Mwenyekiti wa Chadema taifa,
Freeman Mbowe akiongea na viongozi wa Chadema wa
mikoa ya Nyanda za Juu Kusini katika ukumbi wa mkapa jijini Mbeya
|
CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo
(Chadema) kimesema kuwa kimeamua kuanza kutekeleza sera yake ya kuongoza kwa
majimbo sasa ili kuongeza nguvu ya mapambano na harakati za kuhakikisha
wanafanikisha malengo yao ya kushika dola mwaka 2015, badala ya kuendelea
kutumia mfumo wa zamani ambao ilikuwa rahisi kudhibitiwa na serikali ya Chama
cha Mapinduzi (CCM) .
Kadhalika, chama hicho kimesema
hakitampokea mwanachama yeyote wa Chama Cha Mapinduzi atakayekosa nafasi ya
kugombea kwenye chama chake na kutimkia Chadema katika dakika za mwisho
kuelekea kwenye Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2015.
Mwenyekiti wa Chadema taifa,
Freeman Mbowe aliyasema hayo wakati akizungumza na viongozi wa Chadema wa
mikoa ya Nyanda za Juu Kusini ikiwa ni maandalizi ya kuzindua kanda yake kwenye
kanda hiyo.
Alisema kuwa mfumo wa zamani
ambao mambo yote ya harakati za chama hicho yalianzia makao makuu ya chama,
ulikuwa ni rahisi kudhibitiwa na dola ya CCM kwa kuwa walikuwa wakiwavizia
viongozi wa kitaifa wanapotoka nje kwenda kuendesha harakati wanawapiga mabomu,
kuwakamata na kuwafungulia kesi mahakamani.
“Tunataka dola ikusubiri viongozi
wa kitaifa watoke makao makuu ili wawadhibiti, wasikie mapambano yanatokea
kwenye kanda zetu kama hii ya Nyanda za Juu Kusini, kanda ya Magharibi na
nyinginezo,” alisema Mbowe.
Alisema kuwa katika mabadiliko
hayo pia Chadema inaachana na siasa za kiuanaharakati na badala yake inaanza
kujikita kwenye siasa za maandalizi ya kushika dola.
Akizungumzia utaratibu wa baadhi
ya wanachama wa vyama vingine, kikiwemo chama tawala CCM kukimbilia ndani ya
chama hicho baada ya kutoswa kwenye nafasi za uchaguzi, Mbowe amesema kuwa
kuanzia sasa Chadema hakitampokea mwanachama yeyote wa aina hiyo.
Mbowe alisema kuwa Chadema hivi
sasa ipo kwenye maandalizi makubwa ya kunyakua dola mwaka 2015 na hivyo inao
wajibu wa kuwaandaa wanachama wake ipasavyo ili kiweze kuwa na wagombea wazuri,
imara na wenye uwezo wa kuwezesha chama hicho kupata ushindi mkubwa.
“Kama kuna mtu leo anakula
matunda ya ufisadi ndani ya Chama Cha Mapinduzi akidhani kuwa atahamia Chadema
kwa kuwa ana fedha za kununua kura za maoni, ameula wa chuya, hatutampokea mtu
wa aina hiyo, ” alisema Mbowe.
Alisema kuwa kuanzia sasa Chadema
itawapokea wanachama kutoka vyama vingine baada ya kuwapima uadilifu wao,
kuchunguza historia yao na utayari wao wa kutumika ndani ya chama ili waweze
kupata wanachama na viongozi wazuri watakaokisaidia chama kushika dola mwaka
2015.
Alisema kuwa Chama Cha Mapinduzi
kimekuwa kikitumia mbinu mbalimbali za kukisambaratisha Chadema, ikiwa ni
pamoja na kuwatumia mamluki ndani ya chama, lakini kutokana na uimara wa
Chadema mbinu hizo zimekwama na Chadema inasonga mbele.
Mbowe ambaye pia ni kiongozi wa
Kambi ya Upinzani Bungeni alisema kuwa yeye pamoja na wapambanaji wenzake
wametumia zaidi ya miaka 20 kuijenga Chadema na kuipa nguvu kisiasa hadi hapo
na hivyo hatakubali kuruhusu chama hicho kihujumiwe au kusambaratishwa kwa
namna yoyote ile.
Alisema kuwa ikiwa wana-Chadema
wataruhusu Chadema ife leo, itawachukua tena miaka 20 mingine kuijenga na
kuifikisha mahali iilipo hivi leo.
Mbowe alitolea mfano wa vyama vya
siasa vilivyowahi kupata nguvu na umaarufu mkubwa wa kisiasa nchini kama vile
Chama cha Wananchi, CUF, NCCR – Mageuzi na TLP ambavyo alidai kuwa CCM
illifanikiwa kuvizima na kuwa hata vyenyewe itavichukua muda mrefu usiopungua
miaka 20 kurejesha umaarufuvilivyokuwa nao.
|
No comments:
Post a Comment