Monday, November 19, 2012

WAKUU WA MIKOA NA WILAYA KUJIUNGA NHIF

Na Mwandishi Wetu, Dodoma
SERIKALI imeshauriwa kubadili utaratibu wa matibabu kwa Maofisa Waandamizi ili kuwawezesha kunufaika na huduma za matibabu kupitia Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya.
Ushauri huo umetolewa na Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya mjini Dodoma katika kikao kazi cha siku tatu ambacho kiliongozwa na Waziri Mkuu Mizengo Pinda.
Wamesema kuwa utaratibu wa sasa ambao unaonesha kuwa matibabu ni moja ya stahiki zao unawazuia Wakuu hao kunufaika na huduma za matibabu kupitia NHIF ambazo walisema zimeboreshwa sana kwa sasa na zina mtandao mkubwa unaowezesha kupata huduma mahali popote nchini.
Akichangia mada iliyowasilishwa na NHIF kwa wakuu hao, Mkuu wa Wilaya ya Kalambo, Moshi Chang’a alisema kuwa “Tunataka kuwa wanachama wa NHIF hata sasa ila kinachotubana ni hizo stahiki ambazo tumepewa ikiwemo ya matibabu kulipiwa na Serikali, ipo haja sasa ya Serikali kupeleka fedha NHIF ili sisi tutibiwe na Mfuko,” alisema Chang’a.
Alisema kuwa ni vyema wakajiunga na NHIF ambayo itawasaidia kunufaika na fao la wastaafu  lakini pia itawapa hamasa kubwa katika uhamaishaji kutokana na ukweli kwamba watakuwa miongoni mwa watumiaji wa huduma hizo.
Akijibu hoja hiyo, Waziri Mkuu Mizengo Pinda alisema kuwa kwa sasa wakuu hao wanaweza wakajiunga wakati Serikali ikiliangalia suala hilo ili liwe kwenye utaratibu wanaoutaka.
Akitoa maelezo ya awali kwa viongozi hao, Mkurugenzi Mkuu wa NHIF, Emanuel Humba alisema kuwa ili Mfuko ufanikiwe kuwafikia Watanzania wengi kama nchi zingine zilizofanikiwa katika suala hilo ni lazima viongozi wakawa wanachama au wanufaika wa huduma za Mfuko.
“Nchi zilizofanikiwa kuwaingiza wananchi wake kwenye utaraibu wa Bima ya Afya kama Ufilipino, Korea, Rwanda viongozi wake Wakuu ni wanachama wa Mifuko hiyo… hivyo nanyi wakuu wetu mkijiunga itakuwa ni kazi rahisi kufikia malengo yetu,” alisema Humba.
Aidha aliwaomba wakuu hao kuhakikisha wanafuatilia fedha zinazolipwa na NHIF katika Vituo vya Kutolea huduma kwenye maeneo yao ili zisaidie kuboresha huduma za matibabu ikiwemo ununuzi wa dawa na Vifaa tiba.
Katika suala hilo la Malipo, Waziri Mkuu aliutaka Mfuko kuweka utaratibu wa kuwapa taarifa za fedha viongozi wakiwemo Wakuu wa Mikoa, Wilaya, wabunge ili waweze kuzifuatilia katika matumizi yake.a

No comments:

Post a Comment