Monday, January 7, 2013

HAYA NDIYO YALIYOPENDEKEZWA NA VYAMA VYA SIASA YAWEPO KWENYE KATIBA MPYA

Baadhi ya wanasiasa wakichangia maoni ya katiba mpya jana jijini Dar es Salaam.

 Vyama vya siasa jana vilianza kutoa maoni mbele ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba, huku Chadema ikipendekeza umri wa kugombea urais uwe miaka 18.

Wawakilishi wa vyama hivyo vya siasa ambavyo ni pamoja na CCM, CUF, UDP na TLP walitoa maoni yao bila waandishi wa habari kuhudhuria katika kile kilichoelezwa ni kutaka watoa maoni wawe katika uhalisia wao.


Mikutano hiyo ya jana iliendeshwa kwa siri kati ya wajumbe wa Tume na wa vyama hivyo hali ambayo ilifanya wanahabari kusubiri nje huruma ya vyama ambavyo vilikuwa tayari kueleza walichopendekeza ndani.


CCM
ambayo ujumbe wake uliongozwa na Mwanasheria mkongwe Andrew Chenge hawakuwa tayari kueleza kilichomo ndani ya waraka wa chama hicho badala yake Mwenyekiti wa ujumbe huo alijibu swali moja la waandishi wa habari juu ya mgombea binafsi.

Na hata hivyo kuhusu mgombea binafsi Chenge hakutaka kuzungumzia mapendekezo yao kwa kina ila   alisema chama chake kinaliunga mkono kwa hadhari.


Alisema kama wananchi watapendelea mgombea binafsi awepo, basi awekewe mipaka kama ilivyo kwa wagombea wa vyama vya siasa ambao wanabanwa na katiba za vyama vyao ili watende kwa maslahi ya chama na wananchi.


“Na huyu mgombea binafsi kama ataruhusiwa, sisi tunataka awekewe mipaka ndani ya Katiba mpya, kwani kwenye vyama watu wanateuliwa baada ya mchakato mrefu,” alisema Chenge ambaye hata hivyo hakutaka kuzungumza kwa kina juu ya mapendekezo ya chama hicho.


Kwa muda mrefu Serikali inayoongozwa na CCM imekuwa inapinga kuwepo kwa mgombea binafsi kwa madai kuwa muda wa kufanya hivyo bado.

Serikali imebadilisha sheria ya uchaguzi mara kadhaa kuhakikisha suala la mgombea binafsi halipewi nafasi, licha ya ushauri wa Baba wa Taifa hayati Julius Nyerere ambaye alitamani kuwepo na mgombea huyo.

Katika kesi ambazo zilifunguliwa na Mchungaji Christopher Mtikila kupinga sheria ya uchaguzi, Serikali licha ya kubwagwa  mara kadhaa; lakini ilikata rufaa kwa jopo la majaji wa Mahakama ya Rufani ambao walitamka kuwa suala hilo ni la kisiasa na Mahakama haina mamlaka ya kutamka kama mgombea binafsi awepo ama la bali ikaamuru suala hilo lirudishwe bungeni kwani chombo hicho ndicho chenye mamlaka ya kutunga sheria.


Chenge alipoombwa waraka wa CCM wenye mapendekezo ya chama alijibu, “Haya ni mapendekezo ya chama siwezi kuwapa ila wanachama wetu wanafahamu tunachohitaji kiwemo kwenye Katiba mpya,” alisema Chenge baada ya kuombwa waraka wa chama hicho ambao wameuwasilisha kwenye Tume.


Ujumbe wa CCM licha ya Chenge, mjumbe mwingine alikuwa Kingunge Ngombale-Mwiru, Kidawa Salehe na Othman Machano.


CHADEMA
kwa upande wake imependekeza umri wa kugombea urais ushushwe hadi miaka 18 ili kutoa fursa ya mtu yeyote kuwa na haki ya kupiga kura na kupigiwa kura.

"Haiwezekani awe na haki ya kupiga kura lakini asiwe na busara ya kuwa Rais wa nchi hii, tunapendekeza mpiga kura awe na haki za kisheria za kugombea urais, ubunge na udiwani," alisema Tundu Lissu ambaye alikuwa Katibu wa ujumbe wa CHADEMA.


Ujumbe wa CHADEMA katika mkutano huo na Tume uliongozwa na Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe, Naibu  Katibu Mkuu Zitto Kabwe na Mkurugenzi wa Vijana, John Mnyika.


Chama hicho pia kilipendekeza mfumo wa elimu nchini utolewe kwa lugha ya Kiswahili kuanzia shule za msingi hadi vyuoni na Kiingereza liwe somo linalojitegemea. Pia walipendekeza Katiba itamke kuwa Kiswahili ni lugha ya Taifa ya Tanzania hivyo shughuli zote za kiserikali, bungeni na mahakamani itumike lugha hiyo.


“Wabunge wengi hawajui Kiingereza, lakini wanatunga sheria kwa Kiingereza. Mahakamani majaji hawajui Kiingereza lakini wanalazimishwa waandike Kiingereza, umefika wakati Katiba iseme Kiswahili kitumike katika vyombo hivi,” alisema Lissu.


Kwa upande wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, chama hicho kilipendekeza iwe na wajumbe 25 kati yao 15 watokane na vyama vyenye uwakilishi bungeni na wateuliwe kwa uwiano wa wabunge walioko bungeni.


Lakini wajumbe wengine 10 watokane na asasi za kiraia, vyama vya kitaaluma, jumuiya za kidini na vyama vingine vya siasa ambavyo havina uwakilishi bungeni.

"Tunapendekeza Mwenyekiti na Makamu wa Tume hiyo wachaguliwe na wajumbe wenyewe, ila wasitokane na wajumbe kutoka vyama vya siasa kuepuka kuingiza ushabiki kwenye utendaji wao," alisema Lissu.

Alisema wajumbe hao wakishapendekezwa na makundi hayo, majina hayo yapelekwe bungeni kwa ajili ya kuthibitishwa.


"Hapa hakuna sehemu ambayo Rais anateua wajumbe, hivyo Tume hii haitaogopa kutangaza matokeo ya Rais…sisi tunatamani kuwa na Tume huru badala ya hii ya sasa hivi ambayo ni mali ya Rais.”


Kuhusu Muungano, chama hicho kilipendekeza ili kuepusha kuvunjika kuwe na Serikali ya Tanganyika na Zanzibar zote ziongozwe na Rais, Bunge na Serikali yake na pia kuwe na Serikali ndogo ya Muungano itakayoshughulikia mambo saba tu.


Baadhi ya mambo hayo ni Ulinzi na Usalama, Mambo ya Nje upande wa diplomasia. Pia Rais wa Muungano achaguliwe na mamlaka mbalimbali kama wabunge, mameya na magavana wa majimbo.


“Huyu anaongoza mambo machache, haina haja ya kuchaguliwa na wananchi wote, badala yake achaguliwe na viongozi wa mamlaka zitakazopendekezwa kwenye Katiba,” alisema.


Aliongeza kuwa kwa upande wa serikali za Tanganyika na Zanzibar kuwe na serikali yenye wizara zisizozidi 18.

Pia Bunge la Tanganyika liwe na mfumo wa mabunge mawili moja la wananchi ambalo litakuwa na wabunge 250 na lingine la majimbo ambalo litakuwa na wabunge 50.

Walipendekeza kila nchi iwe huru kujitoa kwenye muungano iwapo itaona haifadiki ila wananchi wa upande wa nchi husika inayotaka kujiondoa wapige kura ya maoni na uamuzi huo ufikiwe baada ya kupatikana kwa theluthi mbili ya wapiga kura wote.


Mfumo wa Serikali uwe wa majimbo ili kuondoa ukabila ambao umepangwa kimkoa na kiwilaya. Walisema mfumo wa mikoa na wilaya ambao ulianza mwaka 1962 ulifanywa kikabila. 


Alisema chama chake kinapendekeza Tanganyika iwe na majimbo yasiyozidi 10 na kwa kuanza na majimbo tisa ambayo ni Nyanza Magharibi ambalo litakuwa na mikoa ya Kagera, Geita na Shinyanga na Nyanza Mashariki lenye mikoa ya Mara, Mwanza na Simiyu. Jimbo la Ziwa Tanganyika litakuwa na mikoa ya Kigoma, Katavi na Rukwa, Jimbo la Kati litakuwa na mikoa  ya Tabora, Dodoma, Singida na Iringa. Jimbo la Kaskazini litakuwa na mikoa ya Kilimanjaro, Arusha na Manyara. Pwani Kaskazini iwe na mikoa ya Tanga, sehemu ya mkoa wa Pwani na sehemu ya mkoa wa Morogoro huku jimbo la Pwani ya Kusini likiwa na mikoa ya Mtwara, Lindi na wilaya za Mafia, Rufiji na Ulanga. Lissu alisema jimbo lingine ni la Mji Mkuu la Dar es Salaam ambalo litakuwa na manispaa tatu za mkoa huo na Nyanda za Juu Kusini lenye mikoa ya Njombe, Mbeya na Ruvuma.


Katika mapendekezo yao walisema majimbo yatasaidia kuwa na raslimali mbalimbali mchanganyiko na pia majimbo hayo yataongozwa na magavana ambao watachaguliwa, “Hapo hakuna kuchagua mtu kwa misingi ya kabila, kwani jimbo moja litakuwa na makabila zaidi ya mawili.”


CUF
, kwa upande wake ilipendekeza kuwapo Katiba tatu zitakazoongoza serikali za Tanganyika, Zanzibar na ya Muungano.

Akizungumza baada ya kutoa maoni yao katika  Tume ya Katiba iliyokuwa chini ya Mwenyekiti wake Jaji mstaafu Joseph Warioba, Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahimu Lipumba alisema, kila nchi inapaswa iwe na Katiba ambayo itawawezesha wananchi husika kuendesha mambo yao.


Alisema pia kuwapo Katiba mama ambayo ni Hati ya Muungano ikizungumzia na kusimamia mambo ya Muungano ambayo pande mbili zitakuwa zimekubaliana.


Lipumba alisema kuwapo serikali tatu, kutatoa nafasi kwa Serikali ya Tanganyika kusimamia mambo yake ambayo kwa sasa yanasimamiwa na Serikali ya Muungano na Zanzibar kutoona kuwa wanaonewa.


“Tukisema iwe serikali moja hilo kwa Zanzibar halikubaliki, tukiendeleza mfumo uliopo, bado una matatizo, hivyo ni heri kukawa na serikali tatu; ya Muungano itakuwa ikisimamia masuala ya Muungano. Kwa mfano tunataka masuala ya ulinzi na Jeshi la Polisi yawe ya Muungano, na pia Mambo ya Nje isipokuwa ushirikiano wa kiuchumi ni lazima kila nchi isimamie kivyake. Mambo ya kilimo, michezo na mengine kila serikali isimamie kivyake,” alisema.


Akizungumzia uchaguzi, Lipumba alisema wamependekeza kuwapo kwa mgombea binafsi katika urais na rais apatikane kwa kupata zaidi ya asilimia 50 ya kura halali zilizopigwa, ikiwa ni tofauti na utaratibu wa sasa ambapo mshindi anapatikana kwa idadi kubwa ya kura.


Alisema katika ubunge na udiwani utumike mfumo wa kura za uwiano ambako kura zinapigwa kwa chama na chama kitatoa uwakilishi kulingana na asilimia ya kura ambazo kimepata na kuwa utaratibu huo utafanya kuwepo uwiano sawa wa kijinsia.


“Hatutaki viti maalumu, mfumo wa kura za uwiano zitafanya kuwapo na uwakilishi sawa bungeni na kwenye nafasi za madiwani. Kinachotakiwa kutoa orodha ya wagombea wake katika mkoa na wananchi watapigia kura chama na kitakachopata kura nyingi kitatoa wabunge zaidi. Hapa kura itakuwa na thamani.” alisema Lipumba na kuongeza: ‘Endapo mbunge au diwani ametangulia mbele za haki, chama kilichokuwa kinashikilia jimbo hilo kichague mwingine ili kupunguza gharama za uchaguzi mdogo.”


Aidha, kuhusu uteuzi wa Tume ya Uchaguzi, Lipumba alisema wajumbe wateuliwe kutokana na mapendekezo ya vyama vya siasa vyenye wabunge, asasi za kiraia zinazoshughulika na uongozi na jamii, Msajili wa Vyama, uwakilishi wa wanawake, wazee, vijana, walemavu, mwakilishi mmoja wa dini ya kiislamu na mmoja wa kikristo ambao ndio watachagua mwenyekiti na makamu wao.


Akizungumzia mfumo wa serikali, Lipumba alisema madaraka ya rais ni lazima yadhibitiwe na Bunge ambapo uteuzi wowote wa rais ukiwamo wa mawaziri ni lazima uthibitishwe na Bunge. 


“Rais anapoteua mwanasheria wa serikali, mkaguzi wa fedha za serikali, jaji mkuu, mkuu wa majeshi au mawaziri uteuzi wao lazima uthibitishwe na bunge. Hii itasaidia watu kuacha kugombea ubunge ili waje kuwa mawaziri, bali wagombee ili wawatumikie wananchi,” alisema


Lipumba alisema pia wametaka katiba itaje idadi kamili za wizara ambazo zinatakiwa kuwa kati ya 15 hadi 20 na kama kunahaja ya kubadili basi bunge lihusishwe. “ Hii itapunguza mzigo kwa serikali.”


Naibu Katibu wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Casmir Kyuki alipoulizwa sababu ya kufanya mikutano hiyo kwa siri bila wanahabari, alisema uongozi wa Tume hiyo umeamua kwa nia nzuri kuwa mikutano yake na makundi  mbalimbali iwe ya ndani.


“Hii ni kwa sababu Tume inataka kupata ufafanuzi wa baadhi ya mambo kutoka wa viongozi wa makundi hayo, ndio maana utaona kuwa hata utaratibu wa kukaa nao ni tofauti na ule tuliokuwa tunautumia mbele ya wananchi,” alisema Kyuki.


Alisema miongoni mwa mambo ambayo wajumbe wanawauliza viongozi wa makundi hayo ni misimamo ya vyama vya siasa pamoja na baadhi ya maoni ambayo tulipata kutoka kwa wananchi ambayo tunaamini kuwa yametokana na misimamo ya vyama vya siasa.

Alisema licha ya vyama vya siasa makundi mengine ambayo yataitwa na Tume ni jumuiya za kidini, asasi za kiraia, viongozi wa kiserikali, vyama vya kitaaluma, sekta binafsi, vyama vya wafanyakazi, wamiliki na waandishi wa habari.

“Hatuamini kuwa kufanya mikutano hii kwa siri tunawanyima wananchi uhuru wa kupata habari, ila kwa kuwa wananchi walishatoa, Tume inahitaji ufafanuzi wa baadhi ya mambo kutoka kwa viongozi wa makundi haya,” alisema.


Kuhusu vyama vitakavyoitwa, Kyuki alisema ni 20 vyenye usajili wa kudumu na kuwa CCM ambayo jana wajumbe wake walifika mbele ya Tume, ilishatuma maoni yake mwaka jana, lakini jana waliuondoa waraka wa kwanza na kuwasilisha mpya.


---

via gazeti la Habari Leo

No comments:

Post a Comment