Monday, December 31, 2012

WATOTO YATIMA WA KURASINI WAFAIDIKA NA MSAADA WA MKURUGENZI WA RAHAB CLINICK



OFISA mfawidhi kituo cha kulelea watoto yatima Kurasini, Ramadhani Yahaya ameiomba serikali kufanya jitihada za kuwaondoa vijana wanaoendelea kuishi katika kituo hicho, licha ya kupoteza sifa ya kuishi katika kituo hicho kwa kuwa wamevuka miaka 18.
 
Ofisa huyo aliyaeleza hayo jijini Dar es Salaam jana, wakati Mkurugenzi wa Rahabu Ulcers Clinic, Dk Rahabu Rubago alipokuwa akitoa zawadi mbalimbali kwa ajili ya kusherehekea mwaka mpya ikiwemo chakula, vinywaji na vifaa vya shule kwa watoto wa kituo hicho waliokuwa wamechanganyika na watoto wa kituo cha wasabato.
 
Ramadhani alisema kituo hicho kwa sasa kinakumbwa na changamoto kubwa ya kuwa na vijana wengi wenye umri zaidi ya miaka 18 hivyo wanashindwa kufuata masharti ya kituo hicho ikiwemo kuwa ndani ya uzio ifikapo saa 12 jioni.
 
“Changamoto kubwa ni vijana wenye umri mkubwa kuendelea kuishi katika kituo hiki naiomba serikali iwatengenezee vijana hawa mazingira ya kuwaondoa katika maeneo haya ili nao wakawe na maisha yao na kuachana na utegemezi wa hapa” alisema Ramadhani
 
Naye Dk Rahabu aliwataka vijana na watoto hao kutokukata tamaa katika maisha yao huku akiwataka kusoma kwa bidii ili waweze kukamilisha ndoto zao na  malengo waliyojiwekea.
 
“Mimi niliishi hapa nimekuja kufurahi nanyi na kuwatia moyo msijione kama mpo peke yenu tupo pamoja na kutokana na kujibidiisha tumefanikiwa hivyo nanyi nawahasa mjibidiishe kwa bidii zote ili muweze kufanikiwa na kufikia malengo yenu,” alisema Dk Rahabu”alisema Rahabu
 
Naye mwanafunzi anayesoma chuo cha uhasibu, ambaye anaishi katika kituo hicho, Robert Bernard ameiomba serikali kutowaondoa vijana waliozidi miaka 18 bila kuwatengenezea mazingira mazuri ya kwenda kuishi.
 
“Kuondoka hapa si tatizo tunachoomba kama serikali inataka kutuondoa hapa kwa kuwa umri wetu mkubwa hatukaidi bali tunachoomba watuwekee mazingira mazuri huko wanakotaka twende lakini bila hivyo watakuwa hawajatusaidia” alisema Bernard.

No comments:

Post a Comment