikali yatatekelezwa, suala hili
litapelekwa katika mamlaka za juu za FIFA kwa hatua zaidi ikiwemo
kuisimamisha Tanzania kama ambavyo inakuwa pale panapokuwa na uingiliaji
wa Serikali,” imesema barua hiyo.
Barua hiyo
ambayo nakala yake pia imetumwa Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika
(CAF) imeelezea baadhi ya athari ambazo Tanzania itakumbana nazo endapo
itasimamishwa ni timu za taifa pamoja na klabu kutoshiriki mechi za
kimataifa kwa mujibu wa Ibara ya 14 ya Katiba ya FIFA.
Vilevile si
TFF au wanachama wake na maofisa wengine watakaoweza kunufaika na
programu za maendeleo, kozi au mafunzo yanayotolewa na FIFA na CAF.
“Madai ya
uamuzi uliofanywa na Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo ni
ya kusikitisha kutokana na ukweli kuwa FIFA ilishatangaza itatuma ujumbe
wake kuchunguza jinsi hali ilivyo kwa sasa na kutoa mapendekezo yake.
Kutokana na hali hii, ujumbe wa FIFA uliokuwa uje kuchunguza (suala la
uchaguzi) itabidi usubiri kwa vile ni muhimu kushughulikia tatizo hili
kwanza.
“Katika
mazingira haya tunaomba ueleze msimamo huu wa FIFA kwa mamlaka
zinazohusika (Serikali) na athari ambazo mpira wa miguu wa Tanzania
utakumbana nazo. Tunakushuru na tunatarajia utatufahamisha kila hatua
inayoendelea katika suala hili,” imesema barua hiyo.
Boniface Wambura
Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)
No comments:
Post a Comment