Monday, January 7, 2013

NYARA ZA SERIKALI KIBAO ZANASWA ARUSHA

Mtuhumiwa wa nyara za serikali Peter Laurence (mwenye kofia) akiwa na maofisa wa jeshi la polisi chini ya ulinzi, eneo la Kisongo mtaa wa Mateves nje kidogo ya jiji la Arusha baada ya kukamatwa na shehena ya nyara za serikali nyumbani kwake.
 JESHI la polisi mkoani Arusha limekamata shehena kubwa ya nyara mbalimbali za serikali zilizokuwa zimehifadhiwa kwenye ghala maalumu eneo la Matevesi Kisongo nje kidogo ya jiji la Arusha, zikiwa tayari kusafirishwa nje ya nchi.

Nyara hizo ni pamoja na ngozi za simba, chui na mamba, meno ya tembo, vichwa vya nyani, swala na nyati, pembe za kifaru na zingine nyingi ambazo jeshi la polisi linaendelea kuzitambua pamoja na mfuko wa kuhifadhia silaha.

Sambamba na hilo, jeshi hilo limemtia mbaroni mtuhumiwa wa nyara hizo aliyetambulika kwa jina la Peter Leurence (55) mkazi Ngaramtoni ya chini, ambaye alikuwa amezihifadhi kwenye maboksi zaidi ya 20, kwenye nyumba yake iliyopo eneo hilo.

Kwa mujibu wa kamanda wa polisi mkoni Arusha, Liberatus Sabas kukamatwa kwa nyara hizo kumetokea jana majira ya saa 6.30 usiku wa kuamkia leo  eneo la Kisongo mtaa wa Mateves baada ya kupata taarifa kutoka kwa raia wema.

Kamanda Sabas alisema kuwa baada ya jeshi hilo kupata taarifa za siri majira ya saa 5 asubuhi, walifika eneo la tukio majira ya saa 7 mchana na kupata upinzani mkubwa kutoka kwa walinzi wa wanaolinda eneo hilo kwani waliwanyima kuwapa maelekezo ya kumpata mmiliki wa nyumba hiyo.

Hata hivyo alisema, askari hao waliamua kumuweka chini ya ulinzi kwa kumshurutisha mlinzi mmoja iliaweze kuwapa ushirikiano ambapo aliwapatia namba za simu za mtuhumiwa ambaye aliwaambia yupo Magugu mkoani Manyara na angefika saa 12 majira ya jioni.

Baada ya mtuhumiwa kufika, jitihada za kufanya upekuzi zilifanyika chini ya polisi wenye silaha za moto na ndipo walipokuta shehena kubwa ya nyara za serikali zilizokuwa zimehifadhiwa kwenye ghala maalum na kufungwa kwenye maboksi  tayari kwa kusafirishwa kwenda kusikojulikana.

Alisema kuwa polisi waliamua kumweka mtuhumiwa chini ya ulinzi hadi kulipokucha.

Aidha, kamanda Sabas alisema kuwa kesho yake polisi waliendelea kufanya upekuzi na kuzikuta nyara hizo.

Jeshi hilo linaendelea kumshikilia mtuhumiwa huyo pamoja na watoto wake wawili waliokutwa wakiishi kwenye nyumba hiyo kwa mahojiano na watafikishwa kwenye mahakama pindi upelelezi wa tukio hilo utakapokamilika.

No comments:

Post a Comment