Kocha Mkuu wa Taifa Stars, Kim Poulsen (pichani) ametaja kikosi cha
wachezaji 21 kitakachoingia kambini Jumapili (Februari 3 mwaka huu) kwa
ajili ya mechi ya kirafiki dhidi ya Cameroon (Indomitable Lions).
Akizungumza na Waandishi wa
Habari, Dar es Salaam leo, Kim amesema mechi dhidi ya Cameroon itakuwa
kipimo kizuri kwake kwa sababu ni sehemu ya maandalizi kabla ya kucheza
mechi ya mchujo ya Kombe la Dunia dhidi ya Morocco itakayofanyika Machi
mwaka huu.
“Itakuwa mechi ngumu na kipimo sahihi kwetu. Tuko tayari, tutacheza kwa
staili yetu kwa sababu ni sehemu ya maandalizi kabla ya mechi dhidi ya
Morocco. Ni mechi nzuri kwa sababu wachezaji wameonyesha wako tayari.
“Tumetoka kucheza dhidi ya Zambia na Ethiopia. Lengo ni Taifa Stars
kucheza fainali za AFCON 2015, kwa hiyo mechi dhidi ya Cameroon ni
sehemu ya mipango yetu kuhakikisha tunafika huko,” amesema Kim ambaye
amerejea nchini juzi kutoka Afrika Kusini kuzifuatilia timu za Morocco
na Ivory Coast zilizo kundi moja na Tanzania katika mechi za mchujo za
Kombe la Dunia.
Taifa Stars inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager itacheza na
Morocco, Machi 24 mwaka huu Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. Stars
inashika nafasi ya pili katika kundi lake nyuma ya Ivory Coast
inayoongoza. Timu nyingine katika kundi hilo ni Gambia.
Wachezaji aliowaita kwenye kikosi chake ni makipa Juma Kaseja (Simba),
Mwadini Ali (Azam) na Aishi Manula (Azam). Mabeki ni Erasto Nyoni
(Azam), Nassoro Cholo (Simba), Aggrey Morris (Azam), Nadir Haroub
(Yanga), Kelvin Yondani (Yanga), Shomari Kapombe (Simba) na Issa Rashid
(Mtibwa Sugar).
Viungo ni Amri Kiemba
(Simba), Simon Msuva (Yanga), Frank Domayo (Yanga), Shabani Nditi
(Mtibwa Sugar), Salum Abubakar (Azam), Khamis Mcha (Azam), Athuman Idd
(Yanga) na Mwinyi Kazimoto (Simba). Washambuliaji ni Mrisho Ngasa
(Simba), na Mbwana Samata na Thomas Ulimwengu wanaochezea timu ya TP
Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC).
Boniface Wambura
Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)
No comments:
Post a Comment