MKOA wa Dar es Salaam leo saa 6 usiku unakuwa wa kwanza kuzimiwa mitambo ya analojia ya utangazaji wa televisheni kwa ajili ya kupokea mfumo mpya wa digitali.
Hatua hiyo ya kuhama kutoka analojia kwenda digitali ni utekelezaji wa makubaliano ya nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, Profesa Makame Mbarawa katika hotuba yake ya jana kuashiria uzimaji wa mitambo ya analojia, alisema uzimaji kwa zamu unalenga kuepusha usumbufu kwa wananchi.
Mbarawa alisema kuwa mchakato huo wa uzimaji wa mitambo utafanyika tena Januari 31, 2013 na mikoa itakayohusika ni Dodoma na Tanga. Mkoani Mwanza mitambo itazimwa Februari 28, 2013 na Kilimanjaro (Moshi) na Arusha mitambo itazimwa Machi 31, 2013.
Kwa mujibu wa Waziri, mkoa wa saba kuingia kwenye mfumo wa digitali utakuwa Mbeya ambao mitambo itazimwa Aprili 30, 2013. Utaratibu wa kuzima mitambo ya analojia utakuwa kwa maeneo yenye matangazo ya digitali na kwa yasiyo na miundombinu ya digitali hayatazimwa.
Taarifa ya Waziri inaonesha kwamba miundombinu ya mitambo ya digitali imeenea katika mikoa minane pekee. Mabadiliko hayo yanahusu matangazo kwa njia ya utangazaji wa satelaiti, waya (cable) na redio.
“Tunawataka wananchi wasitupe televisheni zao za analojia bali wanunue ving’amuzi ili kupata matangazo ya digitali,” alisema na kuongeza kwamba Serikali inatarajia kupata ushirikiano kutoka kwa wadau wa sekta ya utangazaji na wananchi katika kipindi cha uzimaji wa mitambo ili kufanikisha kazi hiyo.
Aidha imeelezwa kwamba watoa huduma za miundombinu ya digitali wamejipanga kusimika mitambo hiyo katika mikoa mingine minane ndani ya miezi minane ijayo.
Kampuni zenye leseni za kusambaza ving’amuzi zimetajwa kuwa zimejipanga kuhakikisha vinakuwepo vya kutosha. “Na vingine vimeagizwa ili kukidhi mahitaji ya baadaye,” alisema Waziri Mbarawa kupitia hotuba yake
No comments:
Post a Comment