Yaomba hatua zinazochukuliwa ziwe endelevu kukomesha majanga ya kizembe
Na Mwandishi Wetu
UMOJA
wa Wanawake wa Tanzania (UWT) umelezea kusikitishwa kwake na matukio
ya watu kupoteza maisha na kujeruhiwa yaliyotokea mapema wiki hii,
likiwemo la kuporomoka jengo la ghorofa 16, jijini Dar es Salaam, na
kusababisha vifo vya watu 36 na kujeruhiwa wengine kadhaa.
Tukio lingine
lingine ni lililotokea juzi, Aprili mosi, ambako watu zaidi ya watu 20
wameelezwa kupoteza maisha baada ya kuangukiwa na kifusi katika machimbo
ya Moramu, eneo la Chekereni mkoani Arusha.
Katika taarifa
iliyotolewa na Makao Makuu ya UWT jijini Dar es Salaam, leo, Aprili 3,
2013, Katibu Mkuu wa Jumuia hiyo, Amina Makilagi amesema, UWT pia
inalaani matukio ya kuchinjwa kwa wanawake yanayoendelea kutokea Wilaya
ya Butiama Mkoa wa Mara ambapo taarifa zilizopo Mwanamke mmoja
amechinjwa kinyama kwa kutenganishwa kichwa na kiwiliwili chake na watu
wasiojulikana.
" UWT
imesikitishwa na vitendo vya kinyama vinavyofanywa na baadhi ya watu
wasio na moyo wa kibinadamu kwa kuwakata vichwa wanawake na kuondoka
navyo kwa malengo yao binafsi hivyo kusababisha wanawake kuishi katika
maisha ya wasiwasi katika nchi yao", alisema Amina katika taarifa hiyo.
Alisema, UWT
inaungana na Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Rais Jakaya Kikwete kwa kutoa maelekezo mazito
kwa mamlaka husika kuchukua hatua kali kwa wahusika wa matukio yote.
Hata hivyo UWT
imeomba hatua zinazochukuliwa na serikali dhidi ya majanga hayo,
ikiwemo kuporomoka kwa ghorofa, watu kuangukiwa na kifusi kwenye
machimbo na watu kukatwa vichwa, ziwe hatua endelevu kuhakikisha matukio
hayo hayatokei tena kirahisi.
"UWT pamoja na
kutambua hatua za awali zilizochukuliwa hadi sasa katika matukio hayo,
inaiomba Serikali kuhakikisha hatua inazochukua sasa ziwe ni endelevu
ili kuhakikisha matukio kama haya ambayo kwa sehemu kubwa yanatokana na
uzembe hayatokei tena", alisema Makilagi katika taarifa hiyo na
kuongeza;-
"UWT inaungana
na Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Rais wa Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania, Rais Kikwete kwa kutoa maelekezo mazito kwa mamlaka husika
kuchukua hatua kali kwa wahusika wa matukio yote".
Amina
aliwaombea ndugu jamaa na marafiki wa marehemu kuwa wavumilivu katika
kipindi hiki kigumu cha maombolezo ya wapendwa wao ambao wameacha pengo
katika familia zao na Taifa kwa ujumla na kuwaombea wapone haraka
waliojeruhiwa.
No comments:
Post a Comment