Monday, January 7, 2013

WASANII WATAKIA KUSHIRIKI TAMASHA LA SANAA LA AFRIKA MASHARIKI

Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo imewataka wasanii nchini kujitokeza kushiriki tamasha la sanaa na Utamaduni la Jumuiya ya Afrika Mashariki ambalo litafanyika nchini Rwanda mwezi ujao.
 
Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, kwa Niaba ya Katibu Mkuu, afisa Utamaduni Mwandamizi wa Wizara hiyo Makao makuu, Habibu Mohamed amesema tamasha hilo lijulikanalo kama JAMAFEST litafanyika kwa siku nane kuanzia Februari 9 hadi 16 mwaka huu.
 
“ Kwanza napenda kuwajulisha kuwa tumepata mwaliko wa kushiriki Tamasha la Sanaa na Utamaduni la Jumuiya ya Afrika Mashariki, ‘JAMAFEST – 2013’  ambalo ni tamasha muhimu sana kwa wasanii wetu kushiriki katika hatua ya kutangaza na kuuza kazi zao katika soko la sanaa la Afrika Mashairiki,” amesema Habibu.
 
 Amesema kutokana na mwaliko huo wa Jumuiya, Wizara inatoa mwaliko kwa wasanii, asasi, vikundi, wabunifu wa mavazi na kampuni kwa hapa nchini, ambao zitaweza kufanya maonesho na kuuza bidhaa na huduma za Sanaa na Utamaduni, katika mabanda ya Tanzania kutuma maombi yao wizarani ambapo mwisho wa kutuma maombi ni Januari 25.
 
Amesema washiriki watajigharamia nauli ya kwenda na kurudi, chakula na malazi katika kushiriki tamasha hilo.

No comments:

Post a Comment