Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Leodegar Tenga akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es salaam leo.
DAR ES SALAAM, Tanzania
Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Leodegar Tenga
amewataka waombaji uongozi ambao hawaridhiki na uamuzi wa Kamati ya
Rufani ya Uchaguzi kutafuta haki yao kwa mujibu wa taratibu zilizopo.
Akizungumza na Waandishi wa Habari jijini Dar es Salaam leo (Februari 16
mwaka huu) mchana, Rais Tenga amesema TFF ni moja ya taasisi ambazo
zina utaratibu unaoeleweka kwa wadau wake.
“Wote
tunafahamu taratibu ambazo tumejiwekea juu ya wagombea wetu
wanachaguliwaje. TFF ni moja ya taasisi ambazo zina utaratibu
unaoeleweka. Hii ni kuanzia wilayani. Kama kuna tatizo zipo njia za
kufuata.
“Katika
mchakato wa uchaguzi wengine wanafanikiwa, wengine wanaachwa. Wameachwa
kwa sababu zilizotolewa na Kamati ya Rufani ya Uchaguzi. Ambaye
haridhiki anafuata taratibu tulizojiwekea. Atafute haki yake kwa mujibu
wa taratibu,” amesema.
Rais Tenga amesisitiza kuwa kikatiba hana uwezo wa kuingilia uamuzi
unaofanywa na kamati ambazo ameziunda, kwani utawala bora ni kusimamia
kanuni ambapo wanaofanya uamuzi lazima waweke wazi sababu za uamuzi
waliofikia.
Amesema ambao
hawakubaliani na uamuzi wa Kamati ya Rufani ya Uchaguzi ya TFF dhidi
yao wana njia tatu za kufuata. Njia hizo ni kuiomba Kamati ya Rufani ya
Uchaguzi ipitie uamuzi iliofanya (review), kuandika Shirikisho la
Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) kuomba liingilie au kwenda Mahakama
ya Usuluhishi ya Michezo (CAS).
“Hata ukiweka
ngazi nne, mtu akiathirika ataona ameonewa tu. Kwa Katiba yetu hapa
(Kamati ya Rufani ya Uchaguzi) ndiyo mwisho. Hakuna chombo kingine.
Ukiwaomba FIFA waingilie, watakuja na tutawaeleza mchakato wote
ulivyokwenda. Tunapenda kuwahakikishia hawa (waathirika) kuwa kwa
maslahi ya mpira wa miguu tutasaidia katika hilo wapate haki,” amesema
Rais Tenga na kuongeza kuwa tayari waathirika wawili wa uamuzi wa Kamati
ya Rufani ya Uchaguzi wameomba marejeo (review) kwenye kamati hiyo
hiyo.
Amesema TFF
imelazimika kuzungumzia suala hilo kwa sababu limekuwa likizungumzwa
kinazi zaidi wakati taratibu ziko wazi, hivyo kwa maslahi ya mpira wa
miguu ni vizuri taratibu zikafuatwa.
“Nawaomba washabiki wa mpira wa miguu, tumejenga chombo hiki (TFF) kwa
muda mrefu.
Bado tunaomba
watu watusaidie, kwa hiyo matusi hayawezi kubadili kitu.
Tunachowahakikishia ni kuwa, mtu anapoomba msaada tutampa kutafuta haki
yake.
“Hizi ni kamati huru, lazima ziheshimiwe.
Ukianza
kuziingilia utakuwa umeua mpira wa miguu. Uongozi ni utumishi,
tusionekane tunagombana. Huu si ubunge, mbunge anachaguliwa anakwenda
kulipwa mshahara.
Mjumbe wa
Kamati ya Utendaji ya TFF halipwi mshahara. Tusirudi kwenye matusi,
tulishaondoka huko,” amesema.
Kuhusu mabadiliko ya Katiba yaliyofanyika kwa njia ya waraka, Rais Tenga
amesema yamefanyika kwa mujibu wa taratibu, na haikuwa siri.
Maeneo
yaliyofanyiwa marekebisho ilikuwa ni lazima, kwani mengi yalikuwa ni
maagizo kutoka FIFA na Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF).
Amesisitiza kuwa mabadiliko hayo yamefuata taratibu na hakuna
udanganyifu katika hilo, kwani ridhaa ya kutumia waraka iliombwa, na
Mkutano ni watu ambao ndiyo wamepitisha mabadiliko hayo.
“Mkutano Mkuu ni watu, si kikao.
Katika dunia
ya leo mikutano inafanyika kwa tele conference, si lazima watu wakutane
sehemu moja,” amesema na kuongeza kuwa mabadiliko hayo yalipitishwa kwa
kura 70 dhidi ya 33 zilizokataa.
Kuhusu Kanuni kusainiwa kabla ya Katiba, Rais Tenga amesema tarehe ya
kuanza kutumika Katiba ni siku ridhaa ilipopatikana, na si siku mhuri wa
Msajili ulipopigwa.
Mabadiliko ya Katiba yalipita Desemba 15 mwaka jana, Kanuni zilisainiwa Januari 7 mwaka huu.
No comments:
Post a Comment